Sitta alivyogeuka 'jiwe la chumvi'


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 10 March 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta

SABABU za Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kuamuru bunge kufunga mjadala wa Richmond ni nyingi. Hata hivyo, ni sababu tatu zilizomfanya ageuke mbongo na kufunga mjadala. Hadi sasa, zaidi ya miezi miwili, Sitta hajasema kwa dhati kile kilichomfanya kugeuka mbogo.

Badala yake, anasema ameamua kufunga kwa kuwa “serikali imetekeleza maazimo 21 kati ya 23 yaliyotolewa na bunge.” Hili ndilo alilosema ndani ya bunge.

Nje ya Bunge, Sitta amenukuliwa tofauti. Amesema uamuzi wake wa kufunga mjadala kabla ya maji kuchemka, umetokana na “tishio la kuvuliwa uanachama.” Je, ukweli ni upi?

Sababu ya kwanza ya Sitta kuzibwa mdomo na ambayo hajaisema wazi, ni tuhuma za matumizi mabaya ya fedha yaliyokabili ofisi yake.

Kwamba ofisi ya Spika Sitta ilituhumiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo kutumia mabilioni ya shingi na kushindwa kurejesha masurufu ya safari za spika serikalini.

Cheyo alikuwa akinakiri taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu wa Serikali (CAG) ambaye kwa mara tatu mfululizo ametoa hati chafu kwa bunge kwa kushindwa kuweka vizuri kumbukumbu za hesabu za umma.

Hapa ndipo Sitta alipoanza kunywea; alipoacha kuendelea kung’ang’ana na zimwi la Richmond, akihisi ukaidi ungeweza kuibua mengi.

Hata Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah, ambaye bunge lilimtuhumu na kumtaka kuachia ngazi, angeweza kumchomoa huko aliko na kutangaza kuchunguza ofisi ya spika na hata Sitta mwenyewe.

Katika mazingira haya, Sitta aliona njia pekee ya kujiepusha na “kikombe hicho” ni kujisalimisha kwa kufunga mjadala.

Pili, Sitta aliamua kufunga mjadala baada ya kuona dalili za chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kutompitisha kuwania ubunge katika uchaguzi ujao.

Kwa kuwa naye hana tofauti sana na wanasiasa wengine wa CCM – wale wasioweza kujiondoa katika kwapa la chama hicho – hakuweza kusimamia kile anachoamini hadi mwisho.

Sitta hakuangalia hadhi ya chombo anachokiongoza na mustakabali wake katika siku za usoni. Hakujihangaisha kutafiti kitachotokea kwa yeye kushindwa kusimamia kiapo chake cha kuongoza bunge litakalosimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Hayo yote hakuyaangalia.

Sitta anajua kuwa, tofauti na upotoshaji wa makusudi wa watendaji wa serikali wakiongozwa na Mathias Chikawe, waziri wa sheria na katiba, kwamba kazi ya bunge ni kushauri tu serikali; bunge limepewa mamlaka na katiba kusimamia na kushauri serikali kwa niaba ya wananchi.

Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inalipa bunge mamlaka ya kusimamia na kushauri serikali.

Hata hivyo, Sitta si kwamba hakujua yote hayo, bali alichoweka mbele ni marupurupu yake ya ubunge na nafasi yake ya uspika. Hakupima nyakati za sasa na zile za siku za usoni.

Lakini pamoja na uamuzi huo, kinyume na anavyofikiri, Sitta bado hayuko salama. Ni afadhali angeendelea na msimamo wake wa awali kuliko kujisalimisha. Haitarajiwi kwa watu walewale aliowatuhumu kwa zaidi ya miaka mitatu kumsamehe kwa “fungate” hili la kufunga mjadala.

Wala haitarajiwi kuwa wenzake waweza kuondoa tuhuma walizopanga kumshushia: Kudhoofisha serikali; kutoa nafasi zaidi kwa wapinzani wa serikali kuzungumza bungeni kuliko watetezi na kuhutubia bunge kuliko wabunge wenyewe.

Hata tuhuma ya kujenga mtandao wa kudhoofisha chama bungeni na kutumia bunge kuchafua wenzake, haziwezi kufutwa kwa uamuzi wake wa kuamuru kufunga mjadala.

Kibaya zaidi, hata wananchi ambao tayari walikuwa wameweka tumaini lao kwake la kurejesha taifa katika misingi yake ya asili ya enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere wanasema, “Sitta ametuangusha.”

Hili linapata nguvu zaidi kutokana na kukimbiwa na hata mtetezi wake, Rais Jakaya Kikwete ambaye taarifa zinasema amerejesha mahusiano yake ya asili na maswahiba zake – Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Ukiacha hayo mawili, kuna hili pia. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, nayo haikuwa salama. Baadhi ya wajumbe wa Kamati, hasa wale waliokuwa wamesimama kidete kuhakikisha serikali inatekeleza maazimio ya bunge, tayari walidhoofishwa.

Hii ni baada ya kutuhumiwa kutenda jinai ya kujipatia posho mbili kwa kazi moja. Si mara moja wala mbili, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe alinukuliwa akipinga amri ya TAKUKURU ya kuhoji juu ya jambo hilo.

Hatimaye Mwakyembe alisalimu amri kwa kile kilichoelezwa kuwa angeendelea na msimamo wake wa kutohojiwa, TAKUKURU wangemkamata na kumfikisha mahakamani kwa kosa la kukaidi wito halali wa taasisi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati, mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo tayari alishazibwa mdomo. Alihojiwa kwa tuhuma za kujipatia fedha mara mbili kwa kazi moja.

Katika kufunika kombe mwanaharamu apite, wakati akitoa taarifa ya Kamati yake bungeni juu ya Richmond, Shelukondo alisingizia hatua ya TAKUKURU kuhoji wabunge kuwa imezorotesha kazi yao.

Alisema Kamati yake haiwezi kuendelea kung’ang’ania Hoseah aondoke katika nafasi yake, wakati TAKUKURU inachunguza wabunge.

Lakini Shelukindo hakusema iwapo bunge lilikuwa limejichukulia mamlaka ambayo hayakuwa yake kwa kuchunguza vitendo vya kugushi.

Je, kama haya ndiyo yalisababisha mjadala kufungwa, bunge na serikali wako tayari kueleza umma kilichosababisha Lowassa kujiuzulu?

Je, kama hakuna mkosaji kwa bunge kuridhia ubabaishaji wa serikali, Rais Kikwete alikuwa na ajenda gani na Lowassa hata akakubaliana na matakwa ya Sitta na kundi lake?

Haya ni muhimu yakajulikana ili wananchi wapate kufahamu ukweli, hasa badala ya Kikwete na chama chake kugoma kumsafisha Lowassa.

Je, kama watuhumiwa wote – watendaji wa serikali –wamefutiwa mashitaka, bunge liko tayari kuomba radhi kwa kusababisha nchi kuwa shakani baada ya serikali kuvunjikia bungeni kwa tuhuma za kweli lakini ambazo zinakanwa hivi sasa?

Kama ndiyo. Je, bunge liko tayari kuwajibika kwa hasara iliyopatikana ya kuunda serikali mpya?

Ndiyo maana baadhi yetu tunasema wazi kuwa njia pekee ya kufanya bunge kuwa na meno na spika kuondokana na ukibogoyo, ni kumuondoa spika wa bunge katika minyororo ya chama cha siasa.

Katika nchi zilizoendelea kama Canada, wamefika mbali zaidi. Katika nchi hiyo, spika aliyepo madarakani na ambaye anatamani kuendelea na wadhifa wake, amewekewa hata utaratibu wa kutoruhusu mtu mwingine kugombea ili kumzuia kutumia nafasi yake kujipigia kampeni na kutenda kwa kufurahisha waliomuweka madarakani.

Sheria kama hiyo ingekuwapo nchini, Sitta asingetenda aliyotenda. Asingesimama bungeni na kujipigia kampeni kuwa atagombea tena katika kipindi kijacho. Asingejikomba kwa CCM kwa kulamba matapishi yake ili tu afanikiwe kurudi katika nafasi yake hapo mwaka kesho.

Hakika Sitta angebaki yuleyule wa “Kasi na Viwango.” Bali huyu sasa ni Sitta mwingine. Amegeuka nyuma na kugeuka “jiwe la chumvi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: