Siri ya Sheikh Yahya yafichuka


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version
Sheikh Yahya Hussen

CHANZO cha vitisho vilivyotolewa na Sheikh Yahya Hussen kwamba atakayempinga Rais Jakaya Kikwete atakufa ghafla kimefahamika.

Taarifa za kuaminika ambazo MwanaHALISI limepata, zinasema “msukumo wa kisiasa” ndio ulimtoa Sheikh Yahya “pangoni kujaribu kumnusuru rafiki yake” Kikwete.

Msukumo wa kisiasa uliosababaisha matumizi ya utabiri na vitisho unadaiwa kusababishwa na kundi kubwa la viongozi wa sasa na wa zamani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambalo limejipanga kuweka mgombea urais mbadala katika uchaguzi ujao.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, nchi nzima imevamiwa na “siafu” wanaokutana na kila mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mjumbe wa Mkutano Mkuu, kushawishi mabadiliko makubwa katika vikao vya chama mapema mwaka kesho.

Taarifa zinasema hadi mwishoni mwa Septemba, wajumbe kutoka kundi hili ambao wameitwa “siafu” kutokana na kuvamia nchi nzima, walikuwa wamekutana na kukubaliana na wajumbe 80 wa NEC wanaotaka mgombea urais tofauti ndani ya CCM.

Aidha, tayari kundi hilo ambalo linaongozwa na msukumo wa “Kikwete ametusahau na ameacha tudhalilishwe,” limeorodhesha wajumbe 1,200 kati ya wajumbe 1,700 wa Mkutano Mkuu ambao ndio hutoa maamuzi ya mwisho juu ya mgombea urais.

Taarifa zinasema mratibu wa mpango huo ni mkuu wa mkoa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambaye amepewa jukumu la kujenga mtandao wa kuweka mgombea mbadala “iwapo Kikwete hatabadili msimamo wake wa kuwatenga.”

Miongoni mwa wanaotajwa kuweza kuingia katika mbio za kuwania kiti hicho ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye amekuwa katika juhudi za “kujisafisha” kutokana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa Richmond.

“Si unajua Kamati ya Mwinyi itawasilisha ripoti yake hivi karibuni kwa rais? Tayari watu hawa wamevamia mikoa yote kukutana na wajumbe wa NEC ili ripoti ikiwabana wapate watu wa kuwatetea,” ameeleza mtoa taarifa.

Wiki iliyopita, Sheikh Yahya aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam, kwamba Kikwete ndiye atakuwa rais mwaka kesho na kwamba yeyote kutoka ndani ya CCM ambaye atajitokeza kumpinga, atakumbana na kifo cha ghafla.

Utabiri wa Sheikh Yahya ambao Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu amesema ni maoni binafsi na yanayostahili kuheshimiwa kama maoni ya mtu mwingine, unatajwa kuwa “jibu sahihi kuzima njama za kumwangusha Kikwete.”

“Amelenga kuwapiku, ikibidi kwa vitisho, kwani tayari wamekwenda mbali,” ameeleza mtoa taarifa.

Mtoa taarifa ananukuu kauli ya Naibu Waziri wa Miundombinu, Makongoro Mahanga ambaye ameripotiwa kusema kuwa katika serikali ya sasa ya Rais Kikwete, “hakuna mtu mwenye nguvu zaidi ya Lowassa.”

Makongoro anadaiwa kusema hayo wakati wa mahojiano ya wabunge na Kamati ya Mwinyi iliyoundwa na Kamati Kuu ya CCM kutafuta chanzo cha “chokochoko” miongoni mwa wabunge na kati ya wabunge na serikali.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, “Lowassa ni mwanamme wa shoka,” jambo ambalo lilizua mtafaruku ndani ya kikao cha Mwinyi.

Hoja za kumtetea Lowassa zimekuwa zikitolewa mara kwa mara. Makongoro na Simba wanaongeza chumvi tu lakini wabunge kama Peter Serukamba wa Kigoma Mjini wamekuwa nje nje kumsemea kama alivyofanya siku Lowassa alipojiuzulu nafasi ya waziri mkuu, Februari mwaka jana.

Wakati hayo yanafanyika, tayari imethibitika kuwa mtandao uliomwingiza madarakani Kikwete mwaka 2005, umesambaratika. Mtandao huo ulikuwa na viongozi wakuu watano akiwamo Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta.

Mbali na Sitta, wengine ni Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Hivi sasa Lowassa na Rostam wamo katika kundi moja wakati Membe na Sitta wamo kundi jingine. Rais Kikwete, labda kwa siri, lakini hajaonyesha kuwa upande wowote.

Bali wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema kwa vile Kikwete amekuwa kimya juu ya tuhuma zinazomkabili Rostam na aliwahi kusema kuwa kilichompata Lowassa ni “ajali ya kisiasa,” ameacha watafunane ili aweze kujiunga na mshindi jambo ambalo linaweza kumjengea uhasama na pande zote mbili.

Kauli ya ikulu hata hivyo, kwamba vitisho vya Sheikh Yahya kuwa watakaompinga Kikwete watakufa ghafla ni maoni yake binafsi, imechukuliwa kuwa ni kuimarisha woga na inalenga kudhoofisha wapinzani wa Kikwete.

Naye mbunge wa Maswa, John Shibuda ambaye tayari ametangaza kugombea urais kupitia CCM, amepinga utabiri wa Sheikh Yahya na kumtuhumu kuwa “anatumiwa.”

Shibuda ameliambia gazeti hili kuwa atachukua fomu na kwamba ana hakika kuwa hatakufa kwa vile anajua Mungu hayuko pamoja na “washirikina.”

Taarifa zimeeleza kuwa mjumbe ambaye amepewa jukumu la kujenga mtandao wa kumwengua Kikwete, ana uzoefu wa kujenga mtandao kama ule uliomwingiza rais madarakani mwaka 2005.

“Huyu bwana…ni yuleyule aliyejenga mtandao wetu wa mwaka 2005 ambao ulimwingiza Rais Kikwete madarakani na kupata nguvu kubwa ndani ya chama,” kimeeleza chanzo cha taarifa hii.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: