Sisiem wamenasa penyewe


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KATIKA miaka ya 1980 lilikuwepo basi lililobatizwa jina la Navalonge Swela, ambalo lilikuwa linafanya safari zake kati ya Njombe na Dar es Salaam.

Nasikia, mmiliki wake alikuwa haambiliki; alijenga tabia ya kupuuza malalamiko, “Hata Wakisema Sijali”.

Navalonge Swela lilikuwa linatimua mbio na kuyapita hata mabasi yaliyoondoka saa moja kabla. Tofauti na wazee, wafanyabiashara vijana walikuwa wanapenda sana kusafiri nalo.

Madereva walikuwa kama vichaa maana walikuwa wanaweza kuovateki upande wowote bila kujali usalama barabarani na kuacha abiria wameshika “roho” zao.

Madereva wa Mjengoni Dodoma, Spika Anne Makinda na wasaidizi wake, nao wanasema navalonge swela kwamba hawatajali malalamiko ya upinzani kukandamizwa.

Makinda amefikia hatua hata kumzuia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujibu maswali mazito. Tundu Lissu alimuuliza Pinda swali la kizushi, kwamba kama ameshughulikia mgogoro wa madaktari lakini ameshindwa, kwanini asijiuzulu?

Ghafla Makinda akabwatuka, “Usijibu hilo!” Kama muishiwa Spika ameamua kuwa kituko, wabunge wa Sisiem si wamepewa leseni!

Hebu jiulize kichaa amelazwa katika hospitali ya vichaa ya Mirembe, halafu anadai ni daktari wa vichaa, huyo amepona au bado?

Mtunza fedha wa Sisiem, ambaye ni bingwa wa kejeli na hasira, akasema Mjengoni M4C wakapimwe kabla ya kuingia bungeni eti vichaa. Sisiem wote, hata Mwenyekiti wa kikao, Sylvester Mabumba wakafurahi kwa saaaana.

Kubwabwaja ni mradi wa bwana huyu, kwani aliwahi kupiga chemba kila kitu halafu waishiwa wenzake wakamchangia nyekundu nyekundu tupu.

Akasimama muishiwa aliyepewa cheo cha kepteni kwa kuimba nyimbo za Sisiem alipokuwa jeshini; akakimbia hoja ya uchumi akatoa vitisho.

“Tukizichapa humu mtakufa. Nasema wala msithubutu tupigane humu ndani, sisi ni wengi kuliko ninyi,” alisema kwa sauti ya kukwaruza tofauti na akiimba.

Mabumba yakamtoka maneno, “…usitafute umaarufu hapa” akimzodoa Lissu kisha akamgeukia John Mnyika na kumwambia “unawashwawashwa nini?”

Kwa Sisiem lugha hii si maudhi. Wamelazwa Mirembe na kujidai ni madaktari wa vichaa.

Hata Makinda ameshindwa kutoa uamuzi juu ya lugha hiyo eti navalonge swela. Sisiem wanapenda kutukana, lakini wakitukanwa wao utasikia “Muishiwa Spika mwongozo…”

Akaja mama wa Mkoa wa Rukwa, muishiwa Injinia Stella Manyanya. Akaanza kwa kusema, “mimi ni msomi.” Nikajiuliza, kuna mtu aliyehoji usomi wake? Hivi hajui ‘kwetu’ Kagera na akajangu kange kashomile,  hata paka wangu amesoma?

Aliposema “ashakumu si matusi nitakayosema najua yatawaudhi wengine” nilifumba masikio nisione, sore, nisikie. Akasema, “Nashukuru Mungu amemwepusha Dk. Steven Ulimboka asiue kama Hitler!”

Wasomi hufanya utafiti, lakini huyu amebeba vijineno vya propaganda kutoka vijiwe vya Sisiem kwa lengo la kuinasua iliponasa serikali. Hivi atakuwa na tofauti gani na wasiosoma katika hili?

Majimarefu akaingia kichwakichwa. Akadai anashukuru Dk. Ulimboka naye ameonja kipigo.

Halohaloo! Sisiem wanalo. Vitisho walivyopewa TUCTA mwaka 2010 kwamba wataenda kwenye meza ya mazungumzo wakiwa na bandeji, yametimia kwa Dk. Ulimboka.

Ndiyo maana, wapinzani wakiomba mgomo ujadiliwe, Makinda anakataa. Wakiomba iundwe kamati huru ya Bunge, Makinda anakataa. Wapinzani wakizungumzia kutekwa kwa Dk. Ulimboka, waishiwa Sisiem wananuna, Spika anazuia. Sisiem wakiwazushia wapinzani, Makinda roho kwaaatu.

Huu ni ushahidi Sisiem wanajua watekaji na watesaji wa Dk. Ulimboka.

Navalonge swela; upepo huu haupiti, tutaendelea kudai Tume Huru ya kuchunguza ukatili huu dhidi ya Dk. Ulimboka hadi kieleweke.

0658 383 979
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: