Sinare: Hatukulumbana tu, tulikubaliana


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa, Eve Hawa Sinare amesema malalamiko na malumbano yanayoendelea miongoni mwa wadau wa kahawa nchini, ni jambo la kawaida na wakati mwingine lisiloepukika.

Sinare amemwambia mwandishi wa habari hizi wiki iliyopita, kuwa kitu kimoja wasichozingatia baadhi ya wadau ni kwamba mwisho wa kikao cha wadau cha 24-25 Mei kilichofanyika mjini Morogoro, kulikuwa na makubaliano na maazimio ambayo wadau wengi hawajayapata.

Gazeti hili katika matoleo ya tarehe 13-19 na 20-26 Juni, liliripoti taarifa zilizomnukuu Mbunge wa Mbozi, Godfrey Zambi, akilalamika kwa waziri wa kilimo kuhusu uteuzi wa wajumbe wapya wa bodi ya kahawa, chini ya mwenyekiti Sinare; pamoja na kueleza kuwa mkutano wa wadau ulijaa malumbano badala ya kujadili maendeleo ya zao hilo.

Zambi ambaye ndani ya bunge wiki iliyopita wakati akichangia mjadala wa makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alitaka bodi hiyo ivunjwe, alisema baadhi ya wajumbe walioteuliwa na waziri wa kilimo, kwa nafasi zao sasa, wanaleta utata na ushiriki wao unadhihirisha “mgongano wa maslahi.”

Lakini, Sinare ambaye ameteuliwa na rais, amesema kama watu wanapinga uteuzi wa bodi, ipo nafasi ya waziri husika kufanya mabadiliko akiridhika kwa hicho kinacholalamikiwa.

Huku akizungumza kwa taratibu, Sinare alichomoa waraka na kumkabidhi mwandishi ukiwa na kichwa kisemacho, “Maazimio ya Kikao cha Wadau wa Kahawa Kilichofanyika Hoteli ya Nashera, Morogoro Mei 2012.”

Waraka aliosema una maazimio ya kikao cha wadau, una vifungu 15 juu ya maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:

 • Biashara ya kahawa mbivu iendelee kufanyika kama ilivyokuwa miaka ya nyuma mpaka mkutano wa mwaka ujao ambapo marekebisho na muafaka wa suala hili utakapoletwa upya. Kama mkulima hataki kuuza kahawa mbivu (red cherry) halazimishwi kuuza. Bodi itafuatilia katika maeneo ya Mbeya, Kigoma na Kagera ili kutathmini juu ya ununuzi wa kahawa mbivu kuhusiana na bei kwa mkulima na ubora.
 • Tathmini ya gharama zinazosababishwa na mfumo mzima wa utoaji wa leseni ifanyike kuangalia uwezekano wa kupunguza idadi kubwa ya leseni za biashara ya kahawa zilizopo sasa katika kanuni na sheria.
 • Utaratibu wa utoaji na usimamizi wa leseni za biashara ya kahawa uangaliwe upya ili kuiwezesha Bodi kuwa na mamlaka kamili juu ya suala hili na jinsi itakavyoshirikisha Halmashauri za Wilaya kwa utaratibu wa ugatuaji madaraka (D by D).
 • Kanuni mpya za kahawa zikishachapishwa katika Gazeti la Serikali (Government Official Gazzete) zisambazwe kwa wadau wote.
 • Tathmini ifanyike juu ya mfumo wa uzalishaji wa kahawa utakaochochea ongezeko la wingi na ubora wa kahawa.
 • Mwaka ujao yafanyike mapitio ya kanuni ili tuweze kuboresha maeneo mbalimbali.
 • Leseni za ununuzi wa kahawa mbivu zitatolewa pale tu baada ya kanuni mpya kutangazwa katika Gazeti la Serikali.
 • Katika kikao kijacho, Bodi ya Kahawa iwasilishe uchambuzi wa mnyororo wa thamani wa zao la kahawa kuanzia uzalishaji hadi kwenye soko. Uchambuzi huo uonyeshe mkulima anapata kiasi gani
 • Wadau wengi zaidi wachangie kadri iwezekanavyo na washiriki katika uzalishaji wa miche. Aidha, TaCRI itaweka utaratibu wa kutambua wazalishaji wa miche bora ya kahawa kwa kushirikisha mamlaka husika. Lengo ni kuzalisha miche milioni 200 katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Kila mwaka uzalishaji uwe miche milioni 20.
 • Serikali iendelee kutoa ruzuku ya miche na TaCRI iruhusiwe kuuza miche kwa Sh. 500 mmoja, ili kuwezesha kugharamia uzalishaji wa miche.
 • Kampuni/mashirika yanayotoa hati za ubora wa kahawa (Coffee Certification Standards) yatayarishe gharama zao halisi na kuwasilisha katika mkutano ujao wa wadau ili kutoa fursa kwa wadau kutoa mfumo unaowafaa. Aidha, kampuni zitatoa taarifa kuhusu mchakato/utaratibu unaohusika kupata usajili/hati. Taarifa hiyo itahusisha pia faida ya kusajiliwa.
 • Serikali kupitia Bodi na Taasisi zake ifanye tathmini ya udau wa wakulima katika vikundi na vyama vya wakulima kwa lengo la kuwang’amua wafanyabiashara waliojificha nyuma ya vikundi hivyo na kuchukua hatua kwa vikundi au vyama hivyo.
 • Viwango vipya vya uchangiaji wa maendeleo ya zao la kahawa vimekubalika kama ifuatavyo:

 • (i)    TaCRI (Fedha hizo zipelekwe ndani ya siku 5) – 0.75%
  (ii)   Uendeshaji wa minada (TCB) – 0.20%
  (iii)  Uendeshaji wa Ofisi na kazi za mfuko – 0.20%

 • Taarifa ya matumizi ya fedha hizo za mahesabu yaliyokaguliwa itolewe katika mikutano ijayo ya wadau.
 • Makundi ya wadau yaliyobainishwa katika kanuni yafuatiliwe kama ilivyo kwenye kanuni. Mwaliko rasmi wa makundi hayo upelekwe kwa wawakilishi wa vikundi hivyo ambavyo vitaamua ni nani ataviwakilisha kwenye mkutano huu. Kundi la wadau ambalo halina usajili kama kundi, wajaribu kujiunda kama kikundi kinachotambulika ama kuwasiliana ili kukubaliana kati yao nani awakilishe kundi hilo.
0
No votes yet