Si kazi ya serikali kuchuja habari


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version

MAPEMA mwezi huu makachero wa Jeshi la Polisi nchini walivamia na kupekua ofisi za gazeti hili na nyumbani kwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Saed Kubenea, wakimtuhumu kuchukua akaunti za wateja wa Benki ya NBC na kuzichapisha katika gazeti lake.

Huu ni mtihani mwingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini katika kipindi hiki kigumu cha taifa kuzama katika lindi la ufisadi, kuporomoka kwa maadili ya taifa na nchi kunyemelewa na ukoloni mamboleo.

Uhuru wa mawazo na wa kujieleza ni haki ya raia. Licha ya kwamba sehemu kubwa ya wajibu huu inatekelezwa na vyombo vya habari, vyombo hivi pia ni sauti ya wasio na sauti na waliofungwa midomo.

Ni kwa sababu hii tunatoa tahadhari kwa vyombo vya dola visije vikatumika vibaya, si tu kwa tukio hili, bali pia kwa matukio mengine dhidi ya vyombo vingine vya habari. Kufanya hivyo, kunaweza kutafsiriwa kuwa ni kubana demokrasia na kupora haki za wananchi.

Vitendo kama hivi vinatufanya tuonekane kama watu wanaoishi karne ya 17 na kabla, ambapo adhabu kali ilitolewa kwa waliohoji vitendo au mamlaka ya Wafalme huko Ulaya.

Kwa mfano, mnamo karne ya tisa, Mfalme Alfred wa Uingereza aliagiza kuwa kila mtu aliyeihoji serikali akatwe ulimi ambao ndio ulikuwa nyenzo pekee ya mawasiliano kwa njia ya kujieleza.

Ulimi wa sasa ni vyombo vya habari. Kuibuka kwa uchapishaji wa habari kulikuwa tishio jipya kwa watawala, ikabidi magazeti yasajiliwe kwa lengo la kudhibitiwa.

Ni mwaka 1689 chini ya utawala wa Malkia Mary, Uingereza ilipotunga Sheria ya kulinda Haki za binadamu (Bill of Rights) na kulipa Bunge ukuu (sovereignty) na uhuru wa Wabunge wa kujieleza.

Ni hapo pia uhuru wa kila mtu wa kutoa mawazo moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari ulitambuliwa.

Huko Marekani, uhuru huo ulimea na kukua kwa nguvu baada ya kesi ya jinai dhidi ya mchapishaji John Peter Zenger, mwaka 1735.

Tangu hapo, Sheria ya makosa ya "Uchochezi" ilibakia kwa jina tu hadi ilipofutwa na Rais Thomas Jefferson, mwaka 1801.

Nchini Uingereza, Sheria dhidi ya "habari za uongo" (False News Offences) ilifutwa mwaka 1887. Lakini sisi tu, kinyume chake. Ikiwa sasa ni karibu miaka 50 ya uhuru tunapelekwa kule wenzetu walikwishatoka zaidi ya miaka 120 iliyopita.

Kama huu sio uzuzu ni nini? Uhuru wa kujieleza ni msingi mkuu wa kuelezea matatizo mapya yanayoikabili jamii, na ni njia pia ya kuweka wazi udhaifu wa sera kandamizi na athari zake kwa jamii.

Kama kweli tumeridhia demokrasia, uhuru na haki za binadamu, soko, siasa na uchumi huria kwa viwango hivyo, iweje leo tunaendelea kudhibiti uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari?

Au tunaogopa kuambiwa ukweli kwamba "mfalme yuko uchi" na kwa sababu tu ukweli unauma?

Uhuru wa kujieleza nchini umedhibitiwa na sheria nyingi, lakini hapa nitaeleza sheria mbili unapofikia kiwango cha kuitwa kosa la "uchochezi" - jambo lililofutwa karne ya 18 katika nchi za Magharibi.

Uchochezi (sedition) ni kosa la jinai chini ya Kanuni za Adhabu (Penal Code), na ni kosa pia chini ya Sheria ya Magazeti, Namba 3, ya 1976.

Wakati Sheria hizi mbili zinadhibiti uhuru wa kujieleza kwa kuuwekea mipaka, Katiba ya nchi (ibara 18 ) inafungua mlango wazi.

Kwa kuzingatia matakwa haya ya Katiba, ni maoni yangu kwamba, kile kinachoitwa "uchochezi" ndio uhuru wenyewe wa kujieleza na kutoa maoni.

Tutatoa rejeo kuthibitisha hoja hii. Oktoba 24, 1997, Mhariri wa gazeti la "The Monitor" nchini Uganda, Charles Obo- Onyango-Obo na mwenzake, Andrew Mujuni Mwenda, waliachiwa huru na Mahakana kwa kosa la uchochezi.

Waandishi hawa walichapisha habari yenye kichwa kisemacho: "Rais (Laurent) Kabila aliilipa Uganda dhahabu", kama shukrani kwa Uganda kwa kumsaidia katika vita vya kumng?oa Rais Mobutu Sese Seko.

Licha ya kuachiwa huru, waandishi hao wandamizi walifungua kesi kwenye Mahakama ya Katiba kuitaka itoe ufafanuzi kama Serikali ilikuwa na uwezo na haki ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) kulinda kile kinachoitwa "maslahi ya umma".

Ibara ya 29 ya Katiba ya Uganda ya 1995 ni ibara dada na ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Vivyo hivyo, kosa la "uchochezi" chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai ya Uganda (Penal Code Act), ni kosa dada chini ya vifungu namba 50 na 55 vya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) ya Tanzania, na kifungu 55 cha Sheria ya Magazeti Namba 3 ya 1976.

Katika rufaa yao, baada ya Mahakama Kuu kuitupilia mbali kesi yao, swali lilikuwa kama kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai hakipingani na ibara ya 29 ya Katiba ya nchi hiyo inayotoa kwa mtu na vyombo vya habari uhuru wa kujieleza bila kuingiliwa.

Mahakama katika hukumu yake iliona kuwa kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Uganda kimedumu kabla na baada ya Uganda kuridhia Tamko la Kimataifa juu ya Haki za Binadanu (Bill of Rights), na ni moja ya Sheria za kikoloni za miaka 120 iliyopita nchini Uingereza.

Majaji hao waliongozwa na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu (The African Charter on Human and People?s Rights), na ibara ya 29 ya Katiba ya Uganda inayosemeka kwa maneno sawa na Katiba yetu.

Mahakama ya Rufaa ya Uganda ina hadhi sawa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambapo hukumu zake (precedents) zina ushawishi (persuasiveness) mkubwa katika kufikia uamuzi kwa kesi zinazofanana katika Mahakama za nchi hizi na za Jumuiya ya Madola.

Na kwa kuzingatia kwamba nchi za Afrika Mashariki ni wanachama wa Jumuiya ya Madola zenye kutumia mfumo mmoja wa Sheria (Common Law System), hukumu ya kesi hii ni muhimu kwetu, hasa katika ujenzi wa demokrasia makini.

Tunataka Serikali iviache vyombo vya habari vipige kelele, viwasemee wanyonge, na ikishindwa kufanya hivyo, mawe yatapiga kelele.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: