Songea Mjini wamkalia kooni Nchimbi


Gideon Mwakanosya's picture

Na Gideon Mwakanosya - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Emmanuel John Nchimbi

JIMBO la Songea Mjini ni miongoni mwa majimbo sita ya uchaguzi yaliyopo katika Mkoa wa Ruvuma. Emmanuel John Nchimbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye mbunge wake.

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika kata za Mshangano, Namanditi, Ruhuwiko, Mletele, Lizaboni na Msamala katika jimbo hili, wanazungumzia namna walivyosahaulika kutatuliwa kero nyingi katika huduma za maji, umeme na afya.

Wananchi mbalimbali wamemweleza mwandishi wa makala hii, kwamba mbunge wao hajatekeleza nyingi ya ahadi alizoahidi wakati wa kampeni. Mmoja wao anayeishi kata ya Mshangano, Samson Komba, anasema tangu Nchimbi alipochaguliwa, amewatembelea mara chache.

Hamza Uonjo, mkazi mwingine, anasema, “Kwa kweli tumechoka huyu mbunge ameshindwa kututatulia kero ya maji, umeme na upungufu wa wahudumu na vifaa katika kituo cha afya cha Mjimwema. Pia hajaitisha mkutano na wananchi tangu achaguliwe.

Mwandishi ameshuhudia upungufu wa wahudumu, dawa, vitandaa na vifaa tiba mbalimbali katika Kituo cha Afya cha Mjimwema. Kituo hicho pia hakina umeme wa uhakika.

Daktari alikutwa akimkadiria mgonjwa homa kulingana na maelezo ya mgonjwa na akapewa dawa bila ya kufanyiwa kipimo chochote. Umeme ilielezwa kuwa ndio tatizo.

Tatizo la maji limepungua kidogo isipokuwa maeneo ya pembezoni mwa jimbo katika kata za Ruhuwiko, Subira, Mletele, Lizaboni, Msamala na Mshangano ambako bado maji ni shida.

Zuhura Hamidu, mkazi wa Mletele, anasema huamka saa 11 alfajiri kwenda kusaka maji yaliyoko umbali wa zaidi ya kilomita mbili. “Hii hali inatuletea adha kubwa kiafya na inatupotezea muda mwingi ambao tungeutumia kwa shughuli za maendeleo.”

Tatizo la umeme jimboni linaelezwa vizuri na mkazi wake, Ally Swai, ambaye ni fundi wa kuchomea, ambaye anasema umeme katika manispaa ya Songea umekuwa ukikatika mara kwa mara.

Upungufu huo unasababisha kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na biashara na hivyo kudhoofisha mapato ya wananchi ambao baadhi yao wanapata hasara kutokana na vitu mbalimbali vinavyotumia umeme kuungua.

Hali kwenye Soko Kuu la mjini Songea inaleta malalamiko. Wachuuzi wanalalamikia kitendo cha baadhi ya madiwani kuhodhi vibanda vya kufanyia biashara na kuvipangisha kwa gharama kubwa.

Mbunge Nchimbi anasema anatambua malalamiko ya wachuuzi na ameelekeza idara husika katika manispaa wafuatilie madai yanayotolewa ili utaratibu uliopangwa ufuatwe na kutendea watu haki.

Kwenye afya anasema hali ni tofauti kuliko aliyoikuta miaka mitatu iliyopita na “jitihada zaidi zinaendelea kwa kuboresha kituo cha afya cha Mjimwema na kujenga vituo vipya kila kata.”

Kuhusu tatizo la maji, Nchimbi anasema upatikanaji wake hauridhishi lakini amejipanga kusaidia kurekebisha kasoro zilizopo na tayari amepata ufadhili kutoka serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la misaada la KFW utakaosaidia kujenga miradi ya maji kwenye maeneo yasiyokuwa na huduma hiyo.

Nchimbi anahitimisha maelezo yake kwa kusihi wapiga kura wake wamvumilie kwani amekuta matatizo mengi jimboni na amekuwa akichukua hatua mbalimbali kuyapatia ufumbuzi. Kimya chake bungeni anasema kisichukuliwe kuwa hatekelezi ahadi zake kwa wapiga kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: