Sitta, Kabwe na Slaa msirudi nyuma


Isaac Kimweri's picture

Na Isaac Kimweri - Imechapwa 08 April 2008

Printer-friendly version
Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu CHADEMA

TANGU serikali ya awamu ya nne itangaze bajeti yake ya mwaka 2007/08 haijawahi kupumzika dhidi ya tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wake waandamizi.

Tuhuma hizi ni nyingi, zote ziliibuliwa wakati wa mkutano wa bajeti wa mwaka wa fedha 2007/08.

Kuna tuhuma za mkataba wa madini wa Buzwagi; Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA); na mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Corporation (LLC).

Serikali na chama tawala vilikuwa katika masukosuko mkubwa kutokana na tuhuma hizi.

Hata hivyo, tayari kuna majeruhi kadhaa. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, tayari amejiuzulu kutokana na tuhuma za Richmond.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha, nao wamemfuata Lowassa.

Kwa pamoja hawa waliguswa na kashfa ya Richmond.

Lakini ambalo halijahulikana wazi ni hadi sasa nani wengine watakaofuata baada ya mawaziri hao kufutwa kazi.

Hadi sasa suala la EPA ingawa linadaiwa kuigharimu nchi kiasi cha Sh. 133 bilioni zilizotafunwa na makampuni 22 yaliogushi nyaraka, bado nyuso za watu waliohusika hazijajitokeza katika kashfa hii.

Kumekuwa na juhudi kubwa za kuficha wahusika halisi, kwa maana ya watu wakubwa walio nyuma ya makampuni haya.

Kuna taarifa kuwa wengi wapo serikalini, kwenye chama tawala na wafanyabiashara wenye uhusiano na wakubwa na serikali na CCM.

Kibaya zaidi, inadaiwa kuwa CCM inahusika kwa kiwango kikubwa na kashfa ya EPA. Hili linazungumzwa wazi na bila kificho.

Wapo waliojitolea mhanga kuweka hadharani kashfa hizi. Miongoni mwao, ni viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); wapo wabunge wa vyama vya upinzani kwa ujumla wao; lakini pia kuna Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Sitta ameonyesha uvumilivu mkubwa kwa hoja zinazoikosoa na hata pengine kuiaibisha serikali na chama tawala tofauti na mtangulizi wake, Pius Msekwa.

Chadema, kupitia kwa wabunge wake, Dk. Willibrod Slaa (Karatu) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), wamekuwa mwiba kwa CCM na serikali yake.

Zitto aliibua sakata la Buzwagi lakini CCM kwa kutumia wingi wake bungeni ikamgeuzia kibao eti alidanganya hivyo kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge kwa miezi kadhaa; Slaa naye alikuwa mtu wa kwanza kuibua kashfa ya EPA ambayo bado inaitesa serikali.

Kashfa hii ndiyo imemtemesha Dk. Daudi Ballali kutoka ugavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikawatoa mawaziri Zakia Meghji (Fedha) na Basil Mramba (Viwanda, Biashara na Masoko).

Waliachwa katika uteuzi wa Baraza jipya la mawaziri badala ya lililovunjwa na Rais kufuatia kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri Karamagi na Dk. Msabaha. Mramba alikuwa Waziri wa Fedha (2005) wakati kashfa ya EPA inaasisiwa.

Baada ya matokeo ya Richmond yaliyoitikisa vilivyo nchi, mafisadi wa EPA na hata wa Richmond wanaoishi kwa hofu kubwa wakiogopa hata vivuli vyao, wapo katika mkakati wa kuchafua watu kwa lengo la kuviza mapambano dhidi yao.

Hadi sasa mbinu hizi chafu zimejidhihirisha zilivyotumika kumchafua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye chama chake kimeamua kwa dhati kuwasakama mafisadi.

Mbowe ameitwa fisadi kwa madai kwamba hajamaliza au amekataa kulipa mkopo aliokopa NSSF tangu miaka ya 80. Mbowe amesukiwa kashfa na magazeti yenye waandishi wanaodai kubobea katika utundu wa kuandika habari hizo kwa ukubwa wa kuogofya.

Bila ya aibu wala soni, wamekubali kuungana na mafisadi kukwamisha vita dhidi ya ufisadi.

Dk. Slaa naye hajasalimika. Kwa muda mrefu, CCM na serikali yake, imemlenga mbunge huyu kwa mengi. Vitimbi alivyofanyiwa wakati wa uchaguzi mwaka 2005, na hata madai ya kuwa alikula fedha za walemavu, ni mbinu tu za kumdhoofisha pamoja na chama chake.

Mafisadi wanataka kujenga picha kwamba katika nchi hii kila mtu ni mchafu na kwa sababu hiyo, wafanikiwe kuhalalisha uhayawani wao wa kutafuna nchi.

Mafisadi kwa kutumia mbinu hizo dhaifu hivi karibuni walimjengea Spika Sitta zengwe. Kwamba ni kiongozi mbadhirifu anayetumia madaraka kwa kujichotea fedha za umma kila anaposafiri; kwamba si mwaminifu katika ndoa kwani si tu anatembea nje bali pia anatumia zana za ofisi yake kugharimia vimada.

Kashfa dhidi ya Sitta inatengenezwa kwa maana moja, kwanza kumtia hofu ili aachane na msimamo wake wa kutetea hoja muhimu katika Bunge.

Pili, ni hofu anayojengewa kwamba hata kwenye hiyo nafasi wanaweza kumuondoa maana akishachafuka umma hautakuwa tena nyuma yake.

Nakumbuka ofisi ya Bunge imetoa taarifa kwa vyombo vya habari ikielezea kwamba walioko nyuma ya mpango huu wa kumpaka matope ni majeruhi wa Richmond na kwa kiwango kikubwa nataka wasomaji waamini kwamba hata mkono wa EPA nao upo hapa.

Sitta anatishwa kwa nini? Anatishwa ili apunguze msimamo wa kutetea hoja ili kuwapa wapinzani pumzi waliyonyang'anywa na Msekwa kwa miaka 10 mfululizo; wanataka ajae hofu ili suala la EPA lisifike bungeni.

Wanataka Sitta awe spika goigoi, apoteze kasi na viwango na hivyo Bunge lirejee utaratibu wa mabunge ya kati ya 1995-2005, Bunge la ndiyo mzee, Bunge lisilo meno na Bunge muhuri wa serikali.

Nitawasikitikia Sitta, Slaa, Kabwe na Mbowe kama watakubali kulegeza misimamo yao kwa sababu tu ya kutapatapa kwa mafisadi.

Haya matope yanayoasisiwa na mafisadi ni mkakati wa kizamani usioweza kuwasaidia katika nyakati tulizonazo.

Naamini mafisadi wameshakwama. Ni vema wakajua kuwa jini limetolewa kwenye chupa na katu hakuna wa kulirejesha. Vita dhidi ya ufisadi ni vita ya umma, wananchi, ya kutafuta uhuru wao ulioporwa na wale walioaminiwa na kupewa ofisi na umma.

Enyi Kabwe, Slaa, Sitta na Mbowe, msisite kuendeleza misimamo yenu hiyo inayojali ukweli na maslahi ya umma. Msije mkathubutu kudhoofisha uzito wa dhamira zenu. Hakuna kurudi nyuma!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: