Siri ya Kagoda hii hapa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version
Mkapa na Rostam watajwa
Peter Noni, Malegesi wamo
Rostam Aziz

USHAHIDI wa kwanza na muhimu kwamba fedha zilizoibwa na Kampuni ya Kagoda kutoka Benki Kuu (BoT) uliidhinishwa na viongozi wakuu nchini, sasa umepatikana, MwanaHALISI limeelezwa.

Waraka wa wakili aliyeshuhudia mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya kupata fedha hizo, unamtaja rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa miongoni mwa waliofanikisha mpango huo.

Katika andishi rasmi kwa Kamati ya rais Jakaya Kikwete ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), wakili huyo anakiri kuwa ni yeye alifanya attestation – “kushuhudia mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.”

Bhyidinka Michael Sanze, wakili katika kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers – ya Dar es Salaam, anasema katika andishi lake kuwa alishuhudia mikataba hiyo ndani ya ofisi za kampuni ya Caspian Construction Limited ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Aidha, kwa ushahidi wa Sanze, mbunge Rostam Aziz, ndiye kinara wa mpango mzima uliofanikisha wizi wa zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka BoT.

“Niliitwa na Bw. Malegesi ofisini kwa Bw. Rostam Aziz, 50 Milambo, Ofisi za Caspian Construction Limited. Nilipofika…niliwakuta Bw. Rostam Aziz, Peter Noni na Bw. Malegesi, wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake,” ameeleza Sanze.

Wakili anaeleza kuwa alikuta “documents – nyaraka zimeshaadaliwa ambazo niliombwa nizi-sign (niziweke saini). Nikauliza hizo fedha zinakotoka na nitathibitisha vipi kabla ya kusaini.”

Andishi la wakili linaeleza kuwa Rostan Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia Sanze kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana Ballali kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.

Wakati huo Peter Noni alikuwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchumi katika BoT. Hivi sasa ni Mkurugenzi wa Mpango ya Kimikakati. Ballali alikuwa gavana wa BoT. Alifariki dunia mwaka jana nchini Marekani.

Sanze anasema Malegesi aliishakwenda kujiridhisha  kwa Ballali na Katibu Mkuu wa CCM,Bw. Philip Mangula kuwa yaliyosemwa na Rostam yalikuwa kweli.

Hata hivyo Sanze anaongeza kuwa, “Rostam mwenyewe alisema, ‘system yote inajua.’” Anasema  kwamba baada ya maelezo hayo ya Rostam, alishuhudia mikataba hiyo kwa kusaini.

Kwa mujibu wa andishi la Sanze ambalo linathibitishwa kwa saini yake, Malegesi alimwita Noni ofisini mwake baada ya jina la Sanze kutajwa magazetini akihusishwa na Kagoda, lakini aliambiwa kuwa “nitulie tu serikali inalishughulikia swala hilo.”

Haya hivyo, Sanze anasema katika andishi hilo kuwa baada ya kumaliza kazi yake ya kushuhudia mikataba hakufuatilia kilichoendelea.

Hii ni mara ya kwanza Mkapa kutajwa katika sakata la kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, lakini ni mara nyingi Rostam amehusishwa na ukwapuaji huo ndani ya BoT.

Hata hivyo, haijathibitishwa iwapo kweli kulikuwa na kikao kinachomtaja Mkapa akiamuru gavana Ballali kutoa fedha kwa Rostam, kwani kauli ya Sanze inatokana maelezo ya Malegesi na Rostam Aziz; ama ukiwa ukweli au njia ya kumshawishi Sanze kushuhudia mikataba ya Kagoda.

Kwa miezi 15 sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikikana kushiriki au kutumia fedha zilizotokana na wizi uliofanywa na Kagoda ingawa kimeshindwa pia kuthibitisha kilipopata mabilioni ya shilingi kugharamia kampeni zake ghali za uchaguzi mkuu wa 2005.

Katibu Mkuu Yusuph Makamba na Katibu Mwenezi  John Chiligati wamekana chama chao kutumia fedha za EPA katika uchaguzi mkuu wa 2005. Wamesema kama kuna aliyechukua fedha hizo, basi hakutumwa na chama chao bali ni kwa matumizi yake binafsi.

MwanaHALISI liliwasiliana na wakili Sanze kupitia simu yake ya mkononi, likitaka kujua undani wa andishi lake. Sanze alimwambia mwandishi wa habari hizi, “Siwezi kujibu swali hilo.”

Alipoulizwa kwa nini aliitwa na Malegesi kushuhudia mikataba wakati yeye Malegesi alikuwepo alisema, “Hilo muulize Malegesi mwenyewe.”

Kuhusu kampuni yake kupata mgao na kuchangia CCM na kama kuna risiti inaonyesha walitoa mchango huo, Sanze alisema kwa ufupi, “Sijui lolote. Niambie wewe. Sijui zilitoka mwaka gani.”

Alipong’ang’anizwa kuhusu kuchangia CCM alijibu, “Nikuulize wewe kama zilitoka lini.”

Wakati wote simu ya Malegesi ilijibu kuwa haipatikani. Simu ya Rostam Aziz ilijibu pia kuwa hapatikani lakini ujumbe ulioandikwa na kumwomba awasiliane na mwandishi, ulionyesha kuwa umepokelewa. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, Rostam hakuita.

Namba ya simu ya Mangula nayo ilisema kuwa hapatikani. Mwanasheria Mkuu wa serikali Johnson Mwanyika hakupatikana kuzungumzia andishi la Sanze.

Wiki iliyopita vyombo vya habari viliripoti kuwa 26 Januari mwaka huu, Malegesi alikula kitu kilichodaiwa kuwa sumu na kulazimika kulazwa hospitali ya Mikocheni, Dar es Salaam.

Uvumi ulioenea jijini Dar es Salaam unasema inawezekana Malegesi amelishwa sumu kwa makusudi kwa kuwa ni mtu muhimu katika sakata la Kagoda linalogusa watu wengi na wa nyadhifa mbalimbali.

Ni miezi tisa sasa tangu Daudi Ballali aage dunia kutokana na kile kilichodaiwa “kulishwa sumu” huku akieleweka kuwa mtuhumiwa mkuu au shahidi muhimu katika wizi mkubwa ndani ya BoT.

Gazeti la Nipashe Jumapili, 8 Februari 2009 limeandika kuwa Malegesi alitumia siku 11 hospitalini Mikocheni akipata matibabu ya kuondolewa sumu anayodaiwa kuipata kwenye chakuka.

Muuguzi mmoja aliliambia gazeti hilo kwamba hawawezi kutoa taarifa yoyote juu ya aina ya sumu au lolote walilobaini katika vipimo bila ruhusa ya mgonjwa mwenyewe.

Kampuni ya Kagoda ilikwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka akaunti ya EPA, ikiwa ni wiki moja baada yakusajiliwa. Kampuni ilitawanya fedha hizo katika matawi saba ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.

Ni takriban mwaka mmoja sasa tangu rais aunde Kamati ya watu watatu kuchunguza wizi katika akaunti ya EPA, ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali Johnson Mwanyika. Wengine ni Mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hosea na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema.

Haijafahamika iwapo wote ambao Sanze ametaja kwenye andishi lake walihojiwa na Kamati. Lakini taarifa zilizopo zinasema rais mstaafu Mkapa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, hawajawahi kuhojiwa.

Mwishoni mwa mwaka jana, waandishi wa habari walimuuliza Waziri Mkuu Mizengo Pinda iwapo serikali inaogopa kukamata na kushitaki wahusika katika Kagoda; lakini alijibu kuwa, “Wahusika wote watafikishwa mahakamani.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: