Si bure, Manji ana lake Yanga


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version
Yussuf Manji

"Si Bure, Yussuf Manji ana lake Yanga." Ndivyo ninavyolazimika kuamini kutokana na mambo kadhaa yaliyojitokeza tangu bilionea huyo alipotia mguu Yanga mwaka 2006.

Narudia tena, ndivyo ninavyoamini, hivyo siwalazimishi wengine kuungana nami. Wanaweza kunipinga.

Imani yangu inapata nguvu kutokana na orodha ndefu ya mambo ninayoamini mengi yapo kama danganya toto.

Labda nianze kwa kumpongeza Manji kutokana na kujitoa kuisaidia kwa kiasi kikubwa klabu hiyo kiasi cha miaka hii miwili kuonekana watu wa daraja jingine kabisa, wasio na chembe ya shida kwa mahitaji ya kila siku.

Miayo ya njaa haipo tena Yanga, wanapewa wanachotaka, kuanzia posho, mishahara, usafiri, maandalizi ya mechi muhimu na hata fedha za usajili.

Anayafanya hayo yote bila kupiga danadana, lakini cha kushangaza ni kwamba, mengi aliyoyaahidi awali, ndiyo anayoyapiga danadana, ingawa hayakuhitaji kiasi kikubwa cha fedha kama anachokimwaga.

Kwa mfano, Manji aliahidi, tena siku nyingi kwamba angelifanyia ukarabati mkubwa jengo la makao makuu ya klabu yaliyopo katika makutano ya mitaa ya Twig ana Jangwani.

Mkwara ulianza kwa kupelekwa masinki kadhaa, yakapigwa picha na zikachapishwa kwenye vyombo vya habari kwamba, mambo yameanza.

Lakini mpaka leo hii, hakuna cha ukarabati, wala nini, ni buibui tu ndio waliotanda katika vyumba zaidi ya 20 katika jengo hilo la ghorofa tatu.

Naamini, kama Manji angeitimiza ahadi hii, angekuwa ameisaidia sana Yanga, kwani timu ingepata makazi au kambi ya kudumu na hasa kwa wachezaji wa kigeni wanaopangishiwa nyumba ilhali kuna eneo zuri la kuishi, kama viongozi na mfadhili huyu wangeona mbali.

Badala yake, kwa mradi ambao haungehitaji hata sh milioni 60, umeachwa kuwa hadithi, lakini mamilioni kwa mamilioni yakimwagwa kila kukicha kwenye hoteli ya Lamada, Ilala jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kambi ya timu hiyo.

Iliwahi kuelezwa kwamba, kwa siku, Yanga inatumia hadi sh milioni 2.6 kwa malazi na chakula pekee hotelini hapo.

Je, huku ndiko kuisaidia Yanga au kuitia ujinga ikiamini iko matawi ya juu ilhali Manji akibandua mguu inarudi chini, tena chini zaidi kwa sababu haitakuwa na uhakika hata wa kuilaza timu kwenye hoteli ya sh 20,000 kwa siku?

Kama mamilionui haya yangeingizwa kwenye ukarabati wa jengo na kuweka samani vyumbani, Yanga si ingeweza kunufaika na kuokoa fedha nyingi za kambi kwa miaka nenda miaka rudi?

Kama hali haiku hivyo, Manji anaitakia mema Yanga au anataka awapumbaze ili kila kukicha wampigie magoti? Hilo ni moja.

Manji huyu huyu, aliahidi kuukarabati uwanja wa Kaunda ambao si haba, ukikarabatiwa unaweza kuingiza hata mashabiki 10,000 kwa wakati mmoja.

Kwa hakika, huo waweza kuwa ukombozi mkubwa kwa Yanga, kwani kwa idadi hiyo, kama ni katika mechi ya Ligi Kuu kwa mfano, ikiweka kiingilio cha shilingo 3,000 tu kwa kila kichwa, itaweza kuvuna mapato ya sh milioni 30.

Je, mara ngapi Yanga imeweza kuingia kiasi hicho cha fedha pale Uwanja wa Taifa? Na ikipata, mlolongo wa makato unawaacha na kiasi gani? Akili ni nywele.

Zilianza mbwembwe Jangwani kwa kupelekwa wataalamu, likafuatia greda, likaacha tope, lakini hadithi ikaishia hapo, si Manji wala viongozi wa Yanga wanaoelezea hatima ya uwanja huo, zaidi ya kuwaona wakihamisha timu kila kukicha kwenye viwanja tofauti kwa ajili ya mazoezi.

Kama viongozi waasisi wa klabu hii waliona mbali na kuamua kuwa na uwanja wao wenyewe, inawezekanaje viongozi wa sasa, wenye kuzungukwa na matajiri kama Manji washindwe kuyaenzi mema ya wakati huo?

Mbali ya kuwa chanzo kikubwa cha mapato, kwa klabu ni heshima kubwa sana kuwa na uwanja na vitegauchumi vyake. Manji analijua hili, na katika moja ya mikakati yake ya kutaka kuifanya Yanga ijitegemee, tunadhani angeanzia huko, lakini yupo kimya.

Tunachosikia ni kumwaga fedha za usajili, kuipeleka timu Ulaya na mbwembwe ambazo mwisho wa siku Yanga haitakuwa na kumbukumbu ya kudumu, hasa katika ustawi wa klabu.

Au labda atuambie, ana mikakati gani ya kuisaidia Yanga kuweza kujitegemea? Mbona miaka inakatika, lakini hakuna kinachofanyika?

Ninavyoamini mimi ni kwamba, kwa mtu mwenye mapenzi ya kweli au dhamira hasa ya kusaidia, ingekuwa kuitafutia timu mikakati ya kusimama kwa miguu yake yenyewe.

Hatusikii wahenga wakisema; Mwenye Njaa usimpe samaki, bali mfundishe jinsi ya kuvua?

Kwa mtaji wa kuipa Yanga kila kitu, badala ya kuijengea misingi ya kiuchumi, Yanga inaisaidia au anaidumaza?

Hapa ndipo panapotia shaka, kiasi cha kunifanya niamini kwamba, pengine Manji ana ajenda yake ya siri ndani ya Yanga, lakini si mapenzi ya dhati yanayomsukuma kuwa katika klabu hiyo anayoimwagia fedha kila kukicha.

Wakati umefika Manji awafanyie Wanayanga mambo yatakayoacha alama kwa ustawi wa klabu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: