Siasa-mzaha zinazidisha tu mgogoro Zanzibar


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version

INASIKITISHA sana kuona jitihada zilizochukuliwa na vyama viwili hasimu katika siasa za Zanzibar, zimeishia.

Inasikitisha sana kuona tulipo ni kama vile hakuna kiongozi wa kutoa muongozo ili Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), viondoke vilipokwama na kuendeleza mchakato wa utekelezaji wa makubaliano waliyoyafikia.

Inasikitisha kuona vyama hivi vimeacha kusimama katika ukweli au vinaudhihaki na kuendeleza malumbano ambayo kwa namna yeyote hayajengi, zaidi ya kuonyesha jinsi viongozi wa vyama hivi wasivyowajibikaji kwa maslahi ya taifa.

Lakini inasikitisha zaidi kuona matamshi ya viongozi wa vyama hivi tangu pale muwafaka ulipogota, hayaelekei kwenye momentamu waliyofanikiwa kuijenga kabla ya kuanza kujadiliana yale waliyoafikiana kama ajenda.

Nimeanza hivi makusudi maana hali ya mchafukoge inazidi kushamiri kinyume na matarajio ya wananchi wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano, na ulimwengu kwa ujumla.

Niliposikia viongozi wa juu wa CCM wameitisha mkutano na waandishi wa habari Jumapili 11 Mei, niliamini kwamba wanania ya kutegua kitendawili walichokitega kutokana na maamuzi yao walioyafikia katika vikao vyao vilivyofanyika Butiama, mkoani Mara.

Lahaula! Si kwamba sivyo tu, bali ukweli ni kwamba wametengenezea wigo wa kuhifadhi mtego wao. Wamezidisha tu lawama dhidi ya wapinzani wao na kuendeleza upotoshaji mambo.

Kama wanavyofanya CUF kuzunguka nchi katika wanachosema "kuweka shinikizo" ili CCM warudi kusaini Muwafaka, wameuzidisha utata.

Lakini wakati muafaka umekwama, inasikitisha kuona yale matumaini ya kutatuliwa kwa mgogoro wa kisiasa unaolazimishwa kuwepo kwa sababu za kisiasa zisizozingatia uendelevu wa sehemu muhimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yamebezwa.

Hilo ni moja. Linalonikereketa kwa sasa ni kuona panaendelea kukosekana mtu wa kutoa muongozo wa kuondoa mkwamo, badala yake tunasikia kelele na kuendelea kutazama wakati kuna giza nene. Ndio, tupo kizani.

Hapana wa kumtia shemere hapa isipokuwa Rais Jakaya Kikwete, mwenye dhamana mbili kwa suala hili. Ya kwanza ni ya kuwa kiongozi wa jamhuri, lakini ya pili, ni ya kuwa ndiye aliyeahidi Watanzania na Ulimwengu kuwa atasimamia kupatikana "ufumbuzi wa kudumu" wa alichoita "mpasuko wa Zanzibar."

Lakini simshangai na sababu ninazo: yeye ni kada mzuri wa CCM, chama kikongwe ambacho kinaamini kiko katika harakati za ukombozi wa kinaowaongoza badala ya kuwajenga kihali.

Ninachoweza kusema zaidi kumhusu Rais ni kwamba lazima achukue nafasi yake kama kiongozi mkuu wa kila kitu; Taifa na chama tawala, kuondoa hofu za watu zinazozidi kujengeka kutokana na kuona mgogoro wa Zanzibar haujapatiwa ufumbuzi alioahidi.

Katika hali iliopo, rais hakupaswa na wala hapaswi kwa namna yoyote ile, kusimama kama kiongozi wa CCM, chama chenye maslahi makubwa na matamanio ya kuendelea kuongoza Tanzania ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Anapaswa kusimama kama Baba wa Taifa, si baba wa CCM. Haitakiwi afikirie nini chama atokacho kitakosa au nini cha wapinzani wake kitapata iwapo makubaliano yaliyofikiwa yataanza kutekelezwa.

Kwanza muhimu Rais atambuwe anapaswa kutenda kwa morali uleule aliokuwa nao wakati akiahidi, kupitia hotuba ya ufunguzi wa Bunge aliyoitoa 30 Desemba 2005, kuwa atahakikisha "mpasuko wa Zanzibar" unapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Pili, atambuwe ahadi hiyo ingalipo na inasubiri kutimizwa. Utamaduni unaoaminika kwa watu wanaofikiri vizuri, ni kuwa mtu anayetimiza ahadi huitwa muungwana, kinyume chake huchukuliwa mnafiki.

Ieleweke Watanzania wanaojua Rais wao ameahidi kushughulikia mgogoro unaoendelea kuitafuna Zanzibar hadi kuirudisha miaka 100 nyuma kimaendeleo, wanasubiri atangaze ufumbuzi si mkwamo.

Hivi Rais anajisikiaje katika wakati huu ambapo mkwamo wa dhahiri wa utekelezaji makubaliano yaliyofikiwa na vyama vilivyoshiriki majadiliano, unazidi kuimarika?

Akiamua kuendeleza "siasa" badala ya "kutoa muongozo" usozingatia mawazo mgando, ajue kuwa hajasaidia mkwamo kuondoka.

Kila ninapofikiri naona CCM na CUF vimechoka kufikiri. Vimeamua kurudi vilikokuwa kabla ya kuanza kukaa mezani na kuzungumza.

Tatizo liliopo ni kuwa CUF wanajiona walikuwa na haki ya kueleza wanachama wao waliyoafikiana na wapinzani wao, CCM, iwe walishakubaliana nao au laa kuwa yaliyojadiliwa yafikishwe kwa wanachama.

Vivyo hivyo kwa CCM. Nao wanajiona walikuwa na haki ya kujadili makubaliano waliyofikia na wapinzani wao, CUF, na kuyatolea maamuzi, yakiwepo mapya.

Wala sioni kama ni muhimu kulaumu hatua ya makubaliano yaliyofikiwa kutangazwa kwa umma, kama ambavyo sioni ni tatizo kujadili makubaliano na kuyatolea maamuzi, muradi umma upewe ushahidi wa hoja za vyama hivi.

Kwamba uko wapi ukweli kuwa ajenda ya tano ya mazungumzo; ihusuyo "Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa Makubaliano" haijajadiliwa.

Na uko wapi ukweli kwamba ajenda hiyo imejadiliwa na rasimu ya Muafaka imeandaliwa na kama CUF walikuwa na haki ya kuyatangaza haya kwa wanachama wao.

Tukieleweshana haya, tuchunguze mantiki ya hoja mpya ya CCM kutaka suala la mabadiliko ya mfumo wa utawala lazima lifikishwe kwa watu ili waliamue kupitia kura ya maoni.

Hakuna historia ya kura ya maoni kutumika kwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa baada ya kuwepo mgogoro wa kisiasa. Hatujaona hili Burundi, Sudan, Angola, Afrika Kusini na kwa jirani, Kenya.

Masuala ya utawala huamuliwa na Bunge la Taifa husika wakati kura ya maoni hutumika pale panapohusu mabadiliko ya Katiba ya nchi hasa iwapo kuna upinzani miongoni mwa wana wa taifa husika.

Iwapo CCM imekubali "kimsingi" makubaliano iliyofikia na CUF, kura ya maoni inasaidia vipi kuendeleza utaratibu wa kuyatekeleza? Kenya palikuwa na kambi inayotaka katiba mpya na nyingine inayoikataa kwa kuona haikidhi matarajio ya Wakenya. Hapa Kura ya Maoni ilikuwa muhimu.

CCM imeridhia makubaliano yaliyofikiwa kutokana na mazungumzo yaliyoanzishwa na kiongozi wao mkuu ambaye ndiye Rais wa Watanzania. Sasa hoja ya Kura ya Maoni ambayo haikupata kujadiliwa pamoja na wenzao imetoka wapi?

Yanayofanyika ni mazonge matupu yasiyosaidia isipokuwa kuharibu kazi nzuri iliyokwishafanywa. Na Rais na CCM yake inafaa wakumbuke kuwa vyama hivi vina wafuasi wengi kwa hivyo kazi iliyokuwa inafanywa na wajumbe wake, Kamati ya Makatibu Wakuu, ilikuwa inaaminika kwa wafuasi wao.

Haiwezekani tuone hatua zinazobeza kazi hiyo iliyogharimu mamilioni ya shilingi kama posho za wajumbe na malipo ya gharama za chakula, malazi na makazi ya wajumbe waliokuwa wakijadiliana.

Je ni busara kudharau fedha hizi za Watanzania masikini? Hata kidogo. Hebu kila upande urudi kwenye "utu uzima" na kuacha "siasa-mzaha." Bila ya masharti, kila chama kirudi mezani na kuanza walipofikia.

Kama ajenda ya tano haikujadiliwa, kama wanavyodai CCM, ijadiliwe lakini nao lazima waache kushikilia hoja mpya ya Kura ya Maoni. Hatuna njia ya mkato ila kwenda mbele.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: