Siku 100 za serikali kujiumauma


Sophia Yamola's picture

Na Sophia Yamola - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version

KAMA Rais Jakaya Kikwete angejua anakamilisha siku 100 za kipindi cha pili cha utawala wake wa awamu ya nne kwa staili hii, angeomba kukwepa kikombe hiki.

Haikuwa hivyo. Jumatano ya Februari 16, 2011, siku ambayo vyombo vingi vya habari na hasa magazeti, vilikuwa na habari na makala kuhusu utawala wake, usiku ilikuwa balaa.

Magazeti yalizungumzia matatizo ya kiuchumi nchini, kukua kwa pengo la kiuchumi kati ya matajiri na maskini, kukithiri kwa ufisadi na mafisadi na namna serikali ilivyoshindwa kuwapa matumaini wananchi.

Vilevile magazeti yalizungumzia jinamizi la mgawo wa umeme linalotokana na maji kupungua katika bwawa la Mtera, na mapambano kati ya wawekezaji na wananchi juu ya umiliki wa ardhi.

Usiku wa Jumatano ikawa balaa kwa utawala wa Rais Kikwete. Maghala ya silaha zilizohifadhiwa kwa ajili ya kulinda wananchi yalilipuka yakaua watu zaidi ya 40 na kujeruhi zaidi ya 300 katika kambi ya Gongolamboto, Dar es Salaam.

Wakazi wa maeneo ya jirani na kikosi hicho na 511 KJ walipigwa na mabomu yaliyoruka kutoka katika kambi hiyo.

Japokuwa mabomu hayo yaliruka hadi umbali wa zaidi ya kilomita 20, walioathirika zaidi ni wakazi wa maeneo ya Gongolamboto, Pugu Kajiungeni, Pugu Stesheni, Kinyerezi, Segerea, Mwishowalami, Majohe, Kitunda, Mwanagati, Mombasa.

Nyumba kadhaa zilivunjwa, mali ziliharibiwa na mamia kubaki bila makazi. Hilo ndilo lilikuwa hitimisho la siku 100 za Rais Kikwete ambaye juzi alikwenda Mauritania kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa wa Ivory Coast.

Kambi ya Gongolamboto ililipuka mwaka 2005, halafu mwaka 2009 kambi ya Mbagala na mwaka 2011 kambi ya Gongolamboto tena

Je, ni bahati mbaya, uzembe, hujuma au ujinga? Hakuna anayejua, lakini Rais Kikwete amewataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Tume ya Uchunguzi inafanya kazi kujua sababu za milipuko iliyosababisha maghala yote 23 kuteketea.

Je, itatoa ripoti? Hakuna anayejua maana mpaka sasa hakuna ripoti iliyotolewa kufuatia milipuko ya mwaka 2005 na 2009.

Ahadi za 2010

Vyombo vya habari vimepima utendaji kazi wa Rais Kikwete kuona alivyojipanga kutekeleza rundo la ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Katika kampeni zake za kuomba achaguliwe tena kuongoza kwa kipindi cha pili katika utawala wake wa awamu ya nne, Rais Kikwete alitoa ahadi nyingi kwa wananchi zinazokadiriwa kugharimu kiasi cha Sh. 90 trilioni.

Baadhi ya ahadi alizotoa Rais Kikwete, mwaka jana ni pamoja na kujenga barabara za juu katika jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari, kujenga majengo ya biashara maarufu kama Machinga Complex mawili katika kila wilaya za mkoa wa Dar es Salaam.

Ahadi nyingine alizotoa ni kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa, kujenga hospitali katika kila jimbo, kulipa madeni ya Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) na kufufua chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Mbinga (MBICU) –Ruvuma

Ahadi nyingine ni kununua meli kubwa katika Ziwa Victoria kuliko MV Bukoba iliyozama Mei 21, 1996, kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa, na kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa, ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Rais Kikwete pia aliahidi kuboresha barabara za Igunga –Tabora, Njombe- Makete, Musoma – Mto wa Mbu. Vilevile aliahidi kukarabati barabara ya Moshi-Arusha, na Singida-Dodoma.

Rais Kikwete alifunga mwaka kwa kukimbiwa na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipokuwa anazindua Bunge la 10 mjini Dodoma.

Januari 2011

Wakati Rais Kikwete hajaanza kutekeleza ahadi zake, amani, utulivu na mshikamano wa wananchi umetiwa msukosuko. Analaumiwa kila kona na wengi sasa ni kutoka kwenye chama chake—Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwanza ni hatua yake ya kuwaomba wananchi wakubali ongezeko la gharama za umeme ilimsababishia shutuma nyingi wakidai kuwa serikali yake ililenga kukusanya fedha za kugharimia malipo ya Sh. 94bilioni ambazo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linadaiwa kama fidia na Dowans.

TANESCO ilipandisha gharama za umeme kwa asilimia 18, hali iliyolalamikiwa na wananchi wengi kwamba itachangia kudhoofisha uchumi.

Halafu serikali yake ikakumbwa na shutuma kwamba, pamoja na gharama za umeme kupanda kuanzia 1 Januari 2011, TANESCO ikatangaza mgawo nchi nzima na huenda mitambo ya Mtera ikazimwa Aprili kutokana na mabwawa kupungua maji.

Pili ni msimamo wa chama chake CCM wa kupindisha taratibu za uchaguzi wa mameya nchini ambao umekuwa kiini cha mvutano, maandamano na mauaji.

CCM imekuwa kiini cha maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyofanyika Januari 5, 2011 kupinga utaratibu mbaya wa kumpata meya wa halmashauri ya Arusha.

Katika maandamano hayo, polisi wakishiriki kulinda ukiukwaji wa taratibu, iliua watu watatu—Watanzania wawili na Mkenya mmoja na makumi kujeruhiwa.

Tatu ni katika siku 100, serikali yake imeachia gharama za vitu zikipanda kama vile petroli, dizeli, mafuta ya taa na vyakula. Tayari serikali imeridhia kupanda kwa nauli ya mabasi kuanzia mwezi ujao.

Nne ni serikali yake kushindwa kutekeleza madai ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini. Wanafunzi hao waliomba kuongezewa fedha za kujikimu kutoka Sh. 5000 hadi Sh. 10000 na iliposhindwa kuwasikiliza walifanya maandamano yalizimwa kwa nguvu za polisi.

Mgomo mwingine uliotikisa serikali ya Rais Kikwete ni wa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambao wanataka kujua hatima ya mkataba wa uendeshaji wa reli ulioingiwa kati ya serikali na kampuni ya Rites kutoka India. Serikali imeshindwa kutoa majibu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: