SMZ yalazimisha mradi wa mafao


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kutumia mbinu za kilaghai ili kufanikisha azma yake ya kutengeneza mafao ya viwango vikubwa kwa ajili ya viongozi wa kitaifa wakishastaafu, MwanaHALISI imegundua.

Vyanzo vya taarifa kutoka serikalini na ndani ya vyama vya CCM na CUF vinavyounda serikali ya umoja wa kitaifa (SUK), vimefahamisha kuwa baada ya kubaini upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria iliouandaa, sasa inafanya matumizi yasiyo ya lazima kuujengea hoja.

Moja ya mbinu hizo ni kuwalipa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi posho nzito ili kujadili muswada huo katika semina maalum iliyofanyika wiki iliyopita mjini Zanzibar.

Semina hiyo ya siku moja, ilishirikisha wajumbe wote wa baraza la wawakilishi pamoja na wajumbe ambao ni mawaziri na naibu mawaziri katika serikali.

Kila mjumbe aliyehudhuria semina hiyo alilipwa Sh. 100,000 kama posho ya mahudhurio. Baraza la Wawakilishi lina wajumbe 75.

Semina hiyo iliandaliwa na serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, inayoongozwa na waziri Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.

SUK imeandaa muswada mpya wa “Sheria ya Maslahi na Mafao ya Viongozi wa Kisiasa Baada ya Kustaafu” itakayofuta Sheria ya Ulipaji Mafao ya Viongozi wa Kitaifa Nam. 4 ya mwaka 1988 na Sheria Viongozi wa Kisiasa Nam. 6 ya mwaka 1999.

Katika muswada huo mpya, serikali inawataja viongozi husika wa kulipwa mafao baada ya kustaafu, kuwa ni Rais, Makamu wa Rais, Mawaziri, Washauri wa Rais, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wajumbe wa baraza la wawakilishi.

Ingawa sheria zilizopo zimekuwa zikilipa mafao viongozi kadhaa wa kitaifa – rais, waziri kiongozi, mawaziri, spika na wajumbe wa baraza la wawakilishi - wakishastaafu, imeonekana serikali inataka kuongeza viwango vya mafao na idadi ya watu wa kufuatana kimafao na viongozi hao.

Sheria mpya imekusudiwa kuwaingiza katika mkumbo huo makamu wawili wa rais, wadhifa uliotengenezwa katika mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010 kwa ajili ya kutekeleza maridhiano ya kisiasa yaliyosainiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Sheria mpya ya mafao inamuondoa waziri kiongozi, nafasi ambayo imefutwa kutokana na mabadiliko hayo ya 10 ya katiba.

Kwa muundo wa sasa wa Serikali ya Mapinduzi, wasaidizi wakuu wa rais ni makamu wawili, mmoja akitoka chama alichotoka rais aliyeshinda uchaguzi na mwingine akitoka chama ambacho mgombea wake wa urais alitangazwa kushindwa.

Makamu anayetoka chama alicho rais anakuwa makamu wa pili na kiongozi mkuu wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Sheria mpya inapendekeza kuwa rais, pamoja na maslahi mengine, atalipiwa watumishi 11, makamu wake wawili watalipiwa watumishi wanane kila mmoja, na spika atalipiwa mtumishi mmoja baada ya kustaafu.

Watumishi hao ni pamoja na wasaidizi binafsi, watumishi wa nyumbani, walinzi, makatibu muhtasi na madereva.

Rais mstaafu atakuwa na watumishi wanne wa nyumbani, wasaidizi binafsi wawili, walinzi wawili, katibu binafsi, madereva wawili kwa ajili ya magari mawili yanayogharamiwa na serikali, huduma za ulinzi binafsi na ofisi binafsi.

Viongozi hao watalipwa gharama za matibabu ndani au nje ya Zanzibar, malipo ya maji, fedha taslimu Sh. 400,000 kila mwezi za posho la simu, kupatiwa pasi ya kusafiria ya hadhi ya kibalozi, na kulipiwa mafuta na matengenezo ya magari.

Viongozi hao wakitakiwa kusafiri nje ya nchi kwa kazi ya kuiwakilisha serikali au kuitikia mwaliko wa kiserikali uliotolewa na taasisi ya kimataifa watalipiwa nauli ya daraja la kwanza kila mmoja akiandamana na mkewe, wasaidizi wake wawili binafsi.

Aidha, itakapokuwa ni safari binafsi, serikali italipa gharama kwa safari zisizozidi nne kwa mwaka ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na safari angalau moja kwa mwaka nje ya Tanzania.

Kwa safari binafsi, sheria inapendekeza rais na makamu wake wawili, walipiwe gharama zitakazojumuisha nauli ya daraja la kwanza kwa viongozi wenyewe, wake zao, watoto wao wa umri usiozidi miaka 18, wasaidizi binafsi na iwapo safari ni za nchini, pamoja na madereva wao kwa safari isiyozidi siku kumi.

Katika mafao yao, viongozi hao watatu pamoja na spika, watalipwa posho inayolingana na mishahara ya miezi 24 waliyolipwa wakati wakitumikia nyadhifa walizoachia kwa kustaafu.

Pia watalipwa kiinua mgongo cha kiwango kinacholingana na asilimia 50 ya mshahara wa juu zaidi waliokuwa wakilipwa kabla ya kustaafu kwa kujumlishwa na kipindi mstaafu alichotumikia nyadhifa husika.

Taarifa zimeeleza kwamba licha ya wajumbe wengi waliochangia kuupinga muswada unaopendekeza mafao hayo, kwa kueleza kuwa unataka kuhalalisha matumizi ya fedha nyingi kwa viongozi wastaafu na familia zao wakati hali za wananchi ni duni kimaisha, serikali imejizatiti kuendelea kuupigia debe.

Wakati wa kujadili muswada huo katika semina, Spika Pandu Ameir Kificho, alisema hata yeye haelewi mantiki ya mapendekezo hayo kwani “maelezo mengi yamefungwafungwa.”

Alisema anashangaa ni mke yupi kati ya watatu alionao atakayelipiwa gharama atakaposafiri au ni mjane yupi kati yao atakayelazimika kulipwa mafao pale atakapokuwa yeye amefariki dunia ndani.

“Sijui watachagua mke yupi. Nikishakufa wataamua kumlipa mjane wangu yupi mmoja. Kusema kweli muswada huu una matatizo na ungerudishwa uandaliwe upya ikiwemo kueleza kwa ufasaha nani alipwe,” alisema Spika Kificho na kuamsha makofi.

Mbarouk Mtando (Mkwajuni) alitaka kwanza waelezwe kwani kwa sasa rais analipwa mshahara kiasi gani ili wafanye hesabu ya kiwango cha mafao atakacholipwa na kuangalia kama kinakwenda na hali ya uchumi ya serikali.

Waziri Dk. Mwinyihaji aligoma kutaja mshahara wa rais akisema mshahara ni suala binafsi ambalo ni siri.

Wawakilishi walitoa sauti ya pamoja na kutaka muswada huo usiwasilishwe barazani kwa sasa, badala yake urudishwe na kuandaliwa upya kwa mwelekeo ambao hautakuja kuzusha malalamiko na chuki kwa wananchi.

Serikali inapendekeza sheria hiyo wakati imeanza kulalamikia wahisani walioahidi kutoa misaada ya bajeti kwa kushindwa kutimiza ahadi zao na hivyo kusababisha itekeleze mipango yake kwa kutegemea mapato ya ndani.

Bajeti ya SUK katika mwaka 2011/12 ni Sh. 613 bilioni ambazo Sh. 340 bilioni zinatarajiwa kutoka misaada ya wahisani.

Serikali inakabiliwa na shutuma za kuwa na utitiri wa viongozi na rais amekuwa akiteua viongozi hata wenye umri mkubwa wakiwemo waliokwishastaafu kazi kwa mujibu wa sheria. Sheria ya utumishi inaelekeza miaka 60 kustaafu kwa hiari na 65 kwa lazima.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi Mohamed ameuita muswada huo kama usio na maslahi kwa taifa na wananchi wa Zanzibar.

“Tungeacha kutunga sheria zenye mwelekeo wa kulenga kikundi cha watu wachache kama vile viongozi wa ngazi za juu serikalini. Hii inaweza kusababisha chuki na uhasama kwa wananchi,” alisema.

“Ajabu kwamba serikali inapanga mafao makubwa kwa viongozi wakuu lakini haifikirii namna ya kuinua maslahi ya wafanyakazi wa kawaida ambao hali zao ni ngumu kimaisha na serikali haijapandisha mishahara ya watumishi wake kwa kisingizio kwamba haina fedha za kutosha. Hizi wanazopangiana wakubwa kulipana zimetoka wapi,” alihoji.

0
No votes yet