Siri ya kuu ya kuuza Kigamboni


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
Kigamboni

WAKAZI WA wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam, wameshutumu serikali kwa kusema mpango wa kuwahamisha ili kupisha wawekezaji kutoka nje ni “wizi mtupu.”

Wamedai kuwa mradi wa Kigamboni ni wa kupatia fedha za CCM za kufanyia uchaguzi Oktoba 2010.
 
Siyo siri tena kwamba wakazi wa Kigamboni watapewa “fidia,” watahama au kuhamishwa ili kupisha wawekezaji kutoka nje ambao wanadaiwa watafanya Kigamboni kuwa eneo la kisasa.
 
Uhamishaji utafanyika mwaka huu. Anayetajwa kuwa “dalali” wa Kigamboni ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Zephania Chiligati.

Kwenye uwanja wa Swala, Kigamboni wananchi walimwambia Chiligati,“Huu ni wizi mtupu, sawa na EPA. Ninyi watu wa CCM mnatafuta fedha za kampeni za uchaguzi 2010.”

Wanajeshi wastaafu wamehoji, “Je, askari kastaafu, kapata malipo yake, anaambiwa aondoke kambini lakini nyie (Chiligati) mnamzuia kujenga nyumba eneo lake, sasa watoto wake wakalale wapi, apeleke wapi familia yake?” Chiligati alishindwa kujibu.

Tayari Chiligati amewatangazia wakazi wa Kigamboni kuwa eneo hilo linahitaji “kuendelezwa” na ametaja sababu zifuatazo.

Kwanza, ongezeko la watu jijini la asilimia saba kwa mwaka. Pili, Kigamboni kuwa sehemu ya jiji kwa mujibu wa sheria. Tatu, Kigamboni kuwa karibu na jiji na kuwa na mandhari nzuri ya kuvutia watalii.

Taarifa zinasema tayari mnunuzi amepatikana lakini Chiligati hajawahi kumtaja. Kuna wanaosema mwekezaji ni Mwarabu wa Bahrein; wengine wanasema ni Waarabu wa Dubai; lakini wapo wanaodai eti ni rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush.

Naye Chiligati anasema tayari hatua ya “kuendeleza” Kigamboni imetangazwa kwenye gazeti la serikali ambako inaonyeshwa kuwa kutakuwa na mpango kabambe wa kuijenga upya.

Katika mikutano yake ya Januari 16 (Chadibwa Beach), Machi 18 (Uwanja wa Swala- Tuangoma) na Machi 19, 2009 (Vijibweni) wilayani Temeke, Chiligati alirudia mara kadhaa kuwa madhumuni ya kuswaga wananchi nje ya Kigamboni ni kujenga mji uliopangika.

Alisema serikali inataka mji wenye mifumo mizuri ya majengo; wenye huduma za jamii, wenye maeneo ya wazi, wenye maeneo ya uwekezaji na mji wenye mfumo wa kisasa wa mawasiliano.

Chiligati aliwaambia wananchi kuwa mchakato wa utekelezaji utakuwa pamoja na kutoa tangazo la kusudio alilosema litatoka 24 Oktoba mwaka huu, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi, kutafuta mtaalamu mbunifu wa mji na kuwatambua wakazi na miliki zao.

Waziri alitaja jukumu jingine kuwa ni kutangazia wawekezaji, kulipa fidia na kuunda mamlaka ya usimamizi wa mradi.

Alisema wananchi watakaokumbwa na upitishaji miundombinu watapewa viwanja maeneo ya makazi na kulipwa fidia; watakaoamua kuuza maeneo yao watalipwa fidia na wawekezaji na kupewa viwanja maeneo ya makazi; na watakaoamua kuwekeza wataingia ubia na wawekezaji hao.

Tangazo la kusudio la mradi linalenga kutoa notisi na kuwapiga marufuku wananchi wa Kigamboni kuyaendeleza maeneo yao kwa kuwa watahamishwa.

Hapa ndipo penye mvutano. Baadhi ya wananchi wanahoji itakuwaje wapigwe marufuku kuyaendeleza maeneo yao wakati ndiyo kwanza mchakato wa kutwaa Kigamboni unaanza na wenye ardhi hawajakubaliana?

Wasiwasi wa wananchi unatokana na usiri uliotawala taarifa za “mradi wa Chiligati.” Wizara ya Ardhi haikutoa taarifa yoyote hadi pale habari hizo zilipoandikwa na gazeti la kila siku la KuliKoni.

Vilevile wadau ambao watapokonywa ardhi hawakuhusishwa tangu mwanzo, ikiwa ni pamoja na mbunge na diwani wao. Nayo halmashauri ya jiji iliwahi kukana kufahamu mradi huu.

Wasiwasi unaongezwa na hatua ya Chiligati kuwa mtoa elimu badala ya mamlaka ya kusimamia mradi, ambayo hadi sasa haijaundwa, au viongozi walio karibu na wananchi.

Kinachoshangaza wengi ni kwa nini serikali haikutoa elimu kabla ya kufikia maamuzi? Kwa hiyo, kinachoitwa elimu ya Chiligati kinachukuliwa kuwa uamuzi umefikiwa na sasa wajiandae kusambaa.

Kuna taarifa kwamba mwekezaji hataonana na mwananchi mwenye ardhi bali waziri na wataalamu wake. Wataalamu ni pamoja na wale wanaotuhumiwa na wananchi kupora viwanja kumi au ishirini kila mmoja na kuwakosesha wananchi walioathirika kwa bomoabomoa ya Ubungo, Kurasini na maeneo mengine.

Suala la ubia pia ni jambo lisilowezekana, kwa kuwa Kigamboni hakuna mwananchi mwenye mabilioni ya shilingi ya kuwekeza katika  magorofa ya “kupamba mji.”

Hii si mara ya kwanza kwa Chiligati kufika Kigamboni na mradi wa kuuza ardhi ya wananchi. Iliwahi kutokea wakati Kitwana Kondo (KK) akiwa mbunge wa Kigamboni, huku Chiligati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Alipima eneo la Vijibweni bila fidia na KK akawaongoza wananchi kugomea ardhi yao kuchukuliwa bila fidia; badala yake viwanja hivyo viliuzwa na wenye ardhi.

Kitongojini Vijibweni, mzee mmoja alipora kipaza sauti kabla ya mkutano kuanza na kuwatangazia wananchi waondoke katika mkutano huo kwa sababu Chiligati aliwadharau kwa kutofika siku aliyoadhidi na kwamba siku hiyo alipofika alikuwa amechelewa.

Wengi waliondoka na Chiligati alibaki kuhutubia watu wachache, wengi wao wakiwa watoto.

Kwa mikutano ya Kibada na Mjimwema, Chiligati aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Abdallah Kihato ambaye alitofautiana na bosi wake kwa kudai kuwa wananchi watakubaliana na wawekezaji na siyo kuwakilishwa na serikali.

Kihato alilazimika kutoa lugha ya matusi aliposhindwa kujibu swali la mtu mmoja anayeitwa Machano. Machano alisema, Wewe  (Kihato) na wote waliokutuma ni wanafiki.”

Naye DC Kihato akajibu, “Shekh Machano ulienda jando gani wewe, la porini au la hospitali?” Wakazi wa Pwani wanaamini aliyekwenda jando la porini hufunzwa heshima na adabu.

Alipofika Mjimwema Kihato alishindwa kujibu kwa nini ardhi ya mfanyabiashara wa asili ya kiasia, aliyetajwa kwa jina la Manji, ipatayo hekta 760, haikuingizwa kwenye mradi wa serikali wa kuiuza Kigamboni.

Muuliza swali hakueleza ni Manji yupi. Mfanyabiashara Yusuf Manji aliwahi kuomba ubunge katika jimbo la Kigamboni.

Kutokana na hali inavyokwenda, wananchi wa Kigamboni wamejipanga kupinga mradi huo mahakamani. Tayari wameanza vikao vya mkakati.

Madai ya baadhi ya wananchi ambayo hayajaweza kuthibitishwa yanasema mradi wa Kigamboni ni wa kupatia fedha za CCM za kufanyia uchaguzi Oktoba 2010.

Kumekuwa na madai kutoka kambi ya upinzani kwamba mwaka 2005, CCM ilitumia makada wake kuchota mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT).

Ardhi ya Kigamboni ndiyo pekee katika jiji iliyosalia yenye thamani kubwa, iliyo karibu na jiji, inayouzika haraka na ambayo wakazi wake wengi ni walalahoi wasiojua mtu yeyote ikulu wa kuwasemea.

Lakini, Kigamboni iliyo karibu na jiji, yenye pantoni kubwa ya kubeba magari 60 na abiria 2,000; inayojengewa daraja la njia sita pamoja na reli ya Vijibweni, haiwafai tena walalahoi. Je, wananchi wana ubavu wa kuzuia isichukuliwe?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: