Sitta kung'olewa?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Samwel Sitta

KUJITOSA kwa Andrew Chenge, katika mbio za kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri, kumelenga kumuengua Samwel Sitta aliyeshika kiti hicho kwa miaka mitano iliyopita.

Taarifa za ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinasema Chenge amejitosa kuwania nafasi hiyo ili kushinikiza vikao vya juu vya chama chake kumuengua Sitta katika kuwania nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kuangamizwa kisiasa kwa Sitta, kutatoa fursa kwa wanaotaka kushika utawala mwaka 2015 kujipanga kwa njia ya kuchukua nafasi muhimu katika bunge lijalo.

Wanaotajwa kuwa pamoja na Chenge kumuangamiza Sitta kisiasa ni pamoja na waziri mkuu aliyefukuzwa na Bunge, Edward Lowassa na swahiba wake mkuu, Rostam Aziz.

“Chenge hakujitosa kushinda. Tumempeleka ili kushinikiza vikao vya juu vya chama kumuondoa Sitta katika kuwania nafasi hiyo. Ndiyo maana Chenge ameingia kwa staili ya kurusha makombora,” ameeleza mmoja wa wanamtandao wanaomuunga mkono Chenge.

Taarifa zinasema Chenge na kundi lake wanaamini kuwa hatua ya kumshambulia Sitta itawafanya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama, kukata jina la Sitta kwa maelezo kwamba “Bunge halitatawalika.”

“Unajua ndugu yangu, hapa tunataka kuonyesha kwamba yale makundi ambayo yaliundiwa hata kamati ya Mzee Mwinyi bado yapo, na kwamba kumrejesha Sitta katika nafasi yake kutafanya Bunge lisitawalike,” anasema.

Anasema, “Huo ndiyo msigi wa sisi kuamua kunoa mapanga asubuhi. Tunataka CC wakate majina yote mawili” – Chenge na Sitta.

Chanzo cha habari kinasema maandalizi yamefanywa ili Sitta akiondoka, karata ya watuhumiwa wa ufisadi ielekezwe kwa Anne Makinda.

Makinda ambaye alikuwa naibu Spika katika Bunge lililopita, amejitosa kuwania nafasi ya spika katika mazingira yaliyojaa utata.

Miezi miwili iliyopita, gazeti hili liliripoti kuwa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini walimfuata Makinda na kumuomba kuwania nafasi hiyo.

Tayari ushawishi mkubwa umepenyezwa kwenye vikao vya juu vya chama na una baraka za baadhi ya viongozi, taarifa zimeeleza. 

Mbali na Rostam na Lowassa, vigogo wengine wanaotajwa kutengeneza mkakati wa kumungamiza Sitta, ni katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili iliyopita, Chenge alijikita katika kueleza kile alichokiita udhaifu wa uongozi wa Bunge la Tisa. 

Alipobanwa na maswali kutoka kwa waandishi wa habari mbalimbali nchini, Chenge alisema, “…kulikuwa na ombwe la uongozi. Na hili ndilo lilinisukumu kugombea nafasi ya Spika."

Alidai kuwa uongozi uliopita ulitumia muda mwingi kuruhusu hoja binafsi ambazo hazikuwa na maslahi kwa taifa, kitu ambacho alisema kimechangia kudhoofisha chama chake.

"Kilichotokea wabunge wote wa chama tawala na upinzani waliungana dhidi ya serikali... hii si sahihi. Uongozi wa namna hiyo ni wa kuogopa kama ugonjwa wa ukimwi," alieleza.

Akijibu madai hayo ya Chenge, Sitta aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu kuwa “hawana lolote. Hizo ni kelele za majizi wanaohofu nikirejea katika kiti kile watashindwa kupenyeza ajenda zao za kifisadi.”

Alisema akiwa mwanasheria aliyebobea na anayeifahamu vema kazi yake, anajua kazi zote za Bunge, na kwamba uongozi wake ulitenda kazi zake kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za Bunge.

Mbunge mmoja wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina gazeti alipoulizwa juu ya nafasi ya Chenge katika kinyang’anyiro hicho, alijibu haraka:

“Yaani sisi wabunge, tuchague Spika ambaye mara anaomba ruhusa ya kurejea Dar es Salaam kushughulikia kesi yake ya kibajaji… Hilo haliwezekani.”

Chenge anakabiliwa na lundo la tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka wakati akiwa mwanasheria mkuu wa serikali. Miongoni mwa tuhuma ni kushindwa kueleza utajiri wake akiwa mtumishi wa umma.

Wakati vita kali ikipiganwa ndani ya CCM, kambi ya upinzani imejipanga kucheza karata ya kuhakikisha wanashinda nafasi hiyo. 

MwanaHALISI limeelezwa kuwa tayari vyama viwili vikuu vya upinzani nchini – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), vimejipanga kusimamisha mgombea mmoja kuwania nafasi ya spika. 

Mgombea huyo atakuwa ama mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed, au mwanasheria mashuhuri nchini, Mabere Marando.

Kambi ya upinzani inatarajiwa kuwa na wabunge kati ya 90 na mia moja katika Bunge hili. Kwa hesabu hiyo watatakiwa kupata kura 72 kutoka kwa moja ya kambi zinazoshindana ili kuweza kushinda.

Hadi tunakwenda mitamboni Jumatatu usiku, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilikuwa haijatangaza majina ya wabunge wa Viti Maalumu.

Lakini kuna kila uwezekano wa CHADEMA kuwa kiongozi wa upinzani katika Bunge la sasa.

Hii ni kwa sababu, ingawa CUF kimefanikiwa kupata viti 24, viti viwili zaidi ya CHADEMA, kitazidiwa kwa wingi wa wabunge wa viti maalum kutokana na idadi kubwa ya kura walizopata.

“Kama Chenge atapitishwa na chama chake kuwania nafasi ya uspika, tunaamini kuwa mgombea wetu atapenya,” ameeleza Profesa Mwesiga Baregu, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA.

Anasema hii ni kwa sababu wale waadilifu waliopo CCM “wataweza kutuunga mkono. Hatutarajii katika hili, kuungana na kumchagua Chenge.”

Hali hii inaweza kuwagawa wabunge wa CCM katika makundi mawili na iwapo kundi moja litaungana na upinzani ambao nao utakuwa na mgombea, hapo ndipo kwenye uwezekano wa mgombea wa upinzani kuchukua nafasi hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: