Spika Makinda, kazi kwako!


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Spika wa Bunge, Anne Makinda

FEBRUARI 6, 2008, Spika wa Bunge la 9 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekuwa Spika wa Bunge, Samweli Sitta alitoa dokezo zito kuhusu naibu wake Anne Makinda.

Wakati anatoa taarifa kuwa anatarajia kwenda Marekani, alimwambia Makinda asikurupuke kuongoza mjadala wa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Kauli hiyo, iliwakera wanahabari na asasi za kiraia, wakamkalia kooni Sitta kwa kutumia maneno ya udhalilishaji kwa naibu wake.

Sitta haraka aliomba radhi. Akaeleza anavyoshirikiana naye; wakakumbatiana yakaisha.

Hakuna hata chombo kimoja cha habari, baada ya tukio lile, kilichomfuata Sitta awaume sikio, japo isiandikwe gazetini, alighafilika au ni kweli aliujua udhaifu wa naibu wake?

Miaka mitatu sasa, Makinda akiwa spika kamili, mambo hadharani. Watanzania wanashuhudia kwa macho yao mama huyo anavyofinyanga mijadala tangu mkutano wa kwanza wa Bunge la 10.

Katika mkutano ule uliofanyika Novemba mwaka jana, Makinda, kwa ushawishi wa CCM alipitisha tafsiri mpya ya kambi rasmi ya upinzani ili kuvunja nguvu za CHADEMA, ambacho kwa mujibu wa kanuni, kilifikisha idadi inayostahili kuunda kambi rasmi ya upinzani.

Kaama alivyofanya Februari, Spika Makinda amejitosa wiki mbili zilizopita kumkingia kifua Waziri mkuu, Mizengo Pinda.

Bahati aliyonayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiku (CHADEMA) hakutaka makuu, alipozimwa swali kuhusu mauaji ya watu yaliyofanywa na Polisi, katika mgodi wa North Mara, Nyamongo.

Makinda alikurupuka kumzuia Pinda kujibu swali la Esther kwa madai kuna kesi mahakamani. Mbunge yule hakutaka malumbano, lakini angeweza kusimama na kuomba mwongozo inakuwaje Spika anapolidanganya Bunge?

Esther aliepusha pia aibu kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi.

Makinda angefoka na kumtaka mbunge athibitishe kwa maandishi, na hapo angeadhirika.

Ubabaishaji katika majibu ni sawa na aliofanya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kujibu swali ambalo hakuulizwa kuhusu uvunaji miti katika hifadhi ya msitu wa Myowosi. Mbunge aliomba mwongozo hatua za kuchukua waziri anapojibu swali ambalo hakuulizwa. Makinda amemlinda waziri hadi leo.

Tuache hilo. Makinda alipokuwa anadai kuna kesi mahakamani alilidanganya Bunge. Katika mahakama ya wilaya ya Tarime, hakuna kesi ya polisi kuua watu katika eneo la Nyamongo, kesi iliyopo inahusu watu wanane akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu.

Lissu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, na wenzake wameundiwa mashtaka matatu; kuingia eneo la hospitali bila kibali, kufanya mkutano, na kuzuia watu kufanya kazi. Mahakama ikawapiga marufuku Lisu na wenzake kwenda Nyamongo hadi kesi inayowakabili itakapokwisha.

Walioshtakiwa mbali ya Mbunge Lisu ni Waitara Mwita Mwikwabe, Stanslaus Nyembea, Anderson Deogratias Chacha, Andrew Andalu Nyandu, Mwita Marwa Maswi, Bashiri Abdalllah Selemani na Ibrahimu Juma Kimu.

Esther Matiku si miongoni mwa walioshtakiwa kama Lukuvi alivyolidanganya Bunge. CCM wametengeneza kesi, wanaratibu wao na bado wanadanganya bungeni.

Wakijua kwamba Makinda atapitisha kila wanachotaka, safari hii CCM, wameanza vitimbi vingine kupitia kwa Katibu mkuu, Wilson Mukama kwamba Kamati zote za Kudumu za Bunge zinazoongozwa na wapinzani zirudi katika mikono ya chama tawala. Mukama anafanya hivyo akijua wanaye Makinda.

Makinda akiwa na Sitta walisema mabunge ya Jumuiya ya Madola yanataka baadhi ya kamati hasa za fedha, mashirika ya umma, halmashauri za majiji, mikoa na wilaya ziwe chini ya wapinzani. Vipi Makinda peke yake anatumiwa kuvunja utaratibu huu? Bunge hili litafanana na mabunge ya jumuiya ipi?

Ataweza maana inavyoelekea kazi aliyopewa na CCM ili asinyang’anywe uspika ni kukandamiza kila hoja na kila mtu kutoka upinzani na kulinda kila hoja, kila mtu kutoka CCM. Spika Makinda, kazi kwako!

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: