Sitta, Dk. Mwakyembe hawatoki CCJ - Ng’hily


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

ANAJIAMINI na anasema anaweza kusimamia kile anachokiamini.

Ni Dickson Amos Ng’hily, mmoja wa vijana walioshiriki katika uanzishwaji wa Chama Cha Jamii (CCJ), miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. Alikuwa naibu katibu mkuu.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Ng’hily anasema, “Pamoja na CCJ kutosajiliwa, sijutii uamuzi wangu wa kuacha chuo na kujiunga na harakati za kuanzisha chama hiki.”

Anasema jambo linalomsikitisha ni hatua ya baadhi ya anaowaita “wanasiasa wakubwa,” waliokuwa pamoja katika suala hilo kupotosha ukweli wa kile walichokubaliana kukifanya.

Anasema: ”Inasikitisha kuona wanasiasa wanaoheshimika mbele ya umma; tuliokuwa tunakutana mara kwa mara; tuliokuwa tunapanga mikakati ya pamoja ya kuondoa utawala mbovu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo hii wanahaha kutaka kuficha ukweli kwa ajili ya madaraka. Hii si jambo zuri.”

Miongoni mwa anaowataja kuwa walikuwa pamoja katika kuanzisha CCJ, lakini sasa wanakana, ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Anamtaja aliyekuwa mbunge wa Kishapu, mkoani Shinyanga (CCM), Fred Mpendazoe kama mwanasiasa makini, shupavu na “mkweli katika kusimamia mlichokubaliana.”

Ng’hily anasema Mpendazoe ambaye alitangaza kujivua uanachama wa CCM Aprili 2010, kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kujitofautisha na Sitta, Dk. Mwakyembe na Nape katika kusimamia maslahi ya wananchi.

Anasema, “Ndani ya CCJ tulikuwa na msimamo mmoja, kwamba CCM haiwezi tena kuaminiwa na kukabidhiwa madaraka ya dola. Ni chama kisichofuata maadili, hivyo tulikubaliana tujitoe muhanga kwa ajili ya wananchi.”

“Lakini baadaye, hasa baada ya wenzetu kuahidiwa vyeo na wakubwa wa CCM, mambo yakabadilika. Wenzetu waliamua kumtosa Mpendazoe na kututosa sisi wengine. Na leo wanahaha wakikana ushiriki wao katika CCJ. Hili si jambo dogo linaloweza kuvumilika.”

Anasema hakutarajia Sitta na Dk. Mwakyembe baada ya kufanya kosa la kusaliti wenzao, wangeongeza kosa la kuficha ukweli na la kupotosha umma.

Ng’hily anasema, “Kwanza, hakuna mashaka kuwa CCJ kilikuwa chama chao. Ni wao waliokuwa wanawawezesha watendaji wa chama; wanaoleta siri za Baraza la Mawaziri; wanaovujisha siri za vikao vya Kamati Kuu (CC) na ndiyo waliokuwa wanaleta siri za usalama wa taifa.”

Akichambua kazi za kila mmoja, Ng’hily anamtaja Nape kuwa ndiye aliyekuwa akitoa siri za vikao vya CCM na mipango ya viongozi wake katika kumshughulikia Sitta, huku “Sitta akileta siri za vikao vya CC (Kamati Kuu) na Baraza la Mawaziri, wakati Dk. Mwakyembe akileta siri za Idara ya Usalama wa taifa.”

Anasema hata vikao vyao vilikuwa vya siri kwani, “Dk. Mwakyembe alikuwa anatuambia makachero walikuwa wanatufuatilia.” Anasema, “Kuna wakati tulitumia mbinu kali kufanikisha vikao vyetu vya ndani na vile vya mashauriano sisi watendaji.”

Anasema hata kabla ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kutamka kutoisajili CCJ, Sitta, Mwakyembe na Nape walikuwa tayari wamewaeleza kuwa kuna ugumu wa chama chao kusajiliwa.

“Kuna siku walituambia, ‘Tendwa amewaeleza ameagizwa asitoe usajili kwa CCJ kwa kisingizio cha kutokuwa na fedha za kufanya uhakiki wa wanachama.’ Ndipo Sitta akaahidi kuomba nchi wahisani kutoa fedha hizo,” anaeleza Ng’hily katika kile anachoita, “ukweli usioweza kupotoshwa.”

Ni vipi Ng’hily aliingia katika harakati za kuanzishwa CCJ? Anasema alishawishiwa kurejea nchini kutoka masomoni Afrika Kusini na kiongozi mmoja wa kidini ambaye ni rafiki wa Sitta na Mwakyembe kwa upande mmoja, na yeye kwa upande mwingine.

Hayuko tayari kwa sasa kumtaja kiongozi huyo, bali alipofika nchini alielekezwa kufanya kazi ya kusimamia usajili wa CCJ pamoja na kada mwingine wa CCM, Paul Makonda.

Ng’hily alikuwa Afrika Kusini akichukua shahada ya masuala ya uongozi na uandaaji filamu na vipindi vya televisheni katika Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal, Kompasi ya Cape Town.

“Huyu ndiye aliyeongea na mheshimiwa Sitta na kufanya makubaliano pamoja na mheshimiwa Mwakyembe, kwamba nirejee nchini ili kusaidia kazi hii ya kusajili CCJ,” anasema na kuongeza:

“Nilikubaliana nao na mara moja nikakatiza masomo na kurudi nchini ili kuja kushirikiana na wenzangu kuunda chama kipya. Lakini leo inasikitisha wenzangu wanakana chama chao; wanakana mpango wao na wanakana washirika wenzao. Hili si jambo jema kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa.”

Anasema alipokuja nchini alikutana mara kadhaa na Sitta na Dk. Mwakyembe na kwamba “ni wao waliokuwa wakijulisha hali ilivyokuwa inakwenda ndani ya CCM na uongozi wa juu serikalini kama hisia zao kuhusu harakati za CCJ.”

Anamtaja Sitta kama aliyekuwa kiungo kati ya CCJ na jumuiya ya kimataifa, kwani wanadiplomasia wa nchi mbalimbali za Magharibi walimuamini. Kwa upande wa Nape, Ng’hily anasema alikuwa na mchango mkubwa katika suala hilo ikiwa ni pamoja na  “kushiriki vikao mbalimbali vya mkakati.”

Lakini, anasema mara baada ya kuonekana CCJ haitapata usajili wa kudumu, majadiliano yalianza na viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mkakati huo, anasema taarifa zilitaja karibu wabunge 20 wakiwamo mawaziri watatu kuwa walikuwa mbioni kutoka CCM na kuingia CHADEMA kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

“Sisi tulikuwa tayari tumeondoka CCM. Sitta na Mwakyembe walitujulisha kuwa kuna wabunge 60 wangekuja nao baada ya bunge la tisa kufungwa na ikibidi watajiunga CHADEMA. Mipango ile ilitupa moyo sana,” anasema.

Anawataja baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwapo katika majadiliano kuwa ni pamoja na Freeman Mbowe, John Mnyika, Antony Komu, Erasto Tumbo na Tindu Lissu.

Anaapa kwamba anaeleza ukweli anaoufahamu ambao yupo tayari wakati wowote “kuueleza hata ikibidi mahakamani na kufungwa.”

Ng’hily alikerwa na CCM baada ya kubaini alichoita “sura halisi ya Sitta alipofahamu kuwa hatua yake ya kufunga mjadala wa Richmond bungeni ililenga mkakati wake wa kuendelea kuwa spika.”

Anasema Sitta aliitwa na Rais Jakaya Kikwete na kutakiwa kufunga mjadala huo kwa ahadi ya kuwa tena spika wa bunge baada ya uchaguzi wa 2010.

Dickson Amos Ng’hily alizaliwa 25 Juni 1978 kijiji cha Nyasho, wilayani Musoma. Alipata elimu ya msingi shule ya msingi Azimio Musoma na Nyamikoma, wilayani Magu.

Mwaka 1993 alijiunga na sekondari ya Royal College nchini Uganda. Alimaliza masomo mwaka 1996.

Alisomea kozi ya stashahada ya thioloji nchini Uganda. Mwaka 2000 alijiunga na masomo ya uandishi wa habari Chuo cha TIME, Ilala Dar es Salaam.

Ng’hily alifanya kazi gazeti la Citizen la kampuni ya Mwananchi Communication na gazeti la Guardian jijini Dar es Salaam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: