'Siri za serikali' zinalenga kulea ufisadi


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version

MBUNGE wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa alipouliza bungeni wiki iliyopita, nini hasa 'siri za serikali,' kulizuka hofu. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Philip Marmo, hakujibu ila alitisha wabunge.

Dk. Slaa amejitokeza kuwa mbunge machachari hasa au tuseme muwajibikaji makini kwa wananchi. Anaukalia utawala kooni kwa kila anachoona hakiendi sawa.

Anahoji ufisadi hata pale anapopewa majina na kusakamawa. Kama alivyoapa kuitumikia katiba, hajali kama viongozi akiwemo Rais Jakaya Kikwete wanakasirika kwa anayoyahoji.

Anajua serikali imetangaza vita dhidi ya ufisadi lakini yeye hachoki kuibana kwa sababu haoni matunda ya vita hiyo. Anachokiona ni kile wanachokiona Watanzania; ubabaishaji na upotoshaji mambo.

Ukweli upo wazi. Serikali yenyewe, kwa maana ya baadhi ya watendaji wake wakuu wanashirikiana na mashirika wao kuendelea kufisidi nchi. Wanakabiliwa na tuhuma nzitonzito.

Katika kuwa kwake mstari wa mbele kuibana serikali, Dk. Slaa hujikuta akitumia nyaraka za serikali zikiwemo zile zinazopigwa muhuri wa 'SIRI.' Ndio msingi wa swali lake kwa serikali.

Dk. Slaa anamwaga hadharani yaliomo kwenye nyaraka za serikali, lakini anafanya hivyo kwa sababu wananchi wanampatia. Kwa hivyo serikali haitunzi siri zake vema. Kama zinatoka, ina maana kuna tatizo ndani ya serikali.

Hizi ni nyaraka zinazohusu vikao vya siri na zipo nyaraka zinahusu ripoti za uchunguzi na utafiti wa mambo yanayogusa maslahi ya Mtanzania na mustakbali wa Taifa.

Sasa Waziri Marmo, aliyewahi kushika Ofisi ya Katiba na Utawala Bora, kabla ya mabadiliko ya kwanza ya Baraza la Mawaziri, anasema kutwaa nyaraka za siri za serikali ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.

Kweli ipo sheria inayozuia siri za serikali kutangazwa au kukutwa mikononi mwa asiyehusika. Sheria hiyo ilitungwa ili kulinda yaliyoitwa 'maslahi ya taifa.'

Nchi mbalimbali barani Afrika hutumia sheria ya aina hii. Lakini matumizi yake hayalengi kwenye maslahi ya taifa ila zaidi, ya watawala kupitia njia ya kuficha maovu yake.

Tawala nyingi Afrika huendesha mambo kwa kupindisha sheria na kuvunja misingi ya utawala bora na haki za binadamu. Hutumia sheria hiyo na nyinginezo kukusanya utajiri huku zikizidi kujichimbia madarakani.

Tanzania haijasalimika maana inaendelea kutumia sheria mbovu kulinda inachoita 'siri za serikali' hata pale panapokuwa jambo lenyewe ni ufisadi unaoangamiza taifa.

Mfano wa ujanja kwa nyaraka za siri za serikali duniani ni pale mwaka 1977, serikali ya makaburu wa Afrika Kusini ilipotangaza kuwa mpigania uhuru maarufu wa kizalendo, Steve Biko, amejiua kwa kujinyima chakula akiwa mahabusu.

Bunge la nchi hiyo lilijadili taarifa hiyo na mmoja wa mawaziri akamsifia waziri aliyehusika na mambo ya ndani kwa kuwapa wafungwa uhuru wa kujiua kwa kutokula.

Lakini mwandishi Donald Woods alifanya kama anavyofanya Dk. Slaa leo. Aliizidi akili serikali na kufunua mbinu zake za kuficha ukweli. Woods alitumia ujanja kuupiga picha mwili wa Biko na akasambaza picha zile ulimwenguni kote.

Ingekuwa ni miaka hii angezisambaza picha zile kwenye internet pia.

Kwa hivyo suala kubwa, kama alivyohoji Dk. Slaa kwenye Bunge, ni nyaraka zipi za serikali zinapaswa kuwa siri – zile ambazo kwa dhati zinalinda maslahi na usalama wa taifa, au zile zinazolinda ufisadi unaofanywa na wakubwa?

Na hilo ndilo swali la msingi ambalo Waziri Marmo alionekana kupata kigugumizi katika kulielezea kwa ufasaha.

Dk. Slaa alihoji kama kweli nyaraka za serikali zilizojaa kumbukumbu za ufisadi na ambazo wabunge waliziomba kwa utaratibu wa kawaida na kunyimwa zinaweza kuitwa ni za siri.

Maana hapa, suala la maslahi (na hata usalama) ya taifa halipo kwa sababu, kwa mfano, kuziainisha nyaraka za kumbukumbu za ukwapuaji fedhsa za umma katika Akaunti ya EPA ilioko Benki Kuu ya Tanznaia (BoT), si suala la kulinda maslahi (au usalama) huo.

Kinyume chake ndicho hasa kingepaswa kuwa sahihi –kwamba kuzianika nyaraka hizo hadharani. Ingelikuwa ni nyaraka zinazohusu vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, hapo kila mtu angeelewa. Sivyo sasa, ni ufisadi tu dhidi ya mali na raslimali za taifa.

Kitendo cha kuzianika hadharaani kumbukumbu za ufisadi katika EPA ni halali maana serikali inajigonga katika kueleza ukweli wa ufisadi huo. Ilisema fedha zinarudishwa lakini haitaji nani wanaozirudisha. Lakini pia laiti kama siri hazikuanikwa, hata hizo fedha zisingerudishwa.

Inaonekana serikali iko tayari kutumia sheria kulinda ufisadi na mafisadi, na hili Dk. Slaa alilitamka aliposema haelewi mantiki ya nyaraka hizo kuwa siri wakati hazina faida au maslahi kwa taifa. Anayoona ni maslahi ya wachache.

Umuhimu wa usiri kwa nyaraka za serikali unafahamika, lakini inapofika mahala mfumo wa serikali unaporomoka na siri zinavuja, hiyo ni janga.

Na kwa upande wake, serikali ingepaswa pia kutulia na kujiuliza kwa nini nyaraka za kumbukumbu za siri, za wizi wa EPA kwa mfano, zimevuja na kutua kwa wabunge wa upinzani?

Dk. Slaa alisema kuna wananchi wema wenye uchungu zaidi kwa taifa lao (kuliko hata uchungu ilionao serikali yenyewe) wameona maana ya kuziiba na kuzifikisha kwa wabunge wenye ujasiri wa kuzitumia kuihoji serikali.

Masuala ya ufisadi yakiachiwa tu yanaweza kuliangamiza taifa na hata kuzua migogoro ya kijamii. Athari hii imeonyeshwa mwanzoni kabisa (kwenye Preamble) katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Prevention and Combating of Corruption Bureau Act) iliyopitishwa mwaka 2007, kwa hivyo ni athari inayotambuliwa hata na serikali yenyewe.

Ajabu ni kwamba pamoja na serikali kutambua hilo, bado inafanya mzaha na inavyoonekana inatumia muda mwingi kujaribu kufunika au kutumia vitisho kwa wanaoihoji iseme ukweli.

Dk. Slaa, kama walivyo wale wanaozivujisha siri za serikali, ni wapiga filimbi tu ambao tungekuwa katika nchi makini katika kuzuia ufisadi, wangepongezwa badala ya kutishwa.

Muswada ya Sheria ya 'kulinda wapiga filimbi' wa masuala ya ufisadi bado haujapitishwa. Sheria hii ilikuwa itumike sambamba na ile Sheria mama ya TAKUKURU pamoja na nyingine ya kuzuia uenezaji wa fedha haramu iliyopitishwa tayari.

Danadana hizi za serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kulinda 'wapiga filimbi' wa habari za ufisadi zinafanywa kimakusudi tu na lengo ni kulinda ?mafisadi' waliojikita katika ngazi za juu za serikali hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: