Sitta, Rostam wapasua CCM Igunga


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Samwel Sitta

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaingia katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, kikiwa kimekatika vipande viwili, imefahamika.

Taarifa za ndani ya vikao vya mkakati vinavyofanyika mjini Igunga zinaonyesha CCM kiko hatarini kupoteza jimbo hilo kutokana na migawanyiko inayodaiwa kuchochewa na baadhi ya viongozi wake wakuu.

Habari zinasema mgawanyiko huo umesababisha baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani Tabora na wilayani Igunga, kususia ziara zilizopachikwa jina la “kufufua chama” zinazofanywa na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi.

Miongoni mwa waliotajwa kuwa wamesusia kampeni hizo, ni mwenyekiti wa wilaya ya Igunga, Felix Mkude, katibu wa uchumi na fedha, Ahmed Jambeki na baadhi ya wajumbe wa halmashauri ya wilaya na kamati ya siasa ya wilaya.

Wakasuvi, anayeaminika kutoka kundi la Samwel Sitta, anapingwa na baadhi ya wafuasi wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Rostam Aziz kwa maelezo kwamba anatumia nafasi hiyo kuwashambulia.

Imeelezwa kuwa katika kikao cha kamati ya siasa ya mkoa wa Tabora, kilichofanyika wiki iliyopita katika ofisi za CCM wilaya, mjini Igunga, Wakasuvi alimtuhumu, kwa maneno makali, Rostam na baadhi ya wafuasi wake kwa kusema, “Hata kama mliomo humu ndani ya kikao wengine bado mmenuna, hiyo ni shauri yenu. CCM kitashinda tu. Kama tuliweza kushinda Nzega, na Igunga tutashinda.”

Alisema, “Hata kama Rostam Aziz ana pesa, hawezi kuwa maarufu kuliko chama chetu. Hapa tutashinda uchaguzi hata bila yeye.”

Alisema CCM kitashinda uchaguzi huo “kwa gharama yeyote ile” kwa kuwa ni chama chenye dola.

Wakasuvi ambaye amejitambulisha mara kadhaa kuwa mfuasi mwaminifu wa Sitta, anayetajwa kuasisi Chama cha Jamii (CCJ) wakati akiwa bado kiongozi ndani ya CCM, ni miongoni mwa wanachama na viongozi walioaminika wengemfuata Sitta kwenye chama chake hicho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwamo makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa, Mweka Hazina Nchemba Mwigulu, mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage na mjumbe wa NEC na mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Tabora, Munde Tambwe.

Katika maelezo yake kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, Wakasuvi alimtuhumu Rostam kwa kushindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Alisema, “Tutatumia pesa, tutatumia dola na tutashinda. Hatutishwi na wanasiasa wanaosema tunataka Igunga ipotee ili tuheshimiane.”

Wengine aliowatuhumu ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Igunga, Abubakari Shabani ambaye anatajwa kutoka kundi la Rostam.

Rostam alijiuzulu nafasi zake zote za uongozi ndani ya CCM ukiwamo ubunge na ujumbe wa NEC, 14 Julai 2011 kwa kile alichoita, “kuchoshwa na siasa uchwara, chuki na kufitiniana miongoni mwa viongozi na wanachama.”

Alikuwa mbunge wa Igunga tangu mwaka 1994 alipoingia kupitia dirisha la uchaguzi mdogo.

Taarifa zinasema Wakasuvi haelewani na baadhi ya viongozi wa wilaya za mkoa wa Tabora kwa kile kinachoelezwa kuegemea katika kundi la Sitta aliyedaiwa kuwa mmoja wa mahasimu wakubwa wa Rostam.

Tayari CC imempiga marufuku Nape Nnauye na John Chiligati kukanyaga Igunga katika kipindi hiki cha kampeni kwa kile kilichoitwa, “kukiepusha chama na balaa la kushindwa uchaguzi.”

Mkutano wa CC uliofanyika Dodoma wiki mbili zilizopita taarifa zinasema, ndiyo uliopendekeza Nape na wenzake kutoshiriki kampeni za Igunga, jambo ambalo liliafikiwa na Kikwete.

CC iliamuru kampeni kufanywa na wabunge, viongozi wa mkoa na wilaya za mkoa wa Tabora baada ya baadhi ya wajumbe kuonya hatari ya chama kumtumia Nape, Chiligati na wenzao katika kampeni hizo.

Nape anatajwa na baadhi ya wenzake kwenye chama kuwa ni sehemu ya matatizo yanayokikumba chama hicho hivi sasa.

Hata hivyo, mwenyewe amekana madai hayo kwa maelezo kuwa matatizo yote yanayoikumba CCM yamesababishwa, pamoja na mambo mengine, na mtandao wa Rais Jakaya Kikwete wa mwaka 2005. Anasema mtandao huo ndio uliokivuruga CCM.

Mwigulu aliwaambia wajumbe wa kikao cha Igunga, “CCM kinahitaji kiasi cha Sh. 800 milioni kugharamia mipango ya ushindi wa kiti hiki.” Aliwataka wana-CCM kuweka pembeni tofauti zao.

Alipoulizwa Wakasuvi, iwapo alitoa kauli kuwa CCM wana fedha na dola na kwamba watashinda, alikana kutamka hayo. Alihoji, “Hizi habari hasa umezipata wapi maana katika kikao chetu hakukuwa na mwandishi wa habari hata mmoja?”

Alipoelezwa taarifa zimetoka ndani ya kikao alichokiongoza, Wakasuvi alisema, “Hizo taarifa ni za uongo na unafiki na zenye nia ya kuchonganisha wanachama wa CCM. Chama kipo imara Igunga na nimewasiliana na Rostam juzi tu; naye amenihakikishia atashiriki kikamilifu kuleta ushindi.”

Taarifa zinasema mara baada ya Wakasuvi kutoa kauli ambayo wengi wameita ya utata, Mwigulu alisimama na kusema, “Si vizuri kutumia kauli za mafumbo ya taarabu. Hata ushindi wa Nzega si wako binafsi. Hakuna mtu mwenye uhalali wa kusema mimi ndiye niliyeipa CCM ushindi.”

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Mwigulu alisema, “Bila CCM kuungana, kamwe hatuwezi kushinda uchaguzi huu.”

Mwigulu alitoa kauli hiyo baada ya kubaini Wakasuvi ametumia muda mwingi kushambulia viongozi wenzake.

Kauli ya “tunataka Igunga ipotee (kwa upinzani) ili tuheshimiane” iliripotiwa kutolewa na kada wa CCM, Hussen Bashe katika mazungumzo yake na katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama.

Mukama na Bashe walikutana mjini Dodoma wakati wa mkutano wa baraza kuu la umoja wa vijana (UV-CCM).

Inadaiwa kauli ya Bashe ilitokana na maombi ya Mukama ya kumtaka awanie ubunge wa Igunga. Bashe ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya New Habari Corporation inayomilikiwa na Rostam.

Mwingine ambaye alimshambulia Rostam, ni Aden Rage ambaye pia anatajwa katika kundi la Sitta. Alisema, “Huyu bwana (Rostam Aziz) hajafanya chochote. Ameshindwa kufufua kiwanda cha kuchambua pamba kwa miaka 10.” Kiwanda hicho kipo Igunga.

Wakati Rage akimtuhumu Rostam kushindwa kuondoa umasikini Igunga, naye ameingia katika mgogoro mkubwa na mkurugenzi wa manispaa ya Tabora baada ya kiongozi huyo wa serikali kugoma kutekeleza “matakwa binafsi” ya Rage.

Habari zinasema Rage aliahidi kuchimba visima vya maji ndani ya siku 100 kwa kila kata ya Tabora Mjini; ujenzi wa madarasa na kutoa  mabati katika baadhi ya shule, mambo ambayo hajatekeleza mpaka sasa.

Kiongozi mmoja wa CCM aliyehudhuria mkutano huo ameliambia gazeti hili, “Wamekuja hapa kutuambia mabaya ya Rostam. Kwamba ni fisadi. Tumewasikia. Lakini kwetu sisi tunamuona tofauti.. Umasikini wa Igunga unatokana na kulazimishwa na CCM kulima pamba na kukopwa kwa pamba yetu,” ameeleza.

Hadi siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu, wanachama 13 wa CCM walikuwa wamejitosa katika kinyang’anyiro hicho. Waliojitosa ni pamoja na Ngassa Nicolaus, Amina Ally Said, Shams Feruzi, Adam Brown, Shell David, Dk. Peter Kafumu, Makoba Mchenya, Joseph Ali Omary, Seif Hamis Gulamaly, Hamis Shaaban, Nathan Mboje, Hamad Hemed Safari na Paul Ndohele.

Upinzani mkali katika uchaguzi wa Igunga unatarajiwa kuwa kati ya wagombea watakaopitishwa na vyama vya CHADEMA na CCM.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: