Siri za ulegelege Serikali ya Kikwete


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

SIRI za ugoigoi na ulegelege wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete zimefichuka. Ni uchu wa urais, ambao umeibua makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Baraza la Mawaziri na Bunge, MwaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema zaidi ya mawaziri 10 wanausaka urais, baadhi yao tayari wameunda makundi ya kampeni, na kujipanga kumrithi Rais Kikwete, anayetarajiwa kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi kwa mujibu wa katiba, Oktoba 2015.

Baadhi yao wameanza kuhujumiana, huku wengine wakiwamo kwenye kundi zaidi ya moja. Wengine wamepima upepo na kuachana na mbio za urais, wakaanza kusaka uwaziri mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya serikali, kuibuka kwa makundi haya ya kutaka urais, miaka minne kabla ya uchaguzi mkuu, kumeanza kumshtua hata rais mwenyewe. Hata hivyo, taarifa zenyewe zinamtaja Rais Kikwete kuwa miongoni mwa vigogo wanaosemekana kuwabeba baadhi ya wagombea kwa ajili ya kinyang’anyiro hicho.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI anasema baadhi ya makundi yameundwa baada ya baadhi yao kuelezwa kwamba rais ana mtu wake anayetaka kumwachia kiti cha urais.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kundi la kwanza ni la waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta. Wanaosemekana kuwa vinara wa kambi yake, ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Hata hivyo, Membe naye ana kundi lake, na anasemekana kuungwa mkono na Nape na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Taarifa za nyongeza zinasema Membe anategemea sana nguvu ya Rais Kikwete, na anamtumia Nape kupima upepo.

Hata Dk. Mwakyembe naye anasemekana kutaka urais, lakini amejificha kwenye “kwapa” la Sitta na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya. Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Dk. Mwakyembe alikuwa mpambe wa Profesa Mwandosya, ambaye pia anasemekana kuendeleza nia yake hiyo kuelekea 2015.

“Wanapokuwa pamoja, miongoni mwa wanaojinadi kumuunga mkono Profesa Mwandosya wamo pia  Kilango, Nape na Dk. Mwakyembe,” anaeleza mmoja wa wafuasi wa karibu wa kundi hilo.

Wengine wanaotajwa ni aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

Ngeleja hajawa na kundi linaloonekana wala kufahamika, lakini taarifa zinasema ameshaanza kukusanya fedha kwa ajili ya mchakato wa kuusaka urais. Nahodha na Mwinyi wanategemea zaidi karata ya Uzanzibari na uhasama wa makundi ya Bara.

Chikawe anasemekana pia yumo katika kundi la Mbunge wa Monduli Edward Lowassa, anayeungwa mkono na swahiba wake wa siku nyingi, Rostam Aziz, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga.

Magufuli hajajenga kundi linalofahamika ndani ya chama, “anakwenda kivyake vyake.” Hata hivyo, wapo baadhi ya watu, nje ya serikali, wanaomtangaza mithili ya watu waliopewa jukumu maalumu.

Habari zinasema miongoni mwa wote, makundi yanayoonekana kuwa na nguvu kubwa ni ya Membe, Mwandosya na Lowassa.

Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali alizungumza na MwanaHALISI kwa sharti la kutotajwa jina lake, akisema vita hii ya urais sasa imeingia katika biashara ya mafuta, ambako baadhi yao wanatuhumiwa kuchochea mgomo wa wafanyabiashara wakubwa wa mafuta kwa maslahi binafsi na kuchukua fedha kwa ajili ya mkakati wa kuelekea Ikulu.

Taarifa zinasema baadhi ya washindani hawa wameanza kufanyiana hujuma na kudhoofishana. Mmoja wa wahanga wa karibu wanaotajwa, ni Profesa Mwandosya anayedaiwa kupangiwa mkakati wa kuhujumiwa na baadhi ya mawaziri wenzake, wakimtuhumu kuwa ameshindwa kusimamia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Kwa sasa, Profesa Mwandosya yuko nchini India kimatibabu.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa katika kutekeleza mkakati huo, Ngeleja yuko mbioni kuvunja EWURA kwa kile kinachodaiwa kuwa kumwondoa Haruna Masebu, mkurugenzi Mkuu wa EWURA anayesemekana kuwa ni “mtu wa Profesa Mwandosya.” Hata hivyo, aliyemteua Masebu kushika nafasi hiyo ni Lowassa alipokuwa waziri wa maji.

Tayari Masebu ameshaitwa na kuhojiwa katika Baraza la Mawaziri kilichofanyika Dodoma siku chache zilizopita.

Habari zinasema Ngeleja anataka kuunda mamlaka mpya itakayokuwa inadhibitiwa moja kwa moja na wizara yake.

Mnyukano huu wa mafuta umemwingiza Masebu kwenye mgogoro na wizara kiasi cha Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA kulazimika kuandika barua kujieleza kwa waziri juu ya hatua zilizochukuliwa na menejimenti ya EWURA katika kupunguza bei ya mafuta na kukabiliana na mgomo wa makampuni ya mafuta.

MwanaHALISI limeona barua hiyo iliyoandikwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA, Simon F. Sayore; ya 19 Agosti 2011, kwenda kwa Ngeleja, aliyepo 754/33 Mtaa wa Samora, Dar es Salaam.

Barua hiyo yenye kumbukumbu EWURA/40/2/VOL. V/348, ikibeba kichwa cha maneno, “Maoni ya bodi kuhusu mabadiliko ya bei ya mafuta ya tarehe 15 agosti 2011,” ililenga kujibu maagizo ya Ngeleja aliyotoa 18 Agosti 2011 wakati alipokutana na bodi ya EWURA katika ukumbi wa mikutano wa wizara ya nishati na madini.

Sayore anasema menejementi ya EWURA haina mamlaka hata chembe ya kutoa bei ya mafuta. Anasema, “…kipengele muhimu cha kanuni ya kukokotoa bei za mafuta ni kile kinachoitaka EWURA kutangaza bei mpya kila baada ya siku 14 (wiki mbili).”

Inasema, “Tangu Januari 2009, menejimenti imekuwa ikikokotoa bei kwa kutumia kanuni hiyo na kutangaza bei katika vipindi vya wiki mbili mbili bila kulazimika kuomba idhini ya bodi. Kisheria, bodi ya EWURA inaamini kuwa mabadiliko ya bei yaliyofanyika tarehe 15 Agosti 2011, yalikuwa halali na yalifuata taratibu zilizopo.”

Akizungumzia mgomo ulioitishwa na wafanyabiashara wakubwa wa mafuta, 3 hadi 8 Agosti 2011, Sayore anasema “katika nchi inayofuata utawala wa sheria, mgomo huo haukuwa halali.”

Hata hivyo, Sayore anasema mgomo umewapa changamoto mpya ya kuingizwa kipengele kipya cha “stocks” za mafuta wakati wa kutangaza bei mpya ya mafuta; hakuna uzembe wowote uliotokea kwa kushindwa kuingiza kipengele hicho.

Barua ya Sayore imenakiliwa pia kwa waziri wa Maji, katibu mkuu wa wizara ya maji na kaimu katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini.

Ngeleja alipoulizwa na gazeti hili kuhusu barua hiyo, alisema hajaiona, hivyo hana la kujibu. Lakini
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alithibitisha kupokea barua hiyo.

Hata hivyo, Maswi aligoma kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba yeye bado ni mgeni katika wizara hiyo.

“Kama ni masuala yanayohusu bei ya mafuta na mgomo wa wafanyabiashara wa mafuta, tafadhali niache. Hilo jambo, nakuomba waulize wizara ya maji. Mimi nimeingia juzi katika wizara hii, bado ni mgeni. Sifahamu lolote juu ya hilo unalotaka kuniuliza,” alisema.

Alipoulizwa katibu mkuu wa wizara ya maji na umwagiliaji, Injinia Cristopher Sayi juzi Jumatatu kama wizara yake imepata barua hiyo alisema, “niko Dodoma kwenye mkutano wa Bunge la bajeti. Inawezekana barua imefika ofisini Dar es Salaam. Nakuomba tuwasiliane baada ya kurejea jijini.”

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: