Siyo Bajeti ya 'Kilimo kwanza'


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 June 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWA mwaka wa fedha unaomalizika Juni 2009, serikali ilishindwa kukusanya Sh. 652 bilioni zikiwa sehemu ya matarajio ya matapo yake iliyojipangia.

Katika bajeti ya 2009/2010 serikali imepanga kutumia Sh. 9.5 trilioni. Kazi ya kukusanya kodi iko paleplale.

Kushindwa kukusanya kodi kunaweza kuelezwa kwa njia mbalimbali: Kukataa kutoza kodi; kukusanya fedha na kuzitafuna; kukosa stadi za kufanya kazi hiyo; uzembe au hujuma.

Njia hizo ndizo donda ndugu zilizokosa tiba mjarab, mwaka hadi mwaka. Lakini hakuna njia bora tunazoona serikali inachukua kubana watumishi waliopewa jukumu hili.

Tunachoweza kusema ni kwamba, pasipo na hatua za kweli na wazi, basi tutegemee yaliyotokea katika bajeti iliyopita hata katika bajeti inayoendelea kujadiliwa.

Lakini kushindwa kukusanya au kufuja kodi ni mambo ambayo yanajirudiarudia hata katika mipango ya nchi na hata katika bajeti ya sasa.

Kuna hizi Sh. 300 bilioni zilizotengwa kudhamini  makampuni na wafanyabiashara walioshindwa kulipa madeni kwa mabenki na taasisi za fedha kutokana na kukosa bei nzuri ya mazao ya kilimo.

Tueleze mapema kuwa zitaliwa tu. Nani anatambua nani na nani walitumia vizuri fedha walizokopa na wapi zilitumika? Hawa wanapatikaje kwenye bajeti kabla walipakodi hawajawatambua?

Fedha hizi, zinazoonekana kuwa mgawo maalum kwa “wafanyabiashara bubu,” zitanufaishaje wakulima? Nani anasema hawa waliolazimika kuuza mazao yao kwa bei ndogo kuliko iliyotangazwa na serikali?

Katika mazingira ya kusahau, kudharau au kutothamini mkulima mdogo, yuko wapi mwenye kifua cha kusema bajeti mwaka huu imezingatia “Kilimo kwanza.”

Hata kile kidogo kilichokusanywa, na huenda kwa bahati tu, hakimfikii mkulima. Hii haiwerzi kuwa bahati mbaya. Ni mpango maalum wa kumtelekeza na kumteketeza mkulima.

Bali ni wazi. Katika kunyang’anyana kodi ya wananchi, waliopewa majukumu hawawezi kukumbuka mkulima.

Watapangana 60 katika uwaziri; watanunuliana magari ya kila moja Sh. 130 milioni; watapanga safari za ndani na nje; wataishi kifalme.

Watasamehe kodi hata pasipostahili ili walambe asali japo kwa uficho; wataita wawekezaji ambao watamegeana nao utajiri wa nchi hii na kuwalinda kwa nguvu zote.

Ndio maana hata pale Mkulo anapotangazia umma kuwa bajeti imezingatia “Kilimo kwanza,” kila mwenye akili nzuri anamshangaa. Katika kinyang’anyiro hiki mkulima hafiki, hashiriki wala hawakilishwi.

Wakati mwingine tuiambie serikali, kwamba isichukulie wananchi wote kuwa hawana uwezo wa kufikiri. Tarakimu na matendo ya serikali katika bajeti havionyeshi kumlinda mkulima.

0
No votes yet