Sisiem inasubiri maombi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MTU akiugua, hujikokota hadi hospitalini kutafuta tiba. Ikiwa amezidiwa, ndugu na jamaa ndio humchukua na kumpeleka. Huko ugonjwa hushitakiwa na kuadhibiwa na madaktari kwa njia ya vidonge au sindano.

Ikiwa mgonjwa atazidiwa kufikia hatua ya kutema dawa aliyopewa, huku akitapika na ‘kuendesha,’ madaktari huamua kumtundikia dripu, huku uji akipewa kwa kutumia mrija unaopitishwa puani.

Madaktari huweza kumzungushia mgonjwa kitambaa au humweka chumba maalum kwa uangalizi wa karibu. Madaktari na manesi watatoka na kuwatoa hofu ndugu wa mgonjwa kuwa mgonjwa atapata nafuu maana dawa waliyompa hufanya kazi taratibu.

Hakuna daktari hata mmoja mwenye ujasiri wa kusema mgonjwa atakufa. Haitakiwi kuwajengea hofu ndugu. Hiyo itasababisha zogo hospitalini. Hata akifa, watasingizia “mmemchelewesha ” na wachache wanaouona ukweli na hasa kama mgonjwa amefikia hatua ya kutotibika hospitalini, husema “jaribuni mitishamba” au kama ni ugonjwa wa kisasa watasema “mpelekeni kwenye maombi”.

Madaktari wa aina hii, ndio mwaka jana walisababisha mamia kwa mamia ya watu kutorosha wagonjwa wao hospitalini na kukomba vibubu vyao ili kuwapeleka wapendwa wao Loliondo kwa mchungaji aliyegeuka mganga wa kienyeji. Wakafia huko au wakafa baadaye kutokana na kutekeleza dawa.

Lakini iwe hospitalini au kwa Babu wa Loliondo, mgonjwa akifikia hatua ya kutotambua nani ameingia au kutoka kumkagua, ndugu na jamaa wanapaswa kuwa watulivu, wazungumze lugha moja, wakaze moyo kwani huwa hatua ya mgonjwa kuwafia mikononi.

Hivi hamjawahi kuona mgonjwa anakwenda hospitali akionekana ana nguvu, lakini huzidiwa hapo na kufa? Mwalimu si alikwenda Uingereza akitembea na mtu mwenye nguvu? Tena, ukiona mgonjwa anazungumza sana kuliko hata kawaida, hizo ni dalili za mgonjwa kukaribia mauti.

Inadaiwa pia ndugu wakianza kusutana, kulumbana, kulalamika mbona mnaniachia mgonjwa peke yangu au hata kudai ndugu wengine hawampendi mgonjwa eti huwa nuksi. Wote mnauguza kwanini muanze kudai eti yule yuko vile, ooh mgonjwa akifa sijui mjomba atakuwa umesababisha? Ni dalili mbaya.

Wasikilize jamaa hawa wanavyolumbana hospitalini juu ya mgonjwa wao Sisiem. Mshauri mmoja kutoka Kenya, aitwaye Daniel arap Moi alipokuja kuaga mjini Dodoma – sijui alizungumza na  Bonge wa Jamhuri au NEKI – aliwaasa kwa Kimombo “Donti yu eva bi divaided” yaani kipindi hiki cha mageuzi ninyi Sisiem ni kama mko hospitalini mnauguza mgonjwa, msithubutu kufarakana. Wakashangilia.

Kabla hajaondoka aliulizwa, vipi hali ya nyumbani kwako? Jamaa yule aliyeitwa profesa wa siasa akajibu kwake hawamuwezi. Waswahili wanasema usitukane mamba wakati hujavuka mto. Chama alichokuwa anaongoza ‘kikafia’ hospitalini na mpaka sasa kinanuka si Kanu.

Aliokuwa anawashauri wamelazwa mara mbili 2005 na 2010 wakapona lakini sasa wananyoosheana vidole.

Mgonjwa Sisiem akapewa dawa ya kutimua walarushwa lakini akatema; akapewa dawa mjarabu ya kuvua magamba mgonjwa ametema. Ndugu, jamaa na vijana ambao wanaogopa kufiwa na Mzee wa kaya wameanza kukimbia boma.

Maelfu kwa maelfu wanakimbia boma na kwenda kwingineko. Karibu wote wanademadema kituo cha Chechemea kuanza maisha mapya. Huko wanasikilizia msiba wa Sisiem kutangazwa wakati wowote maana mgonjwa hajui wanaotoka wala wanaoingia. Inasubiri maombi maalum.

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: