Sikufuata mkumbo kuhama CUF - Miraji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

“UAMUZI wangu wa kujiondoa CUF ni muafaka. Wala mimi sikufuata mkumbo,” anasema Said Miraji Abdalla, mwenyekiti mwanzilishi wa chama kipya cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Miraji, mwanasiasa aliyefikia wadhifa wa kaimu naibu katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), anasema ameamua kujenga chama makini baada ya kuona CUF, chama alichowekeza hadi “roho yake,” kimepoteza mwelekeo.

Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Miraji anasema wanaodhani kuwa amekurupuka kuanzisha chama kipya hawaujui ukweli.

“Sikukurupuka hata chembe. Wala sikufuata mkumbo kama viongozi wa CUF wanavyosema; eti wanaotoka wanamfuata Hamad Rashid,” anasema.

Hamad Rashid Mohamed, mbunge wa Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Pemba, ni mmoja wa viongozi waliovuliwa uanachama na chama hicho mapema mwezi uliopita, kwa tuhuma za kuasi chama.

Kwa sasa, wanasubiri hatima ya kesi yao Mahakama Kuu Dar es Salaam, ya kupinga uamuzi huo wa Baraza Kuu la Uongozi (BKU).

Miraji analaumu viongozi wa juu kuwa wamesahau misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho; badala yake wanasakama wenzao wanaohoji mambo yanayoendeshwa ovyo.

“Sasa hawajali wanachama wenzao na wanaendesha chama bila kuzingatia katiba. Kanuni za utumishi katika chama hazipo. Tangu nilipoziacha na kuagiza zichapishwe hakuna kilichofanywa,” anasema.

“Kila ninavyofikiria yanayotokea, najisikia aibu. Nilipojiuzulu uongozi nilishauri mambo mengi… kujenga mfumo mzuri wa kuandaa viongozi vijana ili waje kushika nafasi wazee wanapoondoka. Walipuuza na sasa chama kinavurugwa sote tunaona,” anasikitika.

Miraji anasema aliona matatizo ya msingi hata kabla ya viongozi waandamizi Juma Othman, Fatma Maghimbi na mwaka jana kiongozi mwingine muhimu, mheshimiwa Lwakatare kuhama.

Hata hivyo, hasikitiki kwa wote hao kutoka, bali ameumia kuona viongozi wamempoteza Profesa Abdallah Jumbe Safari. “Huyu ni hazina kubwa,” anasema.

“Alipotoka Profesa Safari moyo wangu uliumia sana. Makosa zaidi yalitendwa wakati wa kupanga safu ya uongozi baada ya uchaguzi wa chama.

“Niliwahi kumshauri Profesa Lipumba afanye awezalo asimpoteze. Niliamini alinielewa, labda hakuzingatia. Kweli, amempoteza profesa mwenzake mahiri,” anasema.

Miraji amepanga kumuomba Profesa Safari aungane nao japo kwa muda kuijenga ADC. “Tukishapata usajili tutamuomba hata kwa mkopo atusaidie. Ni mzuri kwa mipango. Namjua vizuri, ni bahati mbaya tu hakutumika ipasavyo CUF, sisi tutamtumia,” anasema.

Profesa Safari, ambaye alishindwa na Profesa Lipumba alipogombea uenyekiti 2009, alihama rasmi 20 Januari mwaka jana na wiki chache baadaye, akahamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Miraji anasema Profesa Lipumba hana timu nzuri ya kumsaidia kazi ngumu ya kujenga upya chama, jambo analosema “linatishia mustakabali wa chama.”

“Baada ya hao, wanampoteza Hamad Rashid, kiongozi mwingine muhimu. Tatizo (viongozi wa CUF) wanamuangalia kama mbunge tu peke yake. Hawajui mchango wake kwa taifa,” anasema.

Miraji anasema anachokiona ndani ya mgogoro uliopo CUF, ni suala la uhusiano wa Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad na Hamad Rashid.

Uhusiano wao, anasema, unafanana na ule wa aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel arap Moi na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Robert Ouko; kwamba Moi alihofia kupikuliwa na Ouko ambaye baadaye alikutwa ameuawa kikatili.

“Tunawaona viongozi wakijiona nyota zao zinafifia wanahangaika na kuanza kusakama wengine, hasa wanaoona wana mvuto. Mheshimiwa Hamad Rashid hata kama wanaona ana ushindani jimboni, ana nguvu zake na ana mchango mkubwa kwa chama hadi anga za kimataifa,” anasema.

Anasema amejiridhisha pasina shaka hakuna tena viongozi watulivu CUF. “Ndani ya uongozi wa CUF huoni kiongozi mwenye hamasa ya kujenga chama.

“Mtazame Profesa Lipumba, ni mguu ndani mguu nje. Muda mwingi hayupo nchini. Na Maalim unaona hivihivi muda wake mwingi unatumika kwa shughuli zake za Makamu wa Kwanza wa Rais.

“Katika hali kama hii, unabaki kuwategemea manaibu katibu wakuu wafanye kazi zao. Lakini wa Bara amenikatisha tamaa. Hana historia ya kazi za siasa. Kakaa katika chama kwa muda gani hata kupewa nafasi hii… kajiunga lini na CUF.

“Uhai wake ndani ya CUF haujafika hata wa mtoto kuanza shule, huyu haijui CUF… hajui dhamira ya CUF, hawajui watendaji wa CUF. Kweli hajui ndio maana anabaki na majigambo ya Chuo Kikuu.

“Huwezi kuendesha chama chenye historia kubwa kama CUF kwa kutumia mbinu ulizotumia kuongoza wanafunzi Chuo Kikuu. Haya ni mambo mawili tofauti, kila moja lina utaratibu wake na hapa tunazungumzia chama mbadala cha kuchukua madaraka ya nchi,” anasema.

Naibu Katibu Mkuu Bara ni Julius Mtatiro, aliyejiunga mwaka 2009. Oktoba 2010, aliteuliwa mkurugenzi wa haki za binadamu. Mwaka jana mwishoni aliteuliwa unaibu katibu mkuu.

Akimgeukia Ismail Jussa Ladhu, naibu katibu mkuu Zanzibar, anasema anamthamini kama kijana imara, lakini “ana upungufu mkubwa katika mlahaka mzuri na watu ndani ya chama.”

Anasema, “Jussa anakosa PR.” Herufi hizi mbili ni sawa na Public Relations, yenye maana “uhusiano mzuri na umma.”

Anakumbusha upungufu huo ulivyolazimu uongozi ukabidhi dhamana ya kusimamia suala la haki za binadamu kwa kiongozi mwingine pale Jussa alipoteuliwa mkurugenzi wa mambo ya nje na haki za binadamu. Eneo hilo alisimamia Khamis Hassan.

Miraji alijivua uanachama wa CUF 27 Februari mwaka huu alipotangaza kuanzisha chama kipya cha ADC na kupeleka maombi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ya kutaka usajili wa muda, yeye akiwa mwanzilishi na mwenyekiti wa muda.

Lakini, safari yake ya kuhama CUF ilianza Oktoba 2008 alipoeleza viongozi wake dhamira ya kuachia nafasi zote za uongozi.

“Mwanzoni walinikatalia,” anasema. Aliambiwa kama alijiandaa kuachia ngazi, chama nacho kinahaki ya kujiandaa kumkosa kiuongozi. Baadaye mwezi huohuo, alijibiwa kwa barua kukubaliwa kuondoka.

Kwanini Miraji alijivua uongozi CUF, chama alichokitolea jasho jingi na kama asemavyo leo, “alichokiwekea rehani roho yake?”

“Jambo kubwa lililonitoa ni kuona yale mambo ya msingi tuliyokuwa tukiyapigania, sasa hayazingatiwi tena... wakati tunaunda chama, watu walitumainia kiwe mkombozi wa kweli.

“Tulilenga kupigania kuondoa dhulma na ukandamizaji Watanzania. Tukasema tuitoe nchi katika uchumi tegemezi. CUF inapofukuza viongozi wanaohoji mambo yanayokwenda ovyo ni dhahiri imesahau malengo yake,” anasema.

Hata Zanzibar ambako kumepatikana mafanikio ya kuundwa kwa serikali ya ushirikiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema mambo hayaendi vizuri kama inavyoelezwa.

“Maisha yanazidi kuwa magumu kwa wananchi. Mambo yako vilevile kama tulipokuwa nje ya serikali,” analalamika.

Miraji alitoka wapi? Alikuwa nani? Analenga nini kuanzisha chama kipya?

Itaendelea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: