Siasa ‘zaamtafuna’ Karamagi


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Nazir Karamagi

ALIYEWAHI kuwa waziri wa nishati na madini katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alitumia zaidi ya Sh. 400 milioni katika maandalizi ya mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake hadi Mei mwaka huu, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema Nazir Karamagi, alikuwa tayari ametumia zaidi ya Sh. 500 milioni katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge jimboni mwake kwa shughuli mbalimbali za “maendeleo ya wananchi na jimbo kwa jumla.”

Aidha, katika kipindi cha 26 Julai 2010 hadi 14 Septemba mwaka huu, Karamagi ameripotiwa kutumia jumla ya Sh. 171.6 milioni kwa “shughuli za kijamii” wakati wa kipindi cha kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, pamoja na Karamagi kutumia mamilioni hayo ya shilingi, hakufanikiwa kupenya katika kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya chama chake.

Alishindwa na Jasson Rweikiza, mbunge wa sasa wa jimbo la Bukoba Vijijini na hivyo akawa miongoni mwa vigogo wa kwanza kupoteza ubunge katika uchaguzi uliopita.

Taarifa kwamba Karamagi alitumia kiasi hicho cha fedha bila kuambulia chochote, zimefumuka katika mawasiliano kati ya mwanasiasa huyo na  Rose Luangisa, raia wa Tanzania anayeishi nchini Marekani.

Katika mawasiliano yake na Karamagi, Jumapili ya 9 Mei 2010, Rose anasema, “Napenda unavyosaidia chama chenu ili kipate ushindi wa kishindo. Lakini, it seems you are dishing out a lot of money – hivi, is it worth it au mshahara wote unaopata unarudi kwa wapiga kura na chama chenu? Wow, kwa miaka 5 umetoa zaidi ya million 400.”

Akiandika kwa njia ya kusikitika, Rose anasema, “Can you really recoup this money na ubunge au status inatosha? Hawatakuuliza hizi pesa umezitoa wapi kwa vile mshahara wa mbunge unaeleweka?”

Maoni ya Rose yalifuatia hatua ya Karamagi kutuma kwa dada huyo kile alichoita, “Taarifa ya tathimini ya michango ya mbunge na fursa ya kuwezesha wananchi kiuchumi.”

Kuibuka kwa taarifa za Karamagi kutumia zaidi ya shilingi bilioni moja kusaka ubunge, kunakuja miaka mitatu baada ya mwanasiasa huyo kukiri kusainia nchini Uingereza, mkataba wa kinyonyaji wa uchimbaji madini wa Buzwagi uliopo katika wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Karamagi, ambaye kabla ya kuwa waziri wa nishati na madini alikuwa waziri wa viwanda na biashara, anasema katika taarifa yake kwa Rose, “Fedha zote hizi nilizotumia zimetoka mfukoni kwangu mwenyewe.”

Akimshawishi kusoma kitabu chake juu ya Mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Karamagi anasema, “…umaskini ni mkubwa sana vijijini na watu walio wengi hawajishughulishi na nafasi zinazopatikana. Hii ni hatari…”

Katika mazungumzo yake na MwanaHALISI wiki iliyopita, Karamagi alikiri kutumia mamilioni hayo ya shilingi.

“Mimi nilichangia fedha katika miradi mbalimbali ya chama na katika jumuiya zake jimboni kwangu. Lengo lilikiwa ni kupambana na kero zilizokuwa zinaendelea kuwaumiza wananchi.

“Hicho kiasi unachosema ndicho kilichopo kwenye vitabu, lakini nimetumia zaidi ya kiasi hicho cha fedha. Kuna wakati nilichangia, lakini hakukuwapo na rekodi,” anaeleza.

Kwa mujibu wa mchanganuo wa matumizi, baadhi ya fedha zilitumika kwa ajili ya CCM wilaya, umoja wa vijana (UVCCM) na umoja wa wanawake (UWT).

Mchanganuo unaonyesha alichanga pia mifuko 48 katika kata ya Katoma, alichangia shule ya sekondari Nyakibimbiri, ujenzi wa kliniki Rubafu, Sh. 45.9 milioni kwa shule ya sekondari Kabugaro na misaada mingine huko Ibwera na Mikoni.

Alipoulizwa iwapo bado ana nia ya kugombea ubunge Bukoba Vijijini katika siku za usoni, Karamagi alisema, kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia mambo ya kuwania ubunge kwa vile uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ni mbali kutoka sasa.

Kuhusu kwa nini hasa aliweka fedha nyingi kiasi hicho katika shughuli za kisiasa, Karamagi alisema, hiyo ni kwa sababu jimbo lake la uchaguzi liko nyuma kimaendeleo kuliko majimbo mengine ya mkoa huo.

“Mimi niliamua kutumia mapato yangu yote ya ubunge kwa ajili ya kuendeleza jimbo. Sikuwa nikiishi kwa kutegemea kipato cha ubunge kwa vile nina shughuli zangu nyingine. Kama Bukoba Vijijini ingekuwa imeendelea kama kwingine, labda nisingetumia fedha zote hizo,” alisema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: