Sitta atavuna aibu tupu kwa Dk. Slaa


Severine Yombo's picture

Na Severine Yombo - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Samwel Sitta

MGOMBEA ubunge jimbo la Urambo, Samwel Sitta, anatafuta aibu. Anadai kuwa anataka mdahalo na Dk. Willibrod Slaa.

Aibu anayotafuta Sitta, aliyekuwa spika wa Bunge hadi lilipovunjwa Agosti mwaka huu, imo hatika maeneo matatu.

Kwanza, hana ubavu wa kukabiliana na mtafiti na mwasilisha hoja zenye mantiki, Dk. Slaa ambaye anamfahamu tangu bungeni. Sitta anajadili hoja nyepesi.

Pili, kwa Sitta kutaka mdahalo na Dk. Slaa, ana maana kwamba Rais Jakaya Kikwete ameshindwa; kwamba yeye ndiye zaidi. Hili linaweza kutafsiriwa kuwa utovu wa nidhamu ndani ya CCM na dharau kuu – gross insurbodination.

Tatu, Sitta atakuwa amechoka au amechanganyikiwa, kwani hataki kufuata maelekezo ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni utawala wa CCM ulioelekeza kuwa wagombea wote – kuanzia ngazi ya diwani, wabunge hadi mgombea urais – hawapaswi kuingia kwenye midahalo ya aina yoyote.

Hapa Sitta hajui kuwa anatafuta kuitwa muasi ndani ya chama chake; sifa ambayo inaweza kumgharimu sana kisiasa.

Sitta hamwezi Dk. Slaa kwa kuwa ana hoja nyeyesi. Kwa mfano, anasema kama Dk. Slaa angekuwa anapinga mshahara mkubwa sana wa wabunge, kwa nini yeye hakuacha kuchukua mshahara huo kama mfano mdogo tu kwa taifa.

Tujibu: Kama watawala ambao Sitta anatetea na kulinda, wameweza kuruhusu, kushiriki au kufumbia macho wizi wa mabilioni ya shilingi (hadi 300/= bilioni) kutoka Benki Kuu na Hazina, kupitia makampuni feki waliyosaidia kuunda au waliyonyamazia je, mshahara wa Dk. Slaa ni kitu gani?

Kuvurugika kwa uchumi wa Tanzania na hasa kuporomoka kwa thamani ya fedha, pamoja na mambo mengine nje ya nchi, kumesababishwa na mabilioni ya shilingi yaliyomwagwa ovyo na mafisadi nje ya mkondo wa uchumi wa nchi unaoratibika.

Sitta hana jibu la hilo. Juzi aliparamia hoja ya kusomesha watoto wetu. Anasema haiwezekani wakasoma bila kubanwa mbavu kwa kutozwa fedha zaidi.

Spika wa zamani anapaswa kujua kuwa wananchi wanalipa kodi tayari. Kodi hiyo ndiyo inapaswa kugharamia watoto wao shuleni na vyuoni. Lakini serikali ya Sitta inataka juu ya kodi, wazazi waongezewe malipo mengine ya mamilioni ya shilingi kwa madai ya kinachoitwa kuchangia.

Kwa kuwa Sitta ni mwandani wa utawala uliopo; na kwa kuwa anatumia akili yake na nguvu zake zote kuutetea, tayari amekuwa kipofu. Hawezi kuona mabilioni ya shilingi yaliyoibwa na Kagoda Agriculture Limited kwa ruhusa ya watawala.

Hawezi kuona mikataba ya kidhalimu ya uchimbaji madini ambayo inaacha wananchi bila makazi, bila chakula, bila matumaini katika maeneo walikozaliwa na kuishi kwa miaka nendarudi.

Hataona jinsi serikali na taifa kwa jumla, lisivyovuna chochote cha maana kutokana na madini ya nchi hii, bali linaambulia mrabaha ambao unaamuliwa na wachimbaji ambao ndio wanajua walichochimba na makombo ambayo wanaachia serikali.

Sitta ataongea nini mbele ya mtafiti wa mambo makuu kama haya, kama siyo kuimba wimbo uleule wa kusifia wawekezaji na kuendelea kuwapigia magoti kana kwamba nchi hii siyo yetu?

Anachotaka Sitta siyo mdahalo na Dk. Slaa, kwa kuwa anajua hana takwimu wala hoja. Yeye anataka kujirudisha upya mbele ya CCM na serikali baada ya kukanuliana macho kwa kipindi kirefu mwaka jana

Hoja zinazotolewa hivi sasa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hazijibiki kirahisi; na kama siyo umasikini ulioghubika wananchi wengi na ujinga ambao CCM imefanya kuwa mtaji wake, Sitta na wakubwa zake wangekuwa wameondoka uwanjani wiki mbili zilizopita.

Hakika Sitta hana ubavu, siyo tu wa kuwa na mdahalo na Dk. Slaa, bali pia hata wa kujibu hoja za upinzani. CCM inaishi kwa mazoea. Vivyo hivyo viongozi wake, akiwemo Sitta.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: