Sitta amsubiri Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 March 2008

Printer-friendly version

SPIKA wa Bunge, Samwel Sitta, anamsubiri aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Edward Lowassa, ili kumjumuisha katika moja ya kamati za kudumu za Bunge, MwanaHALISI limeambiwa.

Lowassa ambaye ni mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, anatakiwa kujiunga na wenzake katika Kamati za Bunge, baada ya kung'olewa katika nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Spika Sitta alilithibitishia MwanaHALISI mwishoni mwa wiki kuwa Lowassa hakujumuishwa katika kamati kama wenzake kutokana na kuondoka mapema bungeni kabla ya kujaza fomu za kuomba ujumbe.

"Hatukumuingiza katika Kamati kwa sababu, aliwahi kuondoka bungeni wakati ule kabla ya kujaza fomu za kuchagua kamati anayotaka," alisema Sitta.

Kanuni za Bunge zinataka wabunge kuchagua kwa kuweka alama kulingana na vipaumbele kila mmoja anavyoona vinafaa katika kamati husika. Jukumu la mwisho la kuwachagua linabaki kwa Spika.

Kukosekana kwa Lowassa katika orodha ya wajumbe wa kamati za Bunge kulionekana baada ya Spika kutangaza kamati mpya na orodha yake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari.

"Tunamsubiri, wala hatuna haraka naye. Akifika tutamueleza kwamba anatakiwa kuchagua kamati anayotaka kufanyia kazi. Na Mheshimiwa Lowassa anajua vema kanuni zetu, hivyo hatuna mashaka kwamba atachagua," alisema Sitta.

Katika muundo mpya wa Kamati za Bunge badala ya ule wa awali ulioruhusu kamati ziwe 13, Bunge sasa litakuwa na Kamati 17.

Kuundwa upya kwa kamati za Bunge kunatokana na kumalizika kwa muda wa kamati za awali.

Kamati za sasa zimegawanywa katika makundi matatu; Kamati zisizo za Kisekta, Kamati za Kisekta na Kamati za Taarifa za Ukaguzi.

Hii itakuwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mfumo wa vyama vingi, mtu ambaye ameshakuwa waziri mkuu, kuingia katika kamati za Bunge.

Uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati hizo ulitarajiwa kufanyika jana Jumanne, na hivyo kwa kuwa Lowassa alikuwa hajachagua Kamati ya kufanyia kazi, moja kwa moja amepoteza nafasi ya kuwa mwenyekiti.

Aidha, hatua ya Lowassa kutojaza mapema pendekezo la kamati anayotaka kujumuishwa, inamnyima fursa ya kushiriki katika kuchagua kiongozi wa kamati hiyo.

Washirika wa Lowassa katika sakata la Richmond ambalo ndilo lililowaondoa madarakani, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, tayari wamejiunga na kamati hizo.

Dk. Msabaha ameteuliwa mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, huku Karamagi akiwa katika Kamati ya Viwanda na Biashara.

Zakia Meghji, ambaye kabla ya mabadiliko ya baraza la mawaziri alikuwa Waziri wa Fedha, amekuwa mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: