Spika achia kombe lifunuliwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 February 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MBUNGE anaiuliza serikali bungeni: Wale waliochukua fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na wakazirejesha ni akina nani na upi msimamo wa serikali kwa sasa baada ya kitendo cha kuzirejesha fedha walizoiba?

Hakupata jibu. Halikuwepo jibu la swali hilo kwa sababu Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alizuia swali hilo kujibiwa kwa kisingizio kwamba suala la EPA liko mahakamani.

Muulizaji swali kabla ya kuuliza alitangulia kusema hataki kuelezwa kuhusu walioshindwa kurejesha fedha kwa sababu wana kesi mahakamani. Shida yake ni kutaka kufahamu wale waliorejesha fedha serikalini.

Na hili ndilo swali muhimu kwa sasa baada ya serikali kuwa imepeleka mahakamani watuhumiwa wapatao 20 waliohusika na uchotaji wa Sh. 133 bilioni za EPA.

Ni imani yetu kwamba kutokana na umuhimu wa swali hili kwa umma, litaendelea kusubiri majibu tu.

Hata lisipojibiwa mwaka huu na miaka 20 ijayo, litabaki swali muhimu kwa kizazi kijacho. Na wasipopata jibu kwa kuwa wakati huo wanaolifahamu hawatakuwapo, ndipo watasema “wale waliokuwepo walikuwa wajinga wakubwa.”

Tunaamini hawataishia hapo. Wataonyesha hasira zao kwa viongozi waliopaswa kujibu na majibu hayo kubaki kwenye kumbukumbu. Hapo watafinya macho na kuchimbua makaburi ya viongozi.

Watavuta nywele zao na kuwalaani kwa uzembe wao wa kushindwa kulinda raslimali za taifa na matokeo yake kuwaachia wao umasikini.

Kinachojitokeza bungeni ni jitihada za kuharibu mwelekeo mzuri wa serikali kuachiwa wajibu wake wa kujibu hoja yoyote inayotolewa na wabunge.

Vipindi vya maswali na majibu kikiwemo kile kinachompa nafasi Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, vina maana kubwa katika dhana ya kuipa wajibu serikali wa kujiweka wazi.

Tunazungumzia haki ya wananchi kupata habari za vipi serikali yao inaendesha mambo. Hiyo ni haki ya msingi ya binadamu isiyoweza kunyimwa vyovyote vile.

Tunajua yapo masuala yanatafutiwa ufumbuzi kwenye Mahakama, taasisi nyingine ya mhimili wa dola kama ilivyo Bunge na Serikali. Hatuna tatizo hapa kwa sababu ni sehemu ya utekelezaji wa dhana muhimu ya mgawanyo wa madaraka kati ya taasisi hizi tatu.

Ila tunaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakuna uingiliaji wowote wa uhuru wa mahakama kwa serikali kutaja watu waliorejesha fedha za EPA baada ya kuthibitishwa na maodita wa Ernst & Young, kuwa walizichota kifisadi.

Hatutaki kuamini kuwa Spika – baada ya kusifiwa kwa namna anavyojitahidi kuongoza bunge kwa ufanisi – ameamua kujiingiza katika kuminya umma haki ya kupata taarifa.

Wala hatuamini ameanza kujuta na kupigia magoti watu aliopata kusema wanalenga kumhujumu kwa kuona anakwaza mipango yao.

Tunamsihi abaki kwenye kaulimbiu yake: katika uongozi wangu (wa Bunge), nitazingatia KIWANGO na KASI (Standard and Speed). Kila tukiangalia, tunapata moyo wa kuamini umma unamuunga mkono.

Hapo basi, hatutarajii hoja ya kuingilia utaratibu wa mahakama au yoyote ile isiyokuwa na msingi, itumike kuilinda serikali kwani huko itakuwa ni kutaka “kufunika kombe ili mwanaharamu apite.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: