Sifuri hizi wenyewe ni JK, Lowassa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Kiwete na Lowassa

VIONGOZI wakuu wa nchi wamefikia mahali sasa hawaambiliki. Ushauri wa kitaalam waliopewa juu ya uboreshaji elimu waliupuuza; wakakumbatia siasa ili wajisifu.

Mzaha walioufanya katika elimu tangu mwaka 2001 wakati unaanzishwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na baadaye Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) matokeo yake ni asilimia 88 ya wanafunzi kufeli.

Rais Benjamin Mkapa na Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai ndio walioanza kuvuruga mfumo wa elimu nchini.

Walifuta michezo na baadhi ya masomo muhimu, likiwemo la Kilimo. Wakatengeneza mitaala mipya iliyoanza kutumika mwaka 2005. Wabunge walishangilia mipango ile kwa kuamini ililenga kuimarisha elimu.

Jakaya Kikwete alipoingia madarakani Desemba 2005, akishirikiana na swahiba wake, Waziri mkuu Edward Lowassa, wakaanzisha sarakasi zao.

Wakabadili Wizara ya Elimu na Utamaduni ikawa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na wakamkabidhi Mwalimu Margaret Simwanza Sitta.

Kikwete (JK) na Lowassa wakaasisi rasmi Mradi wa Kudumaza Elimu kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.

Alipokamilisha uteuzi wa Baraza la Mawaziri Januari 4, 2006, JK alipita katika kila wizara kueleza anataka wafanye nini katika awamu yake ya kwanza ya uongozi wake.

Katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliagiza kusitishwa mipango ya kubadili vyuo vya elimu kuwa vyuo vikuu. Agizo hilo lilinusuru vyuo vya elimu vya Marangu na Korogwe baada ya Mkwawa (MUCE) na Dar es Salaam (DUCE) kufanywa vyuo vikuu.

Halafu alipendekeza mitaala ya zamani na michezo irejeshwe badala ya ile ya Mkapa na Mungai. Waziri Sitta alilijulisha Bunge kuwa serikali imefuta mitaala ya Mungai na inarejesha ya zamani pamoja na michezo. Wabunge wakashangilia. Waliamini ni mipango ya kuimarisha elimu.

Baada ya uamuzi huo, nilikwenda Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupata maelezo ya kina ni kwa nini wanakanganya wanafunzi wa Tanzania?

Hoja yangu ilikuwa hivi: Mwaka 2005 serikali imeanza mitaala mipya, mwaka 2006 inairejesha mitaala ile ya zamani. Hii maana yake nini hasa?

TET walinijibu kwa maandishi eti wamefanya utafiti na kugundua kuwa Watanzania wanataka mitaala ya zamani.

Nilipowauliza, mbona Watanzania walipinga mitaala mipya lakini serikali ikaruhusu ianze kutumika. Majibu yao yakawa, “kimsingi mitaala mipya haijasitishwa ila inaboreshwa.”

Januari hiyo hiyo, Lowassa aliyeonekana kukamia sana nafasi hiyo, aliwaita, kama wanafunzi; wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya na maofisa elimu kutaka waeleze mipango ya haraka ya ujenzi wa shule za kata.

Aliwapa muda wa miezi mitatu tu wawe wamepata fedha, wawaandae wananchi na kuanza kujenga shule za kata nchi nzima. Baada ya miezi mitatu, waziri mkuu Lowassa alianza kukagua utekelezaji wa agizo lake.

Shule za sekondari zikachipua kama uyoga huku majengo yakiwa na nyufa, sakafu za vumbi na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikikosekana.

Shule hazikuwa na vitabu, maabara, maktaba, ofisi za walimu, viti, meza wala vyoo. Mbaya zaidi, hakukuwa na walimu. Nakusudia walimu wenye ujuzi na uwezo stahiki.

Baada ya kuona wanasumbuliwa na kelele za ukosefu wa walimu, JK na Lowassa wakabuni majaribio mengine.

Wakaagiza shule zitafute ‘bora walimu’ vijana wa kidato cha nne na sita wanaosubiri miujiza ya maisha ili wawe wanafundisha ikiwa ni kinyume na wito wa Siku ya Walimu Duniani iliyosherehekewa Oktoba 11, 2006 (badala ya Oktoba 5) mjini Mtwara mgeni rasmi akiwa JK.

Wito ulisema, ‘Kila mwanafunzi anahitaji mwalimu bora.’ Haukuwa na maana yoyote maana serikali iliteua walimu wa shule za msingi kuwa walimu wa sekondari.

Kwa kuwa lengo lilikuwa kuonyesha mafanikio ya kisiasa kwamba katika kipindi kifupi uongozi wa JK na Lowassa umefanikiwa kuingiza sekondari watoto wengi, hata wale wasiojua kusoma na kuandika, Lowassa akafuta kozi ya ualimu ya miaka miwili. Sasa ikawa ni kozi ya mwaka mmoja.

Walipoona bado wamezidiwa na kelele za uhaba wa walimu, wakatengeneza walimu wa Vodafasta. Hawa ni vijana waliookotwa mitaani (baadhi yao walitumia vyeti vya ndugu zao) wakapewa mafunzo ya wiki nne ya ualimu kisha wakapewa leseni na kuanza kazi ya ualimu. Hapana shaka baadhi yao walikuwa wamefeli.

Wasomi bobezi walipinga mipango hiyo kwa kujua wazi ilikuwa ni maandalizi madhubuti ya kaburi la elimu katika kipindi ambacho nchi za Afrika Mashariki na Kati zimeridhia itifaki ya soko la pamoja.

Matokeo

Matokeo ya kufungua shule hizo kisiasa na kupuuza ubora wa taaluma yalianza kuonekana mwaka 2007. Wanafunzi wengi waliofanya mtihani wa kidato cha pili walifeli, hivyo hawakuingia kidato cha tatu mwaka 2008.

Hii ina maana, matokeo ya mtihani ule wa kidato cha pili yalikuwa pigo kwa JK na Lowassa. JK akafikiria namna ya kujenga taswira yake iliyoporomoka siyo tu kwa matokeo hayo, bali pia ushiriki wa swahiba wake Lowassa katika sakata la Richmond.

Akamtimua kazi Februari 2008, akaunda upya Baraza la Mawaziri na kumleta kitini Mizengo Pinda. Huyu alikuwa waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu (Lowassa) akishughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Alielekeza zaidi akili yake kwenye kilimo kuliko elimu.

Kwa hiyo, mradi wa kudumaza elimu ukabaki kwa JK pekee.

Ni kweli, akatoa pendekezo lililoruhusu ‘vilaza’,  -vijana wasio na uwezo – kusoma bila kufeli.

Katika mkutano na maofisa elimu, walimu wakuu wa shule na vyuo, wataalamu wa elimu na wasomi uliofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, JK alipendekeza mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne isiwe kikwazo katika “juhudi za kuimarisha elimu.”

Pendekezo hilo likawa amri kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe. Akatangaza bungeni mitihani hiyo miwili ‘imefutwa’. Wabunge wakashangilia.

Alisema mitihani itakuwepo lakini haitatumika kuchuja vijana waliofeli ila wataendelea na masomo ya kidato cha tatu na darasa la tano. Halafu wakagatua usimamizi wa elimu ya sekondari kwa Tamisemi.

JK na Prof. Maghembe wakaamua kurejesha mfumo wa kitabu kimoja shuleni badala ya vitabu vingi. Hilo likazua mkanganyiko mwingine.

Madhara

Vijana walioingia kidato cha kwanza mwaka 2006 walipaswa kumaliza kidato cha nne mwaka 2009. Lakini waliofeli mtihani wa kidato cha pili mwaka 2007, walirudia darasa hilo mwaka 2008 wakawa pamoja na walioanza kidato cha kwanza 2007.

Sawa? Kwa kuwa, baada ya kufutwa mtihani wa kidato cha pili mwaka 2008 vilaza wote waliingia kidato cha tatu mwaka 2009 hadi kidato cha nne mwaka 2010, ni dhahiri JK na Lowassa wamefanikiwa katika Mradi wa Kudumaza Elimu waliouanzisha mwaka 2006.

<p> 0753 626 751</p>
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: