Simba, Yanga zimeumbuka


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

MAGAZETINI na kwenye vyombo vingine vya habari, klabu za soka za Simba na Yanga ni bora na moto wa kuotea mbali, lakini dimbani hazina kitu.

Kila klabu ilisifiwa kwa usajili makini kwamba zimepata wachezaji wa viwango katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Matokeo ya mechi za kujipima nguvu dhidi ya klabu za hapa nchini yakazipumbaza, lakini matokeo ya mechi za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati yameziumbua klabu hizo kwamba ni midabwada.

Yanga ilifungwa 2-0 na Atraco ya Burundi na Simba ilitandikwa idadi kama hiyo ya mabao na URA ya Uganda. Timu nyingine ya bara, Azam yenyewe ilitoka sare ya bao 1-1 na Mafunzo ya Zanzibar wikiendi iliyopita.

Tatizo ni nini, usajili au maandalizi mabovu? Mara zote zinapofanya vizuri kama timu, tumekuwa tukisifu uhodari wa vikosi vya timu hizo na hata kwa wachezaji mmoja mmoja kama Haruna Niyonzima wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba.

Kwa mfano leo hii tutakuwa wakosefu wa fadhila kama hatutomsifia kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ wa Yanga na Amri Kiemba wa Simba. Chuji ‘alipotea’ lakini sasa anaonekana kurudi katika kiwango chake, Kiemba naye nusura atemwe na Simba, sasa ni moto wa kuotea mbali, hashikiki dimbani.

Mara tu usajili wa msimu huu ulipoanza, Chuji akaonekana kuwa katika kiwango cha hali ya juu sawa na Kiemba ambaye ilibaki kidogo aachwe na Simba. Hao hakuna sababu ya kuwanyima sifa zao.

Sifa hizo ni dhahiri zinaenda sehemu stahili, lakini anayesifiwa anazipokeaje? Hilo ndilo tatizo la wachezaji wetu na timu kwa ujumla. Timu zinacheza mpira vichwani kabla hata ya kuingia uwanjani huku zikiamini sifa ndizo zinazocheza.

Wiki iliyopita niliandika kuhusu kutoona umuhimu wa Kombe la Kagame kuchezwa Tanzania kwa miaka miwili mfululizo, kwani hakuna mantiki yoyote ya kufanya hivyo zaidi ya kudidimiza soka letu. Leo hii tunaona kwani timu zetu hazijiandai ipasavyo na hali hiyo ya kutetea bendera ya Tanzania.

Simba na Yanga ambazo zimewaacha au kukosa zaidi ya wachezaji watano muhimu katika vikosi vya kwanza, zimeingia katika michuano hiyo bila ya maandalizi ya maana huku zikionekana kujidanganya kwa sifa za magazeti.

Kote duniani anayefanya vizuri husifiwa, kinachofuata ni yule anayesifiwa kulinda sifa anayopewa. Simba na Yanga hazina sifa ya kulinda sifa zake, na mwisho mashabiki wao wengi si wanamichezo, hawatazami sababu za kufungwa.

Timu zao zikifungwa anayehusika ni kiongozi, tena aliye nje ya benchi la ufundi. Huu ni upuuzi unaoendekezwa bila sababu ya msingi, kubadilika ni muhimu kwa kila mdau wa soka ili Tanzania isonge mbele.

Kila siku tunajidanganya na Simba na Yanga kuwa zitakuza soka letu, hakuna hizo zipo kuteka akili zetu na kuamini hata zikija Real Madrid na Barcelona zitafungwa tu. Maamuzi mengi ya klabu hizo ni zimamoto, viongozi wengi wapo kwa ajili ya kujifurahisha tu siyo kuleta maendeleo.

Katika Kombe la Kagame, timu nyingi zinaonekana kujipanga zaidi ili kutwaa ubingwa, Simba na Yanga zenyewe zinatumia muda mwingi kuwazungumzia wachezaji inao wasajili. Sasa midomoni mwao wapo beki Kelvin Yondan na Okwi.

Yanga imemsajili Yondan kutoka Simba na wakati huohuo ipo mbioni kumtwaa Okwi, kazi ipo hapo. Viongozi wapo tayari kumwaga hata mabilioni ya shilingi ili tu kubakisha wachezaji hao katika timu wazitakazo. Hao, hawajuhi lolote kuhusu maandalizi ya timu zao katika michuano mbalimbali.

Kombe la Kagame linaumbua usajili wa Simba na Yanga uliokuwa unafanywa kilazima na vibosile ili tu kujihimarishia tawala za uongozi wanazojilimbikizia ndani ya klabu hizo. Dawa yao pekee iliyobaki sasa baada ya mambo kuwashinda ndani ya uwanja ni kucheza soka nje ya uwanja.

Tutarajie waamuzi kuzibeba klabu hizo ili zifike mbali zaidi ili kufurahisha mashabiki na ndiyo maana katika michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), zinaumbuka.

Ni kama zimetuvua nguo, Simba na Yanga hazikupata muda wa maandalizi, na mbaya zaidi usajili wa wachezaji 20 kwa Kombe la Kagame ni tatizo lingine; wote makocha wao hawajakaa kwa muda wa wiki nne na wachezaji wapya.

Na hata kama wangekaa kwa muda mrefu na timu hizo, timu ambayo kocha hakuisajili hawezi kupata kikosi cha kwanza haraka, nje ya hapo atakuwa anabahatisha kupanga kikosi na hata ushindi utakuwa wa bahati.

Azam yenyewe ina mfumo maalum wa usajili hadi kutema wachezaji lakini siyo Simba na Yanga. Hata Mafunzo ya Zanzibar inaweza kuwa bora kuliko timu hizo kongwe, lakini nani atakayeifahamu Mafunzo? Haipewi nafasi ya kujitangaza.

Simba na Yanga zina mashabiki lukuki nchini, na ndiyo hao wanaonunua magazeti yanayosifia timu zao. Ni hao hao wanaolaumu magazeti hayo hayo kwa kuzisifia timu hizo pindi zikifanya vibaya. Shabiki huyo naye anahusika katika kuiharibu klabu hizo, kwani anaamini habari nzuri ni ile inayozihusisha timu hizo.

Hakika Simba na Yanga zimebebwa mno na magazeti na sasa zinayadhalilisha magazeti hayo.

0713 801 699
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: