Sitta kung’olewa uspika


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Spika wa Bunge Samwel Sitta

KUNA njama za kuwatoa “kafara” wabunge 15 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kusafisha njia ya urais wa Edward Lowassa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema iwapo wabunge hao watasalimika kwenye kura za maoni, jambo ambalo halitarajiwi; basi watatoswa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Wabunge wanaokamiwa ni wale waliojitambulisha kupambana na ufisadi nchini na ambao wamekuwa mwiba kwa kambi inayomuunga mkono Lowassa na swahiba wake Rostam Aziz.

Wengine ni pamoja na wanamtandao ambao wamekuwa wakilalamika kwamba Rais Jakaya Kikwete amemtosa Lowassa na wale wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Hata hivyo, uwezekano wa Lowassa kugombea mwaka huu ni mdogo kufuatia uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumwandaa tayari Rais Kikwete kugombea kwa ngwe ya pili.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kuangamizwa kisiasa kwa wabunge hao mwaka huu, kutatoa fursa kwa wanaotaka kushika utawala mwaka 2015 kujipanga kwa njia ya kuchukua nafasi muhimu katika bunge lijalo.
Uchaguzi mkuu mwaka huu umepangwa kufanyika 31 Okoba.

Chanzo cha habari kinasema maandalizi yamefanywa katika majimbo ya wabunge walengwa, ili wakipona kwenye kura za maoni wakumbane na uamuzi wa NEC.

Zengwe linalosukwa ni tuhuma za kuhujumu chama chao bungeni na kujivisha “ukamanda dhidi ya ufisadi.”

Tayari ushawishi mkubwa umepenyezwa kwenye vikao vya juu vya chama na una baraka za baadhi ya viongozi, taarifa zimeeleza.

Baadhi ya wabunge ambao wanatajwa kusukiwa mkakati wa kuangamizwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, mbunge wa Njombe Kusini na Naibu Spika, Anne Makinda, mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na mbunge wa Nzega, Lucas Selelii.

Wengine ni mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo, mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka; mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, Victor Mwambalasa, mbunge wa Lupa na mbunge wa Viti Maalum, Injinia Stella Manyanya.

Kwenye orodha ya wabunge wa kuangamizwa kisiasa, wapo pia mbunge wa Sikonge, Saidi Nkumba; mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro; mbunge wa Maswa, John Shibuda; mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi na mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo.

Habari zinasema mpango wa kuwang’oa wabunge hao umetengewa mamilioni ya shilingi na kwamba lengo ni kutaka kampeni dhidi ya ufisadi zisiendelee bungeni katika kipindi cha mwisho cha Rais Kikwete.

Aidha, taarifa zinasema wanaojipanga kwa utawala 2015 wanataka kuchukua nyadhifa za spika, wizara ya mambo ya nje na wizara ya fedha.

Makusudi makuu ya kutaka nafasi ya spika, taarifa zimesema, ni kuunda tume ya kurejea kashfa ya Richmond ambayo itapewa jukumu la kusafisha wote waliohusika.

Mlengwa mkuu katika mradi huu ni Lowassa ambaye alipoteza nafasi ya waziri mkuu kutokana na kushinikiza watendaji serikalini kuipa kazi ya kufua umeme, kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na hadhi, uwezo kifedha wala utaalam katika nyanja hiyo. Mbali na wabunge hao, mawaziri wawili, Profesa Mark Mwandosya na John Magufuri, nao wametajwa kuwa wanasukiwa zengwe la kuangamizwa kisiasa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Wanasiasa hao wawili, hawamo katika kundi la wabunge wanaofahamika kama makamanda wa ufisadi. Hata hivyo, kuingizwa kwao kunatokana na kuonekana kuwa wanaweza kujitosa katika kinyang’anyiro cha kutaka kumrithi Kikwete mwaka 2015.

Mwingine ambaye amelengwa na njama hizo ambazo inadaiwa zimetengewa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kile kinachoitwa “kulainisha wajumbe wa NEC,” ni Nape Nnauye aliyetangaza kugombea ubunge katika jimbo la Ubungo.

MwanaHALISI limeelezwa na baadhi ya wasaidizi wa viongozi waandamizi wa mpango huu kuwa tuhuma za wabunge na makada hao tayari zimeshaandaliwa.

“Lengo ni kuwafukuza kipindi cha lala salama na kuwaacha bila mahala pa kwenda kutokana na muda wa kuwasilisha majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumalizika,” ameeleza mtoa taarifa.

Kwa mujibu wa ratiba za vikao vya uteuzi vya CCM, mkutano wa Kamati Kuu (CC) unatarajiwa kufanyika Agosti 15, huku NEC ikipangwa kufanyika 16 na 17. Siku ya mwisho ya kupeleka majina Tume ya Uchaguzi ni tarehe 19 Agosti mwaka huu.

Kutokana na mahakama ya rufaa kutotoa uamuzi katika shauri linalotafuta mgombea binafsi, na kucheleweshwa kusajiliwa kwa Chama Cha Jamii (CCJ), wabunge hao watakuwa wameachwa njiapanda.

Gazeti hili lilishindwa kumpata Spika Sitta kueleza iwapo anafahamu njama hizo. Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Sitta alinukuliwa na gazeti la kila siku la Mwananchi akikiri kuwapo kwa mwanachama mmoja wa CCM anayewania jimbo lake.

Sitta alisema anaamini kuwa mwanachama huyo ametumwa na watuhumiwa wa ufisadi walioathirika kutokana na msimamo wake wa kupinga ufisadi ndani na nje ya Bunge.

Naye Anne Kilango amesema amewahi kusikia “mpango wa kutushughulikia. Kwa upande wa jimbo langu la Same Mashariki, upo ushahidi wa kutosha kwamba inawekwa mikakati ili mimi nisipate nafasi ya kugombea ubunge mwaka huu.”

Akiongea kwa sauti ya uchungu Kilango alisema, “Mtu ambaye anatajwa kutaka kuwania ubunge katika jimbo langu anafanya vitu ambavyo havilingani na uwezo wake.

Anagawa fedha. Mimi na wananchi wengine tumelilalamikia.”
Kilango amesema amerekodi kwenye CD ushahidi unaoonyesha namna mpinzani wake mtarajiwa na wenzake walivyokuwa “wakipanga jinsi ya kunishughulikia.”

Amesema amepeleka CD hiyo kwa Katibu Mkuu wa CCM kama ushahidi wa dhamira mbaya waliyonayo wapinzani wake. Aliyejitambulisha kuwa anataka ubunge Same ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Michael Kadege.

Dk. Kadege alipoulizwa iwapo anahusika na madai hayo alisema, “Hizo tuhuma za kuhonga anazozitoa Mama Kilango, ni za kupika. Yeye ndiye anayewapa hela watu na kuwaambia waseme mimi ndiye niliyewapa.”

Mwalimu huyo wa chuo kikuu amesema CD inayodaiwa kurekodi mikakati ya kumshughulikia Kilango, “ni uongo mtupu. Anatembea nayo kila mahali lakini haina chochote. Ni feki.”

Dk. Kadege amesema tayari amewasilisha malalamiko yake kuhusu Kilango “kwa chama chetu kama taratibu zinavyotaka. Mama Kilango ni mvurugaji tu na tuhuma zake ni za kutunga.”

Kwa upande wake, mbunge wa Kahama, James Lembeli amesema ana taarifa juu ya kuwapo kwa mpango wa kuwashughulikia.

“Jimboni kwangu tayari nimeanza kuwaona wale waliotumwa kutekeleza mpango huo. Utakuta mtu hana shughuli yoyote pale Kahama mjini na anavaa viatu bila hata ya soksi, lakini ameanza kubadilika ghafla katika siku za karibuni,” amesema Lembeli.
Amesema mwanachama huyo amekuwa akichukua teksi kutoka Kahama mjini hadi ndani ya jimbo, umbali wa kilometa 100 hadi 120 kuwaambia wananchi kwamba Lembeli hajafanya kitu jimboni.

“Mimi nawaambia watu hawa kwamba kwanza wanunue soksi za kuvalia viatu, kabla ya kuja kwangu kufanya fitina,” amesema Lembeli kwa kicheko na kuongeza, “Nitapambana nao.”

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, amegoma kuzungumzia njama za kuangamiza baadhi ya wabunge kisiasa. Amesema, “Sina cha kuwaambia.”

Taarifa zinasema jambo linalohitajika kufanywa haraka, hata kama walengwa wa njama wataingia bungeni, ni kuhakikisha kuwa Sitta hachaguliwi kuwa Spika wa bunge lijalo.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Spika wa bunge amepangwa kuwa ama Edward Lowassa au mfuasi wake ambaye atakuwa na kazi moja tu ya kumsafisha Lowassa kutoka tuhuma za mkataba wa Richmond.

“Tukimaliza uchaguzi, Spika wa Bunge la Jamhuri, atakuwa ama Lowassa au yeyote ambaye atalinda maslahi yetu. Yule bwana aliyejiita speed and standard, uspika atausikia redioni,” amesema mtoa taarifa kwa sauti ya kujiamini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: