Sitta ‘kanyea kambi’


editor's picture

Na editor - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SAMWEL Sitta ametuhumu gazeti hili, kuwa linatumiwa na watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini ili “kumchafua” yeye na wenzake.

Alikuwa akiongea kwenye kipindi cha “Dakika 45” juzi Jumatatu, kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Sitta alionekana na kusikika akisema, gazeti hili lilikuwa madhubuti na imara; lakini sasa limeanza kuyumba kutokana na hatua yake ya kushambulia wale wanaopigana na ufisadi nchini, hasa yeye.

Alikwenda mbali hata kutuhumu mtendaji mkuu wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) na mchapishaji wa MwanaHALISI, Saed Kubenea, kuwa amenunuliwa na mafisadi.

Waziri huyu wa Afrika Mashariki anajua fika kwamba gazeti la MwanaHALISI, wamiliki wake, waandishi wake, hawana mkataba naye wa kumwandika anayotaka.

Sisi tuko kazini. Tunaangalia wale tunaowatumikia; nao ni umma wa Tanzania na jamii pana. Siyo Samwel John Sitta wa Urambo, kibarua katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Si gazeti, kiongozi wake wala mwandishi wa MwanaHALISI, aliye na mkataba wa kumwandika Sitta kama anavyotaka. Tuna kanuni ya kuandika yeyote na chochote kama alivyo au kilivyo na siyo kwa upendeleo.

Kama Sitta aliwahi kuandikwa vizuri ajue; na labda akumbuke kuwa, hakuwa ametoa chochote, ameahidi chochote au amefurahisha gazeti kwa lolote lile; bali kwa kuwa alikuwa kwenye mstari wa ukweli na haki.

Pale atakapotoka kwenye mstari; akajiingiza kwenye fikra, kauli na matendo ambayo tunaona na kuamini kuwa siyo sahihi; yanayokinzana na ukweli na haki kwa jamii tuliyomo; tutamwonyesha kwa jamii kama alivyo – bila woga wala upendeleo.

Nani amemtuma Sitta kushiriki vita dhidi ya MwanaHALISI? Nani atamwamini kwa kauli zake ambazo hawezi kuthibitisha? Je, kwamba gazeti limeandika asichopenda au ambacho hapendi wengi wajue juu yake, huko ndiko kushirikiana na mafisadi?

Siyo sahihi kutumia “ufisadi” kujenga urafiki au uadui. Fisadi na hata wanaowashabikia, watafahamika, hasa kwa matendo yao na mapema, kwa kauli zao. Lakini kwa Sitta kujaribu kukimbia kivuli chake, na kutafuta kuegemeza woga wake kwa MwanaHALISI; hakika ni woga uliopitiliza kwa mtu wa umri, elimu, uzoefu kazini na nafasi aliyonayo serikalini.

Hata hivyo, Sitta siyo mwanzilishi wa “mapambano dhidi ya mafisadi” nchini. Hata kwa hatua ya Bunge kuchunguza mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond wakati yeye akiwa spika, hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuona ufahari na kujitwisha ushujaa.

Bunge lilikuwa linafanya mwitikio tu wa mfululizo wa ripoti za vyombo vya habari jasiri ambavyo vilikuwa vikiandika, bila kukoma, ufisadi uliokuwa umefanywa nchini. Richmond ni “cha mtoto” kwa ufisadi mkuu ambao bunge lake halikushughulikia na bado liko kimya juu yake.

Aidha, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichoanika orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi hapo 15 Septemba 2007 kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam; wakati viongozi wa Sitta – katika chama chake na serikali wakidai kuwa “huo ni uzushi mtupu.”

Ukweli ni huu: Walioanikwa ni viongozi wakuu wa nchi wa sasa na waliopita ambao wamekuwa waajiri wa Samwel John Sitta. Bado ni waajiri wake. Hawezi kujitenga nao. Hawezi hata kuwaambia uso kwa uso kwa ukali wa mkweli na mhalifu. Anarukia MwanaHALISI!

Gazeti hili lina rekodi ya kuwa pekee lililoripoti kwa kina na ufasaha tuhuma ya kila mmoja miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi. Mara baada ya kuchapisha taarifa za watuhumiwa na picha zao, baadhi walitishia kwenda mahakamani; lakini tulisimama imara hadi wakayeyuka.

Hata kinachoitwa “ujasiri wa wapinga ufisadi” ndani na nje ya bunge, kilitokana na mfululizo wa uibuaji uoza serikalini. Uibuaji huo ulifanywa na baadhi ya vyombo vya habari; gazeti hili likiwemo au likiongoza.

Bali tukubali kuwa Sitta ana matatizo na wenzake. Ni muhimu amalizane nao vizuri au vyovyote vile bila kujenga viinimacho. Kwa mfano, Sitta anataka kujinasua kutoka kwenye tuhuma za usaliti wa chama chake kwa kile kinachoitwa “kuanzisha chama ndani ya chama.”

Anatuhumiwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Jamii (CCJ) wakati bado ana nafasi ya juu katika uongozi wa serikali ya chama kilichoko madarakani. Hakika hili siyo tatizo la MwanaHALISI; hata pale gazeti litakapokuwa limeandika taarifa zake kwa kunukuu vyanzo ambavyo siyo rahisi kuvikanusha.

Hapa, badala ya kutuhumu gazeti letu, ni vema akajibu madai ya “washirika wake,” hasa Fred Mpendazoe, anayelalamika kuwa Sitta alimtosa. Mpendazoe ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Kishapu (CCM), anasema aliamua kuacha ubunge ili kuimarisha CCJ, wakati wakisubiri “Sitta na wenzake.”

Gazeti halihusiki na chochote walichoahidiana wakati huo. Halijapata ushahidi kama walidhulumiana. Halijapokea taarifa iwapo kuna ambao hawakupata mgawo wa fedha zilizochangwa na wahisani wa ndani au nje kwa ajili ya kazi ya akina Sitta na Mpendazoe. 
Tunachojua na tulichochapisha ni juu ya ujio wa CCJ, nani alikusanya fedha na kutoka kwa nani; nani alilipia kodi ya pango ya ofisi, nani alilipa mishahara ya watumishi wa mwanzo na nani alilalamika, kwamba “wenzangu wameniacha njiapanda.”

Hadi sasa waanzilishi watatu wamesema kile wanachodai wanaelewa vema na hata kwa kiapo. Hao ni Mpendazoe, Dickson Ng’hily na Daniel ole Porokwa. Katika hili, na hasa kama Sitta anadhani tunalikuza kwa kuliandika, alaumu wenzake na siyo chombo cha habari wala wanaokimiliki.

Jingine ambalo tunahisi linaweza kuwa limemfanya Sitta aanze kushambulia MwanaHALISI, ni  pale gazeti lilipomtuhumu hujuma kwa kufunga mjadala wa kashfa ya Richmond. Wakati huo alikuwa spika. Hapa tulisema bayana kwamba hatukubaliani naye. Hata sasa hatukubaliani naye.

Ni kunyenyekea kwake kwa serikali au kutafuta “mwafaka” wa haraka kwa maslahi binafsi ambako kulimfanya azime mjadala muhimu kwa taifa. Bado tunapinga hili. Tunalipinga kwa kuwa linaathiri vibaya hata kauli zake za sasa za kutaka kampuni ya kufua umeme ya Dowans isilipwe zionekana kama mzaha.

Kama kwa msimamo wetu huo anaona ndio tunashirikiana na mafisadi kumchafua, basi amefikia ukingoni. Sharti arudi nyuma au abomoe ngome ya kiza kilichomfunika macho na akili.

Na nani amempa Sitta madaraka ya kuamua kuwa hiki ndiyo ufisadi na kile siyo ufisadi? Kama angekuwa mkweli na safi, asingekuwa anatumikia ambao tayari wamethibitika kuwa mafisadi – kwa kauli, vitendo na kisheria.

Gazeti hili haliwajibiki kuomba ruhusa kwa Sitta ili lirekodi kuyumba au kupotoka na hata kutetereka kwake. Tuna haki ya kuona, kuchambua, kutolea maoni na hata kuchapisha kile tunachoona na kusadiki juu yake na juu ya yeyote na chochote kile.

Atakayejaribu kutunyang’anya haki na uhuru wetu huo, kwa kutuita washirika wa “mafisadi,” tutampinga. Tutaomba wadau wa habari kumpinga. Lakini pia tutamwita fisadi mkuu anayejaribu kutunyang’anya haki ya kufikiri, kuandika ukweli na kutoa kauli.

Sitta ananyea kambi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: