Sigonda: Kamanda wa vita dhidi ya dawa bandia


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

KUNA zoezi linaitwa 'Operesheni Mamba' ambalo linaendeshwa hapa nchini. Kamanda wa operesheni ni Margareth Ndomondo-Sigonda.

Hii ni operesheni ya kukamata wafanyabiashara wanaoingiza na kuuza dawa bandia nchini.

Wakishakamatwa, wahusika wanafikishwa mahakamani.

Operesheni inahusisha jeshi la polisi nchini kwa kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Rais, Bohari ya Dawa (MSD) na kitengo cha huduma za dawa cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mkurugenzi wa TFDA, Margareth Ndomondo-Sigonda anasema awamu ya kwanza ya operesheni hiyo ilifanyika Septemba 2008. Operesheni Na. 2 imefanywa Agosti mwaka huu katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga na Mwanza.

“Operesheni Mamba Na. 2 ilishirikisha watendaji 70 kutoka taasisi mbalimbali katika nchi za Kenya na Uganda katika tarehe hizo hizo, chini ya utaratibu wa Interpol,” anasema.

Utaratibu wa kufanya operesheni hiyo kwa pamoja na kwa muda mmoja ulizingatia makubaliano ya pamoja, yaliyofikiwa kwenye mkutano wa maandalizi uliofanyika 27 Juni, 2009 Nairobi, Kenya.

“Dawa zilizolengwa zilikuwa ni za kutibu ugonjwa wa malaria, viuavijasumu (antibiotics), dawa za kuongeza nguvu za kiume jamii ya Viagra na dawa za kupunguza maumivu jamii ya paracetamol,” anasema Ndomondo-Sigonda.

Mkurugenzi huyo wa TFDA anasema dawa hizo zilichaguliwa kutokana na kutumika zaidi nchini.

Katika mikoa iliyotajwa, operesheni ilifanyika wilaya zote za Dar es Salaam; Arusha mjini, Namanga; Mbeya mjini, Tunduma; Shinyanga mjini, Kahama; Mwanza mjini na Geita.

“Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na yale ya biashara ya dawa ambayo ni maduka ya dawa baridi, maghala ya kutunzia dawa, hospitali binafsi, maeneo ya mipakani, mabasi ya abiria, treni za abiria na popote palipotiliwa shaka kuwapo kwa dawa bandia,” anasema.

Ili kuendelea kutimiza jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa vya tiba, TFDA imeazimia kuendelea kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti nchini, ikiwa ni pamoja na mradi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupambana na dawa bandia, kwa kushirikiana na Interpol.

“Tunapanua uwanja wa ushirikiano kwa kutambua kuwa biashara ya dawa bandia ni haramu, inayovuka mipaka, inayohitaji juhudi zetu sote na pia ushirikiano na nchi tunazopakana nazo kama ilivyofanyika katika Operesheni Mamba Na. 2” anasema Ndomondo-Sigonda.

Katika operesheni kulikuwa na ukaguzi wa famasi 53, maghala ya dawa matatu, maduka ya dawa baridi 39, hosptali sita na maeneo mengine 41.

Kutokana na ukaguzi huo, aina 319 za dawa, zenye thamani ya Sh. 9,538,970 zilikamatwa. Dawa hizo zilijumuisha dawa bandia, dawa zilizomaliza muda wa matumizi, dawa za serikali, dawa zisizosajiliwa na dawa moto kutoka maduka ya dawa baridi.

Katika operesheni hiyo, aina 238 za vipodozi vilivyopigwa marufuku, vyenye thamani ya Sh. 12,555,700 vilikamatwa, vikiwamo aina nne ya dawa zinazosadikiwa kubadilisha au kuongeza maumbile ya binadamu.

Matokeo ya operesheni hiyo ni kuanza kuchukuliwa kwa hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa majalada 38 ya watuhumiwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi. Kesi sita ni za Mkoa wa Dar es Salaam, nne Mbeya, tano Shinyanga, 18 Arusha na tano mkoani Mwanza.

Margareth Ndomondo-Sigonda anazungumzia pia hatua ya TFDA kupata cheti cha kusajiliwa kwa mfumo wake wa udhibiti wa dawa na vipodozi katika kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2008 cha Mfumo wa Kuhakiki Ubora wa Huduma (Quality Management System).

“Ni makampuni na mashirika machache sana hapa nchini ambayo mpaka sasa yamefanikiwa kufikia kiwango hiki cha kimataifa katika utoaji wa huduma.

“Nia ya utekelezaji wa Mfumo wa Kuhakiki Ubora wa Huduma ni kutoa huduma ambazo zinakidhi au kupitiliza mahitaji ya wateja kwa kuzingatia michakato, taratibu, kanuni, sheria na miongozo,” anasema.

Mwaka 2006 menejimenti ya TFDA iliamua kutekeleza kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2000, ambacho baada ya mapitio yake sasa kinaitwa ISO 9001:2008 ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa wateja zinaendelea kuboreshwa.

Mchakato wa kufuata kiwango cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma ulianza mara baada ya kufanyika tathmini juu ya utendaji kazi wa TFDA mwaka 2004 na 2005.

Tathmini hiyo ilibaini ukosefu wa michakato na taratibu sanifu za utendaji kazi zilizoainishwa na kurasimishwa na kutokuwapo utaratibu rasmi wa kushughulikia malalamiko ya wateja.

Aidha, tathmini ilibaini kutokuwepo mfumo rasmi wa mawasiliano ndani na nje ya TFDA na ukosefu wa kumbukumbu na nyaraka ipasavyo, hivyo kufanya hifadhi, ufuatiliaji na utafutaji taarifa kuwa mgumu.

0
No votes yet