Simu ya Rais haina tija


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete anasema simu yake ya mkononi iko wazi kwa yeyote anayetaka kuwasiliana naye. Namba ambayo wengi tunaifahamu ni 0754 777775.

Akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini nchini, mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete alisema amekuwa akiwasiliana na wananchi moja kwa moja kwa simu ya mkononi.

Aliwaambia, “…simu yangu ile ipo wazi muda wote. Watu wananitumia sms (ujumbe mfupi wa simu), wananipigia, wengine wananieleza matatizo yao mbalimbali. Nazungumza nao. Nanyi nawaomba msisite kufanya hivyo.”

Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifunga mkutano wa siku mbili wa viongozi hao uliolenga kufahamisha kilichomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi aliyosaini hivi karibuni.

Rais aweza kuwa anajibu simu; na kama alivyosema wakati mwingine hujibu ujumbe aliotumiwa kwa njia ya kupiga badala ya kuandika.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwenye uhakika iwapo Kikwete anaitumia simu hiyo kupata taarifa kwa ajili ya umma au ni taarifa binafsi. Hii ni kwa kuwa simu ya rais inashikwa na rais mwenyewe.

Ndiyo maana taarifa zinasema, kila anayetuma ujumbe kwa rais hujibiwa na rais mwenyewe.

Baadhi ya wale ambao wamewasiliana naye na ambao nimehojiana nao, wanasema muda mzuri wa kutuma ujumbe kwa Kikwete; na ili ujibiwe, ni kuanzia saa saba usiku.”

Lakini je, rais anastahili kusumbuliwa na mambo kama vile mwaliko wa harusi, kipaimara au mzazi kushindwa kumcheza mtoto mkole? Je, haya hayampi kazi ya ziada ambayo inaminya muda wake kwa shughuli za umma?

Chukua mfano wa mawasiliano ambayo Rais Kikwete alifanya mwaka 2007 na mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Chifupa. Kwa maoni ya wengi hayakulenga kusaidia taifa. Yalikuwa yanamuongezea rais mzigo.

Chifupa alilalamika kwa rais, akituhumu mmoja wa mawaziri wake kuingilia ndoa yake. Alidai waziri huyo alikuwa anamsakama kutokana na kile alichoita, “kutaka kiti cha Umoja wa Vijana CCM.”

Kikwete alijibu ujumbe wa Chifupa kwa kumwambia mengi. Lakini kubwa alisema, “Mungu yupo nawe.”

Amina hakutunza siri ya mawasiliano kati yake na rais. Alitumia mawasiliano hayo kushambulia wapinzani wake kisiasa.

Taarifa zinasema Chifupa aliwapa wengi mawasiliano yake na rais. Alirudi hadi kwa mbaya wake na kumtambia kuwa tayari amemshitaki kwa rais. Baadhi ya mawasiliano ya rais na Chifupa yaliwahi kuchapishwa na gazeti hili.

Hivi ni sahihi kwa rais kutolala usiku kucha akipokea sms wakati ana vyombo vya kufanya kazi ya kupokea taarifa?

Vyombo hivi vimeundwa rasmi kwa kazi hiyo na watumishi wake wanalipwa na wananchi kupitia kodi wanayolipa.

Sasa kwa nini rais hataki kutumia vyombo hivyo kumpa taarifa na badala yake anataka kupokea taarifa yeye mwenyewe?

Ukweli ni kwamba, hata kama rais angekuwa na nia njema ya kuongea na kupata kila taarifa moja kwa moja kutoka kwa wananchi, asingekuwa na uwezo wa kuzifanyia kazi.

Kwanza, ni nyingi mno. Pili, zinahitaji uratibu. Tatu, zinahitajika kuchujwa na nne, zinastahili kuandaliwa kwa vipaumbele. Mpangilio huu, hakika siyo kazi ya rais na ndiyo maana kuna vyombo vya kufanya kazi hiyo.

Kama alivyofanya Chifupa na kama wanavyofanya baadhi ya wabunge na mawaziri “waliochati” na rais, nia imekuwa mbwembwe na majigambo kuwa waliongea na rais.

Kuna wanaotajwa kutumia sms zao na rais kujimiminia sifa na kutafutia ubunge. Haya ni mafao binafsi, hata kama rais hakushiriki kuyaandaa.

Naye, waziri mmoja aliwahi kunidokeza mbinu alizotumia kuangamiza wapinzani wake wa kisiasa. Alidai kuwa alipeleka ujumbe kwa Rais Kikwete, naye haraka akachukua hatua.

Waziri huyo alijigamba kuwa ujumbe huo ulikuwa “mtaji” kwake na kwamba atautumia kujiimarisha na kumuangamiza kisiasa mbaya wake.

Alisema kwa jinsi alivyomueleza Kikwete na rais alivyojibu, hategemei tena mbaya wake kurudi katika ufalme wa kisiasa.

Katika mazingira haya, simu ya rais yaweza kutumika kuangamiza wengi. Yaweza kusambaza umbeya; kufitinisha na kuvunja hata ndoa.

Kwa lugha ya vijana, hapa rais amejiachia mno, kama kweli amekuwa mpokea sms usiku kucha. Licha ya ujumbe wake kutumiwa vibaya, lakini naye aweza kupelekewa ujumbe ambao hakutarajia.

Kwa mfano, rais aweza kupelekewa ujumbe wa kufitinishwa na wateule wake, wafanyabiashara wakubwa, wanaharakati, viongozi wa wafanyakazi na wengine wenye nia njema.

Hili laweza kufanyika kwa kuwa mpeleka ujumbe, ama hakuwaelewa vizuri wahusika au ana nia mbaya nao.

Si hivyo tu, rais aweza kuwekwa kiwewe kwa kupelekewa uzushi kuhusu usalama wa nchi, jambo ambalo siyo tu litashughulisha wengi, lakini pia ni ghali sana kuandaa ulinzi wa nyongeza; kwani rais hawezi kuamua kupuuza tu.

Siyo Rais Kikwete pekee mwenye simu ya mkononi. Marais wengi wana simu za mkononi. Lakini si kila mtu anaweza kuwasiliana nao moja kwa moja.

Hata ofisi kubwa kama zile za mashirika makubwa ya kimataifa, kuna simu ambazo huwezi kupata moja kwa moja mpaka uwe kwenye orodha ya wadau. Hii ni kupunguza usumbufu kwa kuweka mchujo muwafaka.

Ukijumuisha yote haya, utaona kwamba ama kumpigia rais simu au rais kupigiwa; yote yanageuzwa kuwa mambo ya mbwembwe tu; na hili halipingiki.

Rais anatumia simu moja – namba moja. Idadi ya watu wenye shida au maoni na wanataka kuwasiliana naye itakuwa kubwa sana. Kama kampuni yenye njia tano au hata kumi za simu inakuwa “bize” hadi kushindikana kufikika, itakuwaje namba moja ya rais?

Kinachohitajika siyo kupiga mbiu kutaka watu wampigie simu rais; bali kuimarisha taasisi za serikali zilizoundwa rasmi kwa kazi ya kupokea, kuchambua na kuwasilisha panapohusika, madai, matakwa na maoni ya wananchi.

Kwa mtindo wa kutaka kila mmoja aongee au achati na rais, basi taasisi ya urais itazidiwa na vitaarifa dhaifu badala ya hoja kuu za nchi na kwa maslahi ya wengi kupitia vyombo rasmi vilivyoundwa kwa kazi hiyo.

Hatimaye, simu ya rais na hata sms na maongezi, vitakosa tija. Licha ya siku kutofikika, rais anaweza kujikuta anafanya kazi alizopokea kwenye simu kuliko kwa mkondo wa wazi wa asasi za dola.

0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: