Siri ambayo Al adawi ameificha


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version

KUNA siri moja kubwa ambayo anayejiita mmiliki wa Dowans, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, hataki kuizungumzia katika mkakati wake wa kushinikiza serikali kununua mitambo yake, ama kuikodisha.

Siri hiyo ambayo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawataki kuizungumzia, wala watetezi wa Dowans hawataki kuigusia, ni deni la dola za Kimarekeni 184 milioni (Sh. 250 bilioni) ambazo kampuni hiyo inadaiwa na vyombo vya fedha.

Katika maelezo marefu yaliyojaa lugha ya vitisho na mikwara ya mbuzi, Al Adawi amekiri kuwa kampuni yake baada ya kuchukua mkataba wa kuzalisha umeme wa Richmond, ilitumia dola 109 milioni (Sh. 130 bilioni) kwa ajili ya  “kulipia mitambo, transfoma, vifaa vingine, wahandisi na gharama za kuiunganisha.” 

Hii ina maana kuwa mwaka 2006 hadi mwanzoni mwa 2007 kampuni ya Dowans ilipata fedha mahali za kuwekeza katika mitambo yake iliyopo Ubungo, Dar es Salaam. Swali ni hili. Je, mabilioni hayo ya fedha yalitoka wapi?

Kuna njia kadhaa ambazo zingemuwezesha Al Adawi kupata mabilioni hayo ya fedha katika siku chache za kupata mkataba: Kwanza, kutoka mfukoni mwake; pili, faida ya makampuni yake; tatu mabenki; ama nne, kuchangisha watu wa karibu ambao wangewekeza kwenye mradi huo kwa makubaliano ya kugawana faida itakayopatikana.

Kati ya njia zote hizo, njia ya kutoa mfukoni mwake kwa mfanyabiashara mkubwa kama yeye ni ngumu kuiamini kwa sababu inahatarisha uhai wa fedha zake.

Njia ya kutumia faida ya makampuni yake pia ni ya hatari hasa tukizingatia maelezo yaliyopo katika tovuti yake, kwamba kampuni yake inatengeneza faida ya dola 50 milioni, ingawa mwenyewe amejitapa kuwa anaingiza faida ya dola 200 milioni kwa mwaka.

Hakuna mfanyabiashara yeyote mwenye akili timamu na mwenye uzoefu wa karibu miaka 33 katika sekta ya biashara anayeweza kutoa fedha kwenye kampuni yake yenye faida na kuziingiza kwenye mradi ambao hana uhakika nao, hana uzoefu nao, na kibaya zaidi mradi huo upo katika eneo ambalo miradi mingine kama hiyo imetumbukia kwenye migogoro.

Hivyo njia pekee ambayo Al Adawi angeitumia ni kukopa benki na kukusanya mitaji toka kwa vyanzo vingine. Katika yote mawili la benki ni la hekima zaidi; benki kama Royal Bank of Canada ambayo anaushirika nao wa karibu ingeweza kutoa fedha hizo.

Al Adawi alisema kuwa alipoombwa na Rostam Aziz kuwekeza katika mradi wa umeme nchini aliambiwa kuwa serikali inataka “mwekezaji mwenye uwezo na ambaye anaweza kufanya kazi hiyo kwa haraka.”

Hivyo hapa tunaweza kupata mwanga kidogo wa kuwa chanzo cha dola 109 milioni hakikuwa benki peke yake, bali na vyanzo vingine ikiwamo matajiri wengine ambao wangetaka kuingia katika dili hilo.

Kwa hiyo, vyovyote alivyofanya Al Adawi aliweza kupata dola 109 milioni  ndani ya mwezi mmoja, kwani Dowans iliingia mkataba na Richmond huko Houston 14 Oktoba 2006 bila kupata idhini ya TANESCO na bila ya TANESCO kujua na wiki mbili baadaye majenereta ya kwanza yakaingizwa nchini.

Mtu yeyote mwenye ujuzi mdogo tu wa biashara ataweza kuhitimisha kuwa Al Adawi aliingia yeye mwenyewe katia deni hili aidha kwa kukopa kutoka kwa mabenki au kuwashawishi watu wengine kuwekeza. Naamini kuwa fedha nyingi zilizotoka kwa watu wa kawaida miongoni mwao wakiwa ni wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Hii ndio sababu pia ya kampuni kuandikishwa Costa Rica ambako wamiliki halisi wa makampuni wanalindwa kwa kiasi cha kutisha na vyanzo vyangu vya taarifa vinasema wamiliki wa Dowans ni zaidi ya mtu mmoja!

Kwa hiyo deni la kwanza ambalo liko nyuma ya Dowans ni hizo milioni 109 ambazo wamiliki wake wanahaha kutaka kuwabebesha Watanzania mzigo wake. Wanaotetea Dowans hawataki kulizungumzia hili kwa sababu linahusiana na ujio wa Dowans; na ubabe wa kujipatia mkataba kutoka kwa Richmond kinyume cha sheria.

Siyo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, wala ikulu wanaoweza kusimama hadharani na kueleza kuwa Dowans ilirithi mkataba feki wa Richmond – bali wataishia kusema, “ICC imesema mkataba huu ulirithiwa kihalali.”

Hata hili si kweli. Kilichorithishiwa 23 Desemba 2006 ilikuwa ni geresha. Mkataba tayari ulisharithiwa miezi miwili kabla ya TANESCO kulazimishwa kuidhinisha uhamisho huo. Bahati mbaya, hili wahariri wa vyombo vya habari waliokutana na Al Adawi hawakumuuliza na wala hawajaweza kumuuliza Rostam!

Wakati deni hilo la kwanza tunaweza kusema ni la kibiashara na la kupata mtaji na ambalo halitatizi sana, kampuni ya Dowans Tanzania Limited (DTL) nayo ikajikuta inajingiza katika mzigo mwingine wa madeni.

Kati ya Aprili na Novemba 2007, DTL chini ya Rostam Aziz ilikopa karibu dola 75 milioni kutoka benki za Barclays na Stanbic za jijini Dar es Salaam. Dhamana ya deni hilo ni mitambo ya Dowans iliyopo Ubungo, Dar es Salaam;  iwapo kiasi hicho fedha hakitarejeshwa, basi benki wanaruhusiwa kupiga mnada mitambo hiyo ili kufidia fedha zao.

Nakumbuka nilipata nafasi ya kumuuliza Al Adawi juu ya deni hilo na alikanusha kabisa kufahamu lolote kuhusu mkopo wa fedha hizo. Watu waliokaribu na Al Adawi wanasema hakuna kitu kilichomvuruga kichwa kama kuwapo kwa deni la dola 75 milioni!

Kwa hiyo hofu iliyotanda sasa ni kuwa deni lisipolipwa mitambo itakamatwa na vyombo vya fedha. Hii ndiyo siri amabyo “mmiliki wa Dowans” imemfanya kuja nchini kufanya “mazungumzo” na serikali ili “asamehe” sehemu ya tuzo ya Sh. 94 bilioni, lakini sharti serikali ikubali kuingia  mkataba mpya.

Kimsingi, Dowans haiwezi kusamehe deni bila mitambo yake kununuliwa au serikali kukubali kuingia mkataba mpya. Uamuzi wowote wa kusamehe bila moja kati ya hayo mawili kufanyika, kutaingiza kampuni hiyo katika mgogoro mkubwa wa kifedha utakaohatarisha hata mahusiano kati ya Rostam na Al Adawi.

Wapo wanaosema, hatua hiyo itafichua hata siri nyingine iliyojificha kati ya Al Adawi, Rostam na vigogo wengine wa serikali.

Swali kubwa ambalo tunahitaji kulijibu, ni ujasiri gani walionao viongozi wetu kwanza kufanya biashara na kampuni ambayo imeingia nchini kilaghai?

Lakini pili, kufanya biashara na kampuni ambayo kutokana na uzembe wake na tamaa ya kutengeneza faida kwa haraka, imejiingiza kwenye madeni makubwa ambayo haiwezi kutoka?

Sasa katika mazingira haya, kwanini serikali inataka kuwalazimisha wananchi kubeba Dowans ili kuikoa katika mikono ya benki, wakati kuna makampuni mengi ya umma na yale yanayoendeshwa na wazawa, serikali imeshindwa kuyasaidia kujikwamua katika mzigo wa madeni?

Lakini kubwa ambalo watawala hawaweza kulieleza ni hili. Serikali inahubiri tu – Dowans hailipiki, deni halipunguziki na mitambo haiwashwi – lakini haina mpango mkakati wa kukabiliana na upungufu wa umeme.

Nionavyo mimi, serikali haina uwezo wa kufikiria wala kutenda kitu kingine chochote nje ya Dowans, kwa sababu baadhi ya watendaji wake wametopea katika uzembe wa kufikiri. Wameshindwa kuwawajibisha watuhumiwa wakuu katika Dowans akiwamo Rostam Aziz na wenzake na wameshindwa  kuikamata mitambo ya Dowans na kuitaifisha.

Serikali makini ilitakiwa kutaifisha mara moja mitambo hiyo ili kupata suluhisho la kudumu la mgao wa umeme litakalorejesha hadhi ya serikali mbele ya wananchi.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: