Sitta afanywa kondoo wa kafara


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version
SPIKA wa Bunge, Samwel Sitta

SPIKA wa Bunge, Samwel Sitta ameshikiwa bango na wapinzani wake wa kisiasa wakishinikiza afukuzwe katika chama kutokana na msimamo wake wa "kujenga Bunge lenye kasi viwango."

Taarifa kutoka ndani ya vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mijini Dodoma, zinasema baadhi ya wajumbe walishinikiza Sitta aachie ngazi kwa madai kwamba amekuwa akitumia Bunge kama silaha ya kupambana na wenzake katika chama na serikali.

Kikubwa ambacho kimemjengea Sitta maandui ni ujasiri wake katika kusimamia suala la kashfa ya Richmond. Kingine kinachohusishwa ni maamuzi yake kuhusu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba katika malalamiko yake dhidi ya mbunge wa CHADEMA, Halima Mdee.

Hata hivyo, ukichunguza kwa makini mwenendo wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, haraka utabaini kuwa Sitta ndiye mtetezi mkuu wa serikali. Anaweza kunyongwa na wana-CCM kwa kuwa siyo wepesi wa kung'amua.

Spika hauyuko bungeni peke yake. Pamoja na kuwepo wabunge wengi wa CCM ambacho ni chama chake, kuna Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Kikao cha Bunge cha CCM na kamati za kisekta.

Spika hana uwezo wa kuzima hoja za vikao na wawakilishi hawa wa serikali na CCM. Kwa mfano, spika hana ugomvi na waziri mkuu au mwanasheria mkuu wa serikali. Wala hajagongana na Kamati ya Uongozi ya Bunge yenye wawakilishi wa vyama vyote bungeni.

Anachofanya spika Sitta ni kutoa fursa sawa kwa mawazo kutoka kwa wabunge na wawakilishi wa serikali na kuongoza hadi muwafaka.

Mfano hai ni hatua ya serikali kuondoa muswada wake wa sheria ya uchimbaji wa madini katika mbuga za wanyama. Wabunge walijadili chini ya uongozi wa spika hadi serikali ikapata kuelewa na kuafiki hoja za wabunge na kuondoa muswada wake.

Hapa huwezi kusema spika ameongoza bunge kuasi. Kwa nia njema kabisa unaweza kusema ameongoza kikao kutoa maoni mazuri ambayo serikali imekubali na kufanya mabadiliko katika maamuzi.

Angalia suala lingine. Ni lile la kufuta misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini. Bunge, chini ya Sitta liliona hapo serikali inaangamia. Likasimama kuhakikisha kwamba hayo hayatendeki.

Katika hili serikali haikushawishiwa wala kushinikizwa na Sitta. Wabunge, wakiwemo waziri mkuu na mwanasheria mkuu wa serikali, walikubaliana juu ya suala hilo na ikabidi serikali ikubaliane nao. Hapa hakuna ushawishi wala shinikizo la spika. Katika mazingira hayo, serikali ilipaswa kumshukuru Sitta.

Aidha, kwa mujibu wa kanuni za bunge, ili suala lolote lifikishwe bungeni, sharti lipitie kwenye kamati ya kisekta. Spika si mjumbe wa kamati za kisekta, bali ni mwenyekiti wa Kamati ya uongozi.

Lakini kubwa zaidi, hakuna jambo lolote ambalo linaweza kuingizwa bungeni bila kufikishwa kwanza kwa Kamati ya uongozi ya Bunge. Ndani ya kamati ya uongozi, serikali inawakilishwa na wajumbe watatu; waziri mkuu, mwanasheria mkuu wa serikali na waziri anayeshughulikia Bunge.

Wajumbe wengine wa kamati ya uongozi, ni wajumbe wote wa kamati za kudumu za Bunge na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni. Katika mfumo wa sasa wa Bunge, wengi wa wajumbe hawa wanatokana na CCM.

Ni wajibu wa serikali pale inapoona kuwapo kwa mapungufu ya jambo lolote, kuomba kwa kamati ya uongozi au kamati ya sekta kutowasilishwa suala hilo bungeni hadi hapo itakaporekebisha mapungufu yaliyopo.

Hivyo ndivyo inavyotendeka katika mambo yote, vinginevyo kuwe na hoja maalum ya mbunge. Lakini hata hilo la hoja maalum kwa utaratibu wa sasa, hakuna mbunge anayeruhusiwa kuwasilisha hoja binafsi bungeni, kabla ya hoja hiyo kupitia kwenye vikao vya chama chake.

Chukua mfano wa kashfa ya Richmond. Kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa, kamati ya uongozi ya Bunge ilipitia kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM. Kamati hii ilikuwa chini ya waziri mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa. Pale kamati ilipojiridhisha, ilipeleka suala hilo kwa kamati ya uongozi ya Bunge.

Hata Lowassa ambaye amekuwa mwathirika wa uchunguzi wa Richmond, hajasema na hatarajiwi kusema kwamba hakukubaliana na kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza Richmond.

Ndiyo maana mpaka sasa, ameshindwa kusema kwamba haya yote yalifanyika bila kufuata taratibu. Hajasema kuwa Richmond lilibebwa na Sitta mwenyewe bila kupitia kwa kamati hii ya sekta au kamati ya uongozi au katika kamati za CCM.

Kama Sitta angekuwa amepitisha jambo hili kienyeji, angalau wapinzani wake wa sasa, wangekuwa na hoja.

Lakini kinachofanyika hapa, ni ubabe na mbinu za kulazimisha mambo. Lakini si hivyo tu, bali hizi ni jitihada za wale wasiokubali uongozi wake katika Bunge kwa sababu ya maslahi binafasi.

Wengine wanaweza kusema ni kujaribu kile mwenyewe alichoita, "kuzorotesha jitihada zake za kuligeuza Bunge kuwa chombo imara, badala ya Bunge poa."

Hata katika kesi ya Makamba hali ni hiyohiyo. Ni Makamba mwenyewe aliyepeleka mashitaka yake kwa spika na yeye ndiye aliyekimbia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kisha akajitoa katika shauri ambalo tayari lilianza kusikilizwa.

Sasa katika mazingira hayo, nani ameaibisha CCM? Sitta au Makamba? Tatizo hapa si Sitta, bali ni serikali kushindwa kutenda kazi zake ipasavyo. Hata pale inapobaini watendaji wake wametenda kinyume na taratibu, serikali imeshindwa kuchukulia hatua kwa watendaji hao.

Katika hali hii, Sitta ameonyesha ujasiri na uzalendo. Angalau amejitoa kusaidia kurekebisha mambo kutokana na hatua yake ya kuruhusu serikali ikosolewe na ishauriwe.

Hata kama njama za kumng'oa zitafanikiwa, iwe leo au kesho, tayari Sitta atakuwa amejijengea heshima kwa umma. Kwamba amefanikiwa kujenga bunge imara.

Hatua yeyote ya sasa ya kumdhibiti Sitta, inazidi kuangamiza Kikwete, serikali na hata chama chake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: