Simba mwendo mdundo kama 1993?


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

BAADA ya wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kuondolewa, Simba ya Dar es Salaam ndiyo klabu pekee iliyosalia na inayobeba matumaini.

Yanga, iliyokuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika imetupwa nje baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-1 na Zamalek ya Misri. Mwishoni wa wiki iliyopita Yanga ilichapwa bao 1-0 jijini Cairo wakati katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa ililazimishwa sare ya 1-1.

Wawakilishi wengine katika michuano hiyo, Mafunzo ya Zanzibar wanasubiri kurudiana na Muçulmano Maputo ya Msumbiji utakaopigwa 10 Machi mwaka huu huko Msumbiji. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Zanzibar, Mafunzo ililala kwa mabao 2-0.

Nayo Jamhuri ya Zanzibar imeaga michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa jumla ya mabao 7-1 na Hwange ya Zimbabwe. Katika mechi ya kwanza Zanzibar, Jamhuri ilipigwa 3-0 na marudiano mwishoni mwa wiki iliyopita ilipigwa 4-1.

Matokeo hayo yanaifanya Simba ibebe matumaini ya wadau wa soka nchini baada ya kuifunga Kiyovu FC ya Rwanda jumla ya mabao 3-2, kwani wiki iliyopita ilishinda 2-1 wakati awali ilitoka sare 1-1 ugenini.

Je, Simba itarudia rekodi ya takriban miaka 20 iliyopita? Mwaka 1993 Simba ilifika fainali ya kombe hilo lakini ilichapwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Siri kubwa ya mafanikio ya Simba kwa mwaka 1993 ilikuwa kushinda mechi zote za nyumbani na kulazimisha sare mechi za ugenini na ilipofungwa basi ilikuwa kwa idadi ndogo ya mabao.

Mwaka huo Simba ilianza safari kwa kuitoa Ferroviário ya Msumbiji ; sare ya  0-0 Dar es Salaam na  1-1 Maputo; kisha ikaitoa Manzini Wanderers ya Swaziland 2-0 ; robo fainali ikaiondoa USM El Harrach ya Algeria 3-2 na nusu fainali ikaigalagaza AS Aviação ya Ang   3-1 kabla ya kukwaana na Stella.

Simba ililazimisha sare ya  0-0 Abidjan lakini ikakubali kichapo cha  2-0 Dar es Salaam na kukosa kombe mbele ya mashabiki wake. Matokeo haya ya kihistoria yanaihamasisha Simba kufanya vizuri mwaka huu.

Nyuma ya matokeo haya kuna mambo ya kujifunza kwa timu zetu hasa kwa kutumia uzoefu wa timu walizopambana nazo. Kwa mfano, Yanga ilicheza na Zamalek iliyoonekana kuwa katika matatizo lukuki, lakini kwa vile haikujiandaa kushindana ilitoa nafasi kwa timu hiyo ya Misri kufanya itakacho.

Inawezekana historia ya mafanikio ya Zamalek iliizubaisha Yanga na kusahau kilichofanya wakutane uwanjani. Sishawishiki kuamini kwamba, ubutu wa washambuliaji kama Kenneth Asamoah na Davies Mwape, ndiyo uliokosesha ushindi.

Bado katika soka letu kuna tatizo kubwa la kutotambua wajibu. Timu hazina mfumo wa kukidhi mahitaji yake kuanzia usajili hadi maandalizi ya michezo ya kimataifa.

Baada ya kutoka sare ya kizembe ya bao 1-1 nyumbani na Zamalek iliyokuwa hohe hahe, Yanga ilichukua mazingira ya mchezo wa kwanza ili icheze mechi ya marudiano. Hilo ndilo kosa kubwa. Hakukuwa na kubwa la tofauti katika mechi ya marudiano na matokeo yake ikaambulia kipigo cha bao 1-0.

Hata Simba iliyoifunga Kiyovu nyumbani 2-1, kuna kitu inaweza kukosa na hata kufungwa endapo kikosi kitaingia uwanjani bila ya wachezaji fulani. Hebu jaribu kuwatoa kikosini Emmanuel Okwi na Felix Sunzu halafu wape nafasi Gervais Kago na Uhuru Selemani uone kitakachotokea.

Kazi kubwa iliyo mbele ya Simba ni kuhakikisha inaachana na mfumo tegemezi kwa idadi ndogo ya wachezaji. Sitaki kuamini kwamba kuaminiwa kwake ndani ya kikosi kunampa Okwi kiburi cha kufanya madudu ya nje ya uwanja mara kwa mara.

Mabao aliyofunga Sunzu mbele ya Kiyovu ndiyo yale ambayo Asamoah na Mwape walikosa dhidi ya Zamalek nyumbani.

Miaka kadhaa sasa timu zetu zitaendelea kuishia hatu ya pili au ya awali katika michuano hii ya kimataifa, sababu hazina mfumo mzuri wa kuwa na vikosi bora kutokana na matakwa ya wachache wasiojua lolote katika soka.

Kila baada ya miezi sita vikosi vya Simba na Yanga vinabadilika na kutoa kazi kubwa kwa kocha. Mbaya zaidi hata makocha nao wanaweza kubadilika ndani ya kipindi hicho hicho cha nusu mwaka.

Mipango mbalimbali ya maendeleo ya vijana haitekelezwi katika timu na zenyewe zinaishia katika nadharia pekee si vitendo. Hili ni janga la kitaifa, hakuna soka la vizazi katika mfumo wetu wa soka. Na kinachofanyika sasa katika kusaka vipaji ni kichekesho.

Kwa muda huu ambao hata hamasa ya watu kufika uwanjani imebakia kwa ngazi ya klabu pekee, tunapaswa kukubali uwezo wa timu zetu kisha kupanga mikakati thabiti itakayowezesha klabu kuwa na mfumo mzuri kuanzia kiutendaji hadi kwa wachezaji.

Idara ya ufundi inapaswa kuwa na watafuta vipaji wenye taaluma hiyo, tena kwa kuzingatia mahitaji ya klabu na uwezo wa kufanya hivyo kwa matumizi ya baada ya miaka michache. Hapo tutaondokana na kasumba ya kusajili wachezaji wa kigeni wasio na msaada kwa timu.

Watu wa masoko na udhamini nao watapaswa kufanya kazi zao kwa mafanikio kwa kupata wadhamini watakaokuwa tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha michezo na hosteli za uhakika, pia mishahara na posho mbalimbali za wachezaji.

Hakuna miujiza katika soka zaidi ya kuwekeza katika soka la vijana, tazama nchi na timu nyingi zilizopata mafaniko ambazo ziliwekeza katika soka la vijana. Tatizo Tanzania timu nyingi hazitaki kupanda, zenyewe zinataka kuvuna pekee.

Tunapaswa kukubali uwezo wa sasa wa Simba lakini tupange mikakati ya kuwa na vikosi imara vitakavyofanya vizuri katika michuano ijayo mwakani.  Siiombei mabaya Simba, lakini mwisho wa safari yake ni kama nauona.

0713801699
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: