Siasa si uongo, ni uongozi mwema


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

KATIKA dunia leo, siasa inatafsiriwa kuwa ni uongo unaotumiwa na kundi dogo la watu wenye nia chafu ya kutaka kutumia madaraka kujinufaisha binafsi.

Uongozi wa kifisadi unawavutia sana watu wenye tamaa ya mali kuingia katika siasa ili wakaibe na kupewa rushwa kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa. Ndiyo sura halisi ya siasa nchini. Badala ya siasa imekuwa “sihasa.”

Nchi imekosa viongozi makini, wabunifu, waaminifu, waadilifu na wazalendo wa kweli. Uongozi mbaya umetengeneza ombwe la uongozi na kuwa kikwazo kikuu cha maendeleo.

Maneno “siasa na uongozi” yana maana sawa kwa maudhui ya makala hii. Nimekumbuka alichokisema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipohutubia kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya CCM na miaka 20 ya Azimio la Arusha mwaka 1987.

Akizungumzia dhana ya uongozi, Mwalimu Nyerere alisema, “uongozi ni kuonyesha njia.”

Kwa maana hiyo, viongozi shurti wafahamu vema matokeo ya uongozi wao. Wasome imani za wanaowaongoza na nyakati zilizopo ili kutambua matumaini ya umma kimaisha.

Ramani na dira ni itikadi ya chama na taifa – imani na ahadi zake kwa umma ambazo viongozi wanapaswa kuzifuata.

Siasa haikamiliki bila itikadi. Kama viongozi hawaijui siasa na itikadi ya chama chao na ile ya taifa lao, labda kwa makusudi, na hasa kwa sababu ya kulinda maslahi binafsi, wajue wanalipeleka ovyo taifa.

Wajue wanalirudisha nyuma taifa ambalo limetarajia watu wake wafaidi matunda ya maendeleo kuliko kushuhudia maendeleo ya vitu. Hii ndiyo ilikuwa imani ya Mwalimu Nyerere.

Uongo na uzandiki vinapofanywa ndio siasa na itikadi, kila kitu kinachohusu maendeleo ya watu kinakufa. Hakutakuwa na tiba bora, elimu bora, maji safi na salama, tija katika uzalishaji wala ajira.

Badala yake, katika safari isiyo na mwelekeo wa kujenga taifa, watu watabaini umasikini, ujinga na maradhi, maadui wakuu wa binadamu, vikishamiri.

Hayo ndio matokeo ya uongozi ulioshindwa kutambua umuhimu wa kutumia raslimali watu kuwaendeleza watu – wananchi.

Kitu kibaya hapa ni kwamba taifa limekosa viongozi wanaojali kuwa watu wana haki ya kupata chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora kwa jumla. Watazalishaje mali wakiwa dhaifu?

Nao “wanasihasa” wanapoulizwa kulikoni, hutoa majibu yaliyojaa kiburi. Utasikia, “vijana warudi vijijini wakajiajiri, wale nyasi, wavivu wa kufikiri, shauri yao hawapendi shule au wanadharau kazi”.

Ni majibu yanayovunja moyo wananchi. Wanajisikia vibaya kwamba hawathaminiwi.

Yapasa viongozi watambue kuwa siasa njema hutatua matatizo na shida za wananchi zikiwemo zinazokwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi na wa familia mojamoja. Siasa mbaya huangusha huduma za jamii.

Kwa kuwa siasa ni uongozi, basi viongozi lazima waongoze kiadilifu, kizalendo na kwa kuzingatia hali halisi ya mambo. Wanapaswa pia kuwa wenye huruma na imani kwa wananchi.

Kazi ya wanasiasa na hasa Afrika ni kuongoza harakati za kukomboa watu kutoka kwenye makucha ya unyonyaji, umasikini na ukoloni mamboleo.

Madhila hayo hayajaondoka Tanzania. Lazima yaondolewe ili kuwapa matumaini wananchi. Kumbe siasa ya nchi haitakiwi kuwa iliyolala au inayojengwa na kucheza mchiriku na bongo fleva.

Siasa iliyolala hukwamisha maendeleo na huchangia umasikini na udhalilishaji wananchi.

Basi mwanasiasa yeyote katika nchi masikini kama Tanzania, anapochaguliwa kuongoza popote, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri. Atumie stadi za uongozi mwema kuonyesha njia.

Tabia ya viongozi kuongoza kwa kufikiria zaidi maslahi binafsi mwiko. Viongozi wa nchi hizi masikini waangalie maisha ya Manabii ambao waliongoza karne za mwanzo za ulimwengu.

Walitumia stadi za uongozi kusimamia haki za waliowaongoza; wanyonge na hata waliokuwa na uwezo. Walitumwa na utashi na imani ya kutumikia Mwenyezi Mungu aliyewaumba.

Walijua kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.

Lakini wanaoifanya kazi ya siasa kwa kuigeuza ni pango la wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji na hata kuua raia, wajiandae kupokea adhabu ya muumba. Yeye anaona kila tendo linalotendwa na viumbe wake wakati wote.

Mafunzo ya wanafalsafa wa Kiyunani – Plato na Aristotle pamoja na upungufu wake, ni mwongozo wa kisiasa katika nchi zinazoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Wanafalsafa hawa wanasisitiza siasa ni msingi bora wa mambo yote.

Wanasisitiza viongozi lazima wawe waadilifu na umma uwe na uwezo wa kuwajibisha viongozi wao wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.

Ni wapi pa kuanzia kufanya mabadiliko ya kisiasa na kuwaondoa “wanasihasa”? Ni watu wenyewe. Muhimu waamke na kutambua wajibu wao katika kuwaweka viongozi wao kwenye mstari ulionyooka.

Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu.

Kupitia siasa safi kila kitu cha kunufaisha wananchi hupatikana. Bali ni muhimu viongozi wanaotarajiwa kufanikisha ustawi wa wanadamu, wapatikane kwa njia ya haki. Watokane na ridhaa ya watu wenyewe wanaotaka kuongozwa.

Hata kwenye vyama vya siasa au vikundi vingine vya kiraia, viongozi lazima wapatikane kwa njia ya haki siyo vurugu na upindishaji wa sheria na taratibu.

Kuhakikisha hayo yanatokea, zile taasisi za kidola zilizokabidhiwa wajibu wa kuchunga nidhamu ya mambo – kama vile vikosi vya ulinzi na usalama, vyombo vya uchunguzi na mahakama, zapasa kutenda kwa dhamira ya kujenga.

Utamaduni wa ubabaishaji na ubaguzi mbele ya sheria usipewe nafasi maana taasisi hizi zina jukumu zito na muhimu la kusimamia haki kutendeka.

Taasisi hizi zikiendesha mambo kwa chuki na ubaguzi unaoelekea kuhifadhi maslahi ya viongozi tu, zitambuwe zenyewe zitakuwa zimetengeneza mazingira ya kuleta vurugu katika nchi.

Uongozi ukishajua unalindwa na taasisi hizi, unazidi kujisahau na kujinufaisha binafsi huku wakibeza haki za raia.

Hapo raia watakuwa wamefikishwa pabaya. Watakataa kustahamili maudhi ya viongozi wao kwa kujua kuwa kuwaendekeza, ni kujimaliza wenyewe na nchi yao. Watachagua kubaki na nchi yao viongozi waondoke.

+447404486150
0
No votes yet