Sitta, Mwakyembe shujaa wa nani?


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Samwel Sitta

WALIOJIITA wapiganaji dhidi ya ufisadi na watetezi wa maslahi ya taifa, sasa wako “sebuleni” katika serikali ya rais Jakaya Kikwete.

Ni Samwel Sitta, spika wa bunge la tisa la Jamhuri na Dk. Harrison Mwakyembe, mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa Richmond.

Vinara hawa wawili, wiki iliyopita walijikuta njia panda ya kufanya uamuzi mgumu katika maisha yao ya kisiasa baada ya kuteuliwa kuingia katika baraza jipya la mawaziri.

Kwa miaka mitano iliyopita, wanasiasa hawa wawili, wamekuwa wakiikosoa serikali ya Rais Kikwete kuwa inashindwa kufanya maamuzi magumu.

Sasa wao wamechukua uamuzi mgumu. Wamekubali uteuzi wa Rais Kikwete kwenye baraza lake la mawaziri. Ni uamuzi wa gharama lakini ungekuwa wa gharama ileile pia kama wangekataa uteuzi.

Kwa kuukubali uteuzi kama walivyofanya, wanaanza maisha mapya yatakayotawaliwa na unafiki, hatia na taswira ya usaliti kwa harakati walizozianzisha na kuzitelekeza katikati ya mapambano.

Sasa Sitta na Mwakyembe wameingia serikalini, ingawa si kama ambavyo wenyewe walitaka.

Kwa mfano, baada ya kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha spika, inadaiwa na marafiki wa Kikwete na Sitta, kuwa spika wa zamani alitaka kuwa waziri wa sheria na katiba.

Naye Mwakyembe anadaiwa kuhaha hapa na pale akitafuta kuwa waziri na hatimaye kuambulia unaibu, huku wengi wa wanafunzi wake wakipewa uwaziri.

Katika mazingira haya, hatuhitaji mnajimu mwingine wa kutueleza nini kitatokea mbeleni.

Jibu liko wazi: Hali zao katika utendaji serikalini haziwezi kuwa tofauti na watendaji wengine ambao waliteswa sana na matamshi yao ndani na nje ya Bunge.

Historia imejaa watu ambao walianzisha harakati za kudai mambo kadhaa, lakini pale walipoteuliwa na kuingia katika serikali, hatukuwasikia tena wakidai au kupiga kelele kama ilivyokuwa awali.

Mathalani, Philip Marmo, Njeru Kasaka na wengine wengi, walijitosa kuanzisha harakati za kudai serikali ya Tanganyika ndani ya Mungano. Walijiita G55.

Harakati zao ziliungwa mkono ndani na nje ya chama tawala. Lakini baada ya Sitta, Marmo na Kasaka kuingia serikalini, ndiyo haohao waliopewa jukumu la kuandaa hoja ya kupinga serikali ya Tanganyika na hoja hiyo kuizikwa.

Hadi leo, usaliti huu unaendelea kuwatafuna baadhi ya wafuasi wao na nina uhakika bila ya ndugu hawa kuja hadharani kufafanua usaliti wao, hawatakaa waaminike.

Kwa bahati mbaya hata muda wao wa kuishi katika siasa umebaki mdogo, kwa hiyo wanaweza kwenda mbele ya haki na mzigo wa usaliti waliowafanyia Watanzania walioitikia harakati zao.

Kama ilivyokuwa kwa G55, hata katika kundi la vinara wa kupambana na ufisadi, usaliti umejitokeza kwa kuwatosa wapiganaji wenzao.

Baadhi ya waliokuwa katika kundi la G55 hawajulikani hata waliko. Imesikitisha zaidi kuona mtu kama Sitta akikaa kimya, kwa miaka mitano akiwa spika, bila hata ya kujaribu kuonyesha umuhimu wa kuandaa katiba mpya inayoweza labda, kufufua sehemu ya ndoto za kundi la G55.

Katika hali hii, Sitta amepoteza fursa ya kujenga kumbukumbu muhimu katika historia ya taifa letu. Hatutawashangaa watakaopendekeza kuwa Sitta huongozwa zaidi na maslahi yake binafsi.

Nafasi yake ya uspika ilikuwa nzito kwa kuwa pamoja na maslahi mazito ya kiitifaki, lakini pia alijijengea jina kubwa kwa kuwa na fikra za maendeleo katika taifa.

Baadhi ya wafuasi wameadhibiwa na wapiga kura wao kwa sababu tu waliamua kuchukua uamuzi mzito wa kumsikiliza na kumfuata.

Orodha ya “walioadhibiwa” kwa kuwa pamoja na Sitta ni ndefu. Inahusisha akina Lucas Sellelii, Aloyce Kimaro, Benson Mpesya, William Shelukindo na Fred Mpendazoe.

Mmoja wa waathirika hawa wa usaliti wa Mwakyembe na Sitta ameniambia kuwa, “Kwa kuwa Sitta na Mwakyembe wanapenda harakati zisizo na gharama, watajikuta wanauza utu kwa kuwapigia magoti mafisadi na kuwaomba radhi.”

Kwa kuwa sasa sura halisi za wanaharakati hawa ziko wazi mbele ya wananchi, ni vema tukajiuliza: Nani hasa mtetezi wa kweli wa maslahi ya Watanzania?

Jitihada za CCM kuua upinzani wa ndani wa chama hicho umefanikiwa kwa kuwanasa Sitta na Mwakyembe.

Rais Kikwete, akiwa rafiki wa watuhumiwa wengi wa ufisadi, ametumika vema kuiua ajenda ya “wanaharakati” hawa na sasa mafisadi wanaweza kula mawindo yao bila kubughudhiwa na kelele za “makamanda.”

Mwadhama Kardinali Pengo aliwahi kusema katikati ya mnyukano juu ya Richmond kuwa, kelele za wapinga ufisadi zaweza kuwa ni kilio cha kukosa nafasi ya kufisidi na wala si kelele za kweli zenye uzalendo ndani yake.

Je, maono ya Mwadhama Pengo yaweza kuwa yametimia sasa?

Jitihada za CCM kuua upinzani nje ya CCM pia zimefanikiwa kwa kuwazibia hewa viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuwafanya wajisalimishe kwao kupitia kinachoitwa, “Serikali ya umoja wa kitaifa.”

Kama walivyonaswa Sitta na Mwakyembe, ndivyo CUF walivyojikuta wakidai wao ni wapinzani, lakini bila hata kuamini wasemalo.

Kilichobaki sasa ni CUF kuwa “chama cha upinzani” kinachopinga upinzani na siyo CCM waliyofunga nayo ndoa.

Kitendo cha Sitta na rafiki yake Mwakyembe kukubali kuwa sehemu ya serikali waliyokuwa wakiikosoa kwa muda mrefu, kina faida zaidi kwa watuhumiwa wakuu wa ufisadi kuliko taifa.

Hatua yao yakuingia serikalini haina faida kwao wala kwa taifa, kutokana na mfumo wa kifisadi uliojikita serikalini na majeraha makubwa waliyoyasabisha wao kupitia mfumo huo.

Kutokana na utaratibu wa “uwajibikaji wa pamoja,” hawawezi kutofautiana na mfumo huo wakiwa ndani.

Ama kwa hakika, mkono usioweza kuukata, si bora kuubusu? Wameubusu. Jamii inawaonaje? Wao wanajionaje?

0
No votes yet