Siri za Zitto nje


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Mawasiliano yake yanaswa
Aponzwa na mwandishi wa habari
Zitto Kabwe

SIRI kubwa kuhusu mwenendo wa Zitto Kabwe (Mb) ndani ya chama chake zimeanikwa mitaani na zinaweza kumzamisha kisiasa, MwanaHALISI sasa linaweza kuripoti.

Siku nne baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Willibrod Slaa kusema wamenasa taarifa za mawasiliano ya Zitto, baadhi ya taarifa zimepatikana jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Zitto ananukuliwa akiapa kusaidia wagombea uongozi katika vyama vingine; na katika moja ya taarifa ananukuliwa akisema atasaidia David Kafulila kupata ubunge “hata kabla ya akina John Mnyika…”

Mnyika ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA na Kafulila alikuwa Afisa Habari ambaye baada ya kuondolewa wadhifa huo amekimbilia NCCR-Mageuzi. Mnyika anatarajia kugombea ubunge jimbo la Ubungo.

Naye Zitto amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la Jumatatu akilalamika kuwa ameingiliwa katika mawasiliano yake ya baruapepe (e-mail); jambo ambalo Mkurugenzi wa Upelelezi, Robert Manumba, amedakia haraka na kusema Zitto akiwapelekea malalamiko watashughulikia.

Kwa mujibu wa mpangilio wa taarifa husika, lazima aliyezitoa amepata ufunguo wa baruapepe (password) wa ama Zitto au mwandishi wa habari wa Mwananchi, Denis Msacky.

Karibu mawasiliano yote ni kati ya Zitto na Msacky juu ya “ushujaa” wa Zitto na jinsi anavyopendwa nje ya chama huku “akichukiwa” na viongozi wake wakuu.

Katika moja ya mawasiliano, inaonyeshwa kuwa  Msacky alimwandikia Zitto akieleza, “Leo hii Mrema (Augustine Lyatonga) anasema anakuheshimu wewe, lakini si Mbowe; hivyo hivyo, Lipumba (Profesa Ibrahim) na James Mbatia wanasema wewe una visheni.”

Katika mawasiliano hayo ya Jumanne, 1 Desemba 2009, saa 6.45 adhuhuri, Msacky anaonyeshwa kumwambia Zitto pia kuwa, “CCM nao…wanakusifu kwamba pamoja na kwamba unawaliza sana, lakini ni kiongozi shupavu.”

“Leo hii siasa za CHADEMA zingekuwa zinatisha kama ungekuwa mwenyekiti wa CHADEMA, vijana nchi nzima wangejiunga na chama, uko nao karibu, unaongea nao, una elimu nzuri, unajua mambo, unasoma sana,” imeeleza sehemu ya mawasiliano kutoka kwa Msacky kwenda kwa Zitto.

Kinacholeta wasiwasi ndani ya CHADEMA kinaweza kuwa lugha inayotumiwa katika mawasiliano hayo. Kwa mfano, katika waraka huohuo, Msacky ananukuliwa akiandika:

“Wanataka kukumaliza, nami sitakubali mtu ammalize rafiki yangu nikiangalia…wanasema Mbowe hata Mbatia akikaa vema anaweza kumpita kama siasa za kufukuza zitaendelea. Muhimu, usisikilize watu, tulia, urudi tupange tufanye nini? Lakini ukweli ni kwamba sasa wanakuogopa…Mwenyekiti Mtarajiwa…”

Mawasiliano yanaonyesha kuwa Zitto hakufurahishwa sana na taarifa za Mwananchi kuwa amemsaidia Kafulila magari matatu kwenda Kigoma kufanya kampeni chini ya NCCR-Mageuzi, lakini Msacky anaonyesha kumfariji.

“Kaka, mimi nimeiona story, haina matatizo zaidi ya kuwafanya akina Mbowe kusitisha mpango mbaya dhidi yako maana wanaanza kuogopa. Hata Mrema Lyatonga amesema kwamba Zitto huwa unamsaidia akiwa na shida. This shows that ur a leader katika opposition, wewe ni mtu wa maridhiano, unakuza upinzani Kigoma,” anaeleza.

Anasema, “Leo nasikia akina Mnyika wanahaha sana, waambie familia yako wasiingie katika mtego wa kuanza kuhojiwa na akina Kubenea (Saed wa MwanaHALISI), watawachanganya. Wewe usiongee kitu chochote, wabaki wanahaha, lakini for sure you are safe, na hizo kampeni za Mnyika kukuchafua huku akitaja majina ya Kafulila, ataziacha.”

Akionyesha juhudi za kushawishi, kuliwaza au kufarakanisha, Msacky anaandika, “Katika hili Zitto, mimi niko na wewe, huna kosa ambalo umefanya, na wala usihofu maana wewe utakuwa nguzo ya upinzani Tanzania…Wanakupa majina ya ajabu, wanakuita Mr Dowans, wanatumia akina Halima Mdee kukuchafua katika magazeti…”

Awali Zitto alikuwa amemwandikia Msacky akisema, “Stori niliyoiona kwenye mwananchi itaniletea matatizo sana.” Hiyo ilikuwa Jumatatu 30 Novemba 2009, saa 5.21 asubuhi. Baruapepe hiyo ilikuwa na kichwa kisemacho: “Muhimu na haraka.”

Aidha, katika mawasiliano mengine, Zitto anaendelea kuonyesha kutofurahishwa na taarifa juu ya magari matatu kwa safari ya Kafulila.

Naye anaandika kwa Msacky, “tatizo la stori ni wingi wa magari, itaonekana mimi nina magari mengi na ni fisadi unajua? Hilo ndio tatizo.”

Saini ya Zitto inatofautiana katika baadhi ya baruapepe. Pengine anaandika “zitto” na kwingine anaandika “Zi.”

Moja ya mawasiliano ambayo yanazua mashaka yanaonyesha Zitto akikiri kuwa na mawasiliano na waasi nchini Kongo akiandika, “take it from me (niamini), nina contacts nyingi sana Congo na hao rebels (waasi) huwa wananiomba sana ushauri na kutaka kuwaunganisha.”

Katika moja ya mawasiliano, Msacky anamwonya Zitto kutotumia baruapepe ya “CHADEMA kwa mawasiliano ya siri” na kutaka amwambie mama yake Shida Salum akatae kuongea na waandishi wa habari. “…nasikia Mbowe anataka mama awe akiongea na waandishi, usikubali,” alieleza.

Zitto alipoulizwa kuhusu taarifa ya Mwananchi kuwa anatembea na barua mfukoni ya kujiuzulu uanachama CHADEMA, alisema “Sina la kusema.”

Alipong’ang’anizwa kwamba imekuwaje hawezi kuzungumzia suala hilo ambalo ni muhimu kwa mustakabali wake wa kisiasa kwa chama chake, Zitto alisema, “Ni kwa sababu sitaki kuingia katika malumbano na katibu mkuu wangu (Dk. Willibrod Slaa) kwani malumbano hayo hayataijenga CHADEMA.”

Alipotakiwa kueleza juu ya baruapepe ambazo zinadaiwa kuwa mawasiliano kati yake na Msacky, haraka alijibu, “Sina la kusema.”

Alipoelezwa umuhimu wa yeye kueleza msimamo wake juu ya baruapepe hizo, Zitto alijibu, “Chochote nitakachosema sasa hivi, kitawachanganya Watanzania.

“Sitaki malumbano. Hakuna sababu ya kuwachanganya Watanzania. Hiyo haina maana yoyote,” alisema Zitto kwa sauti ya ukali. Zitto alikuwa akiongea kutoka Ujerumani kwa simu Na. +4915222493231.

MwanaHALISI ilimtafuta Msacky. Baada ya kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa, hatimaye aliandika ujumbe “Kaka, niko katika kikao. Tuma ujumbe.”

Msacky aliulizwa, “Kaka, tumesikia kwamba umetajwa katika sakata la Zitto na chama chake na kwamba wewe ndiye mtibuaji. Je, ni kweli?” Hakujibu ujumbe na alipopigiwa simu ilikuwa inaita hadi kukatika.

Gazeti lilipowasiliana na Mnyika na kumueleza kwamba amekuwa akitajwa katika ujumbe wa Zitto na Msacky, alikiri kupokea ujumbe huo wa baruapepe uliotoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni “Mtanzania mwema.”

Alisema alipoona ujumbe mmoja unahusu Zitto kushauri Msacky kutochapisha habari za mkutano wake na waandishi wa habari, ndipo aliamua kupeleka ujumbe huo kwa Zitto.

 “Nilimuuliza kuna hiki kitu nimetumiwa. Je, haya ni maandishi yako au kuna mtu ameingilia emaili yako na kujiandikia haya? Hadi leo hii, bado sijapata jibu,” alisema Mnyika kwa sauti ya masikitiko. Alisema yeye hana cha kusema na kuongeza, “labda umuulize Zitto.”

Alipoulizwa anachukuliaje suala hilo, Mnyika alisema, “Ukiniuliza mimi kwa upande wangu, nilitegemea mambo hayo yangemalizwa katika vikao vya chama na si kwa vyombo vya habari. Lakini kwa hatua ya hivi sasa, nadhani Zitto bado anayo fursa ya kulieleza hili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe alipoulizwa juu ya madai ya kuwapo njama za kuhujumu chama chake zinazofanywa na Msacky kwa kumtumia Zitto, haraka alijibu, “tuna utaratibu wetu wa kushungulikia mambo ndani ya CHADEMA.”

Alisema, “Sina la kusema. CHADEMA ina utaratibu wake wa kushughulikia mambo yake.”

Kwa kadri mawasiliano ya Zitto na Msacky yanavyoonyesha na iwapo yatathibitishwa kuwa kweli, jambo ambalo linaanza kuthibitishwa na Zitto kwa kulalamika kuingiliwa kwenye faragha, basi uhusiano wake katika chama utakuwa umepata nyufa.

Wachunguzi wa siasa za upinzani nchini wanasema kwa hali hii, uwezekano wa Zitto kubaki ndani ya chama chake ni mdogo. “Ama atajiondoa mwenyewe au hatimaye atafukuzwa,” ameeleza mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hata hivyo, Zitto amenukuliwa na Mwananchi akisema, “Sitaki kugombana na mtu mimi. Wala msiniweke kwenye kifungo cha siasa. Ni bora niishi huru kuliko katika mateso ya siasa za kipumbavu kabisa. Nitafanya maamuzi ambayo hayajawahi kufikiriwa.”

Wiki iliyopita Kafulila aliwaambia waandishi wa habari kwamba Zitto atafanya maamuzi makubwa ambayo hawakutegemea.

0
Your rating: None Average: 3.2 (18 votes)
Soma zaidi kuhusu: