Siri za Nape nje


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Ni zile zinazomhusu Lowassa
Profesa Mwandosya pia atajwa
Nape Nnauye

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amejiingiza katika mradi wa kutafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, imefahamika.

Andishi la 14 Julai 2011 lililotoka kwa ofisa mmoja wa idara ya usalama wa taifa kwenda kwa Nape linaeleza namna mkakati huo utakavyotekelezwa. Nape anadaiwa kutumiwa na baadhi ya viongozi wa CCM wanaosaka kwa udi na uvumba urais wa Muungano.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa walengwa wakuu kutoka moja ya kambi inayoungwa mkono na Nape, ni waziri wa maji, Profesa Mark Mwandosya.

Akiandika kwa njia ya msisitizo, mwandishi aliyejipa jina la Lucy Mwandosya anasema, “…hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumuacha Profesa Mwandosya katika wizara ya maji kutamfanya awe kipenzi cha wanawake ambao ndiyo wadau wakuu katika sekta hiyo.”

Inadaiwa mwandishi ametumia jina la Lucy Mwandosya ili kuzubaisha baadhi ya wanasiasa. Lucy Mwandosya, ni mke wa Profesa Mark Mwandosya ambaye kwa vyovyote vile asingeweza kuingia katika mkakati mchafu wa kuimharibia mumewe, lakini pia mama huyo hana utamaduni wa kujiingiza kwenye harakati za kisiasa, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanasema limelenga mkakati wa Nape wa kupima upepo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Nape alimuunga mkono Profesa Mwandosya na alikuwa mmoja wa watu wa karibu katika kambi ya John Malecela na Fredrick Sumaye.

Akiandika kwa ukali Lucy “feki” anasema, “Iwapo (Profesa Mark Mwandosya) atatumia fursa aliyopata kuzindua na kujihusisha na miradi ya maji mijini na vijijijini, kuna uwezekano mkubwa wanawake wengi ambao ndiyo wapiga kura),wakamuunga mkono. Hivyo suala hilo liangaliwe kwa makini na ikibidi lisipewe nafasi.”

Mawasiliano ya Nape na msiri yameegemea zaidi katika minendo ya waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashifa ya Richmond, Edward Lowassa. Wanasema, “Lowassa tayari ameanza kampeni kabla ya wakati, na kwamba kwa njia hiyo, itakuwa ni vigumu kumsimamisha.”

Akiandika kwa uchungu, mtoa taarifa anasema, “…Kinachofanyika sasa, ni sawa na kusema Lowassa ameanza kampeni rasmi. Wakati wenzake wakisita kujitokeza ama kwa kuogopa kutajwa au kwa kutokujua mbinu, yeye ameanza kukutana na watu wa rika tofauti, jumuia, dini na makundi mbalimbali ili kuthibitisha ni kiongozi wa kitaifa na ambaye siku chache kabla ya Bunge kuahirishwa atatoa kauli nyingine nzito ili kuendeleza mjadala na hatimaye kumuweka juu kisiasa.”

Hata baadhi ya “vyombo vya habari maalumu,” anasema tayari vimeingia katika diri la kumpeleka Lowassa ikulu. Hata hivyo, msiri huyo anasema, “suala hilo nitalieleza vizuri baadaye katika mazungumzo yetu ya simu.”

Anasema jukumu kubwa la vyombo vya habari ni kuchapishwa taarifa zenye lengo la kumpamba Lowassa, ili baadaye ziweze kutumiwa na idara ya usalama wa taifa kumfagilia. Anasema lengo kuu la mpango huo, ni kutaka kuonyesha Lowassa ndiye anayekubilika miongoni mwa wanachama wa chama hicho.

Akizungumzia utekelezaji wa mkakati wa CCM wa kujivua gamba, “msiri” huyo wa Nape anasema, mkakati huo ni mgumu kutekelezwa kutokana na hatua ya watuhumiwa kukutana na baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwashawishi kutouunga mkoano mpango huo.

Mawasiliano kati ya Nape na msiri wake yalifanyika 14 Julai 2011, siku moja baada ya Rostam Aziz kutangaza kuachia uongozi.

“Anasema kuna jitihada kubwa zimewekwa kupinga hoja ya kujivua gamba katika vikao vya chama vitakavyofanyika mjini Dodoma.”

Anasema tayari watuhumiwa hao watatu Lowassa, Rostam na Andrew Chenge wamekutana na viongozi mbalimbali wenye ‘uzito’ kwa ajili ya kuwaomba kuwatetea kwenye vikao hivyo. Miongoni mwa walionwa na kuombwa kufanya kazi hiyo, ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Naye Nape akijibu ujumbe kutoka kwa msiri wake anasema, “Nimekupata. Nafahamu kuwa viongozi hao ambao wanashiriki kwenye vikao vyote viku vya CCM, watasimamia utetezi kuwa hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya Lowassa, Chenge na Rostam, zitakuwa zinakwenda kinyume na utawala wa sheria.”

Anasema aliyepewa jukumu la kuongelea suala hilo ndani ya vikao vya chama, ni Rais Mwinyi ambaye katika kusisitiza hoja yake atasema, “hatua yoyote ya kuwafukuza Lowassa na wenzake katika chama itachukuliwa kuwa ni kuwachukia wakristo.”

Anasema, “kauli hiyo itaungwa mkono na Rais mstaafu wa Zanzibar ambaye atashawishi suala hilo lishushwe hadi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili kufanyiwa uamuzi. Anasema ni katika kikao hicho, ndipo wajumbe waliopangwa wataibuka na kupinga utaratibu wa kumfukuza Lowassa na wenzake.

Naye msiri wa Nape katika mradi huu anaeleza, “Ni kweli. Kwa wale ambao hawajaingia kundini, ushawishi wenye lengo la kuwavuta utaendelea.” Anasema wahariri wengi watazidi kuvutwa na kulishwa ‘sumu’ kwenye mkutano mwingine utakaofanyika mjini Arusha kuanzia 14 Julai 2011.

Akiandika kwa njia ya taarifa mpya, mtoa taarifa huyo wa Nape anasema, “…Kitakachofanyika ni wajumbe kupinga hatua kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa kwa madai kwamba hawajafikishwa mahakamani. Watasema kama hatua zitachukuliwa, ni bora wao wahesabike kuwa walikuwa nje ya kikao – “wata walk out.”

Anasema, “Kitendo hicho kitawashtua baadhi ya viongozi ambao wataomba msimamo huo ubadilishwe ili kunusuru chama na watataka watuhumiwa hao wasamehewe.”

Anasema nguvu nyingine imewekwa katika kukamata wahariri wa vyombo vya habari na uchaguzi wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi.

Anasema, “taarifa sahihi ni kuwa kambi ya Lowassa imekubaliana huyo bwana aendelee kujitokeza kwenye maeneo ya umma ili wananchi waendeleze mjadala juu yake. Lengo ni kuvuta ushawishi.”

Hata hivyo, mawasiliano ya wawili hao yanaonya kutomshirikisha katibu wa NEC, Mambo ya Nje, January Makamba. Anasema January ndiye anayetumika kupokea maelekezo kutoka kwa baaadhi ya viongozi na kuyapeleka kwa Lowassa. Hakufafanua.

Anasema, “Tahadhari kubwa imeelezwa kuwa inapaswa kuchukuliwa kutokana na mazingira yalivyo katika uongozi wa sasa na hasa sekretarieti ambayo imenza kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuwaondoa katika nafasi zao makatibu wa CCM katika baadhi ya mikoa.”

Mikoa inayotajwa ni Shinyanga, Dodoma na Kagera ambayo wanasema viongozi wake walikuwa ni kutoka kambi ya Lowassa.

Anasema, “…Lowassa atakuwa akizungumza na kuchangia hoja na mbalimbali katika jamii ikiwa ni sehemu ya kumfanya aonekane na kukumbukwa. Taswira nzima inalenga kumuonyesha ni mtu jasiri na anayefaa kuwa kiongozi wa nchi.”

Tayari Lowassa amezungumza bungeni na kusema, “serikali ina ugonjwa wa kutofanya maamuzi magumu.” Alisema ni kheri kulaumiwa kwa kufanya maamuzi, kuliko kulaumiwa kushindwa kufanya maamuzi.”

0
Your rating: None Average: 3.5 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: