Spika Sitta ameweka viwango, mwingine nani?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

BUNGE la kwanza la serikali ya Rais Jakaya Kikwete linamaliza muda wake wiki hii na kama kuna nafasi ambayo ilipewa maana mpya na Bunge hilo, basi ni ile ya Spika wa Bunge.

Alipoingia madarakani, Spika wa Bunge, Samwel Sitta, aliwaahidi Watanzania kwamba bunge hilo litakuwa la kasi na viwango. Wachache tulifahamu nini hasa alikusudia.

Leo hii, miaka takribani mitano baada ya ahadi yake hiyo, Sitta anaweza kusimama mbele ya Watanzania na kusema walau yeye alitekeleza majukumu yake.

Niseme mapema hapa, kwamba kusema Sitta alifanya vizuri katika kipindi chake haimaanishi kwamba hakufanya makosa hapa na pale. Yapo aliyoyafanya ambayo sikuridhika nayo, lakini kwa ujumla wake, nafikiri alifanya vema.

Katika kipindi ambacho serikali ililaumiwa kwa mengi yakiwamo matumizi mabaya ya mali ya umma, idara ya mahakama ikilaumiwa kwa kushindwa kuwatia hatiani watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na serikali kwa tuhuma mbalimbali, pengine ni Bunge pekee ambalo wananchi wanaweza kudai limewawakilisha vema.

Na tofauti kubwa katika hili imeletwa na utawala wa Spika Sitta. Yeye ndiye aliyeruhusu mijadala mikali na migumu kwa serikali na chama tawala cha CCM kujadiliwa bungeni.

Katika kipindi cha uspika wa Pius Msekwa, kuna kipindi mijadala ilikuwa mikali pia. Lakini sote tunajua namna ilivyokuwa ikiuliwa ‘kiaina’ na kiongozi huyo mwenyewe au kupitia vikao vya chama.

Ndiyo maana nampongeza Sitta kwa kuruhusu mijadala mizito kama ule wa Richmond ndani ya Bunge. Ule ulikuwa ufunguo wa mijadala mingine mikubwa kujadiliwa bungeni.

Jambo la msingi hapa ni kujiuliza ni kwa vipi kile alichokianzisha Sitta kinaweza kuendelezwa na yeyote atakayefuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu? Je, atakuwa Sitta mwenyewe?

Hata hivyo, kwa upande wangu, Bunge hili lilikuwa na mapungufu mawili makubwa ambayo kwa kiasi fulani yalizorotesha ufanisi wake.

Kwanza ni ule ukweli kwamba Sitta, kwa mujibu wa taratibu za CCM, pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na alikuwa akishiriki vikao vingine muhimu vya chama hicho.

Kuna baadhi ya maamuzi yake yalikuwa yakizua maswali mengi. Kwa mfano, kuna lile la kuruhusu kufungiwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto.

Sitta alikubali hilo kutokana na presha kutoka ndani ya wabunge wa chama kilichompa nafasi hiyo. Kama asingekuwa mwana CCM, pengine Zitto asingefungiwa.

Ninakumbuka pia namna spika huyu alivyokuwa akiandamwa ndani ya chama chake, kiasi cha kutishiwa kuvuliwa uspika wenyewe kwa vile aliwaumiza watu wa chama chake.

Matukio haya yameonyesha, pamoja na mambo mengine, haja ya kuwa na mfumo wa Bunge ambao spika wa Bunge hawi kiongozi wa chama chochote cha siasa. Anakuwa mtu huru na anafanya mambo kwa maslahi ya taifa na si chama chake.

Hili linawezekana. Nchini Kenya, kwa mfano, Spika wa Bunge la nchi hiyo, Kenneth Marende, alikuwa mwanachama wa chama cha ODM wakati wa uchaguzi. Baada ya kushinda ubunge na kupata uspika, alijivua ubunge na uanachama wa chama chake na sasa hana chama.

Kuna namna mbili ya kulishughulikia suala kama hili. Kuna kufanya kama wanavyofanya Kenya ambapo mtu anayewania uspika, lazima awe mwanasiasa lakini anauweka pembeni unazi wake na kuitumika nchi.

Njia ya pili ni ile ya kutafuta mtu anayeheshimika kwenye jamii na kumpa nafasi hiyo. Mtu huyo anaweza kuwa msomi wa hadhi ya pengine Prof. Issa Shivji, ambaye ataishika nafasi hiyo kwa sababu ya heshima yake mbele ya jamii.

Ninaamini, mtu kama huyu atafanya kila awezalo kuhakikisha bunge linakuwa na makali zaidi kuliko hili la sasa. Ataruhusu mijadala yenye tija kwa taifa bila ya hofu ya kuwekwa kiti moto huko mbele ya safari.

Ningependa mabadiliko haya yafanyike katika bunge lijalo ili kuisaidia nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kuongeza mijadala yenye siha kwa taifa letu.

Jambo lingine ambalo ningependa lifanyike katika bunge lijalo ni kuondoa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu na badala yake Bunge lipewe uwezo wa kuwahoji watu watakaokuwa wakiteuliwa na rais kushika nyadhifa kubwa serikalini.

Ingawa kipindi cha maswali kwa waziri mkuu ni kizuri, lakini kimepoteza maana kwa vile waziri mkuu wa Tanzania si mkuu wa serikali na hivyo kuna maswali mengi ambayo hayawezi kuyajibu kwa vile yeye hana mamlaka ya mwisho.

Utaratibu huu unafaa tu katika nchi zenye mfumo ambao Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa serikali kwa mfano Uingereza na India. Kwa hapa kwetu, kipindi kile huwa kinamtesa tu waziri mkuu.

Kuna umuhimu mkubwa kwa bunge kuthibitisha uteuzi wa watu kama Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Gavana wa Benki Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mkuu na viongozi wengine ambao nyadhifa zao zinagusa walio wengi.

Bunge litafanya kazi ya kuchunguza tuhuma dhidi ya aliyeteuliwa (kama zipo) na kuhakikisha nchi inapata viongozi wenye sifa zinazostahili na wasio na madoa katika maisha yao.

Sote tuna madoa katika maisha yetu. Lakini kumteua mtu ambaye amewahi kushitakiwa kwa kukwepa kulipa kodi kuwa waziri wa fedha ni tatizo kubwa. Sawa na kumpa mtu nafasi ya ugavana wakati historia yake inaonyesha ameua mashirika karibu matano kwa utendaji wake mbovu katika siku za nyuma.

Huku ndiko kusogea mbele ninakokuhitaji katika bunge lijalo. Najua wapo wenzangu wenye mawazo mengine katika kuimarisha bunge lijalo na tukaribishe pia mawazo yao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: