Steven Wassira anatumikia mtandao, si serikali


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
STEVEN Wassira

STEVEN Wassira ni waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano  na Uratibu katika jamii. Yasemekana lengo kuu la wizara hii ni kushughulikia mahusiano katika jamii na kuhakikisha migogoro inadhibitiwa kabla haijatokea.

Lakini sasa tunamwona Wassira akichochea migogoro, badala ya kuitatua. Kwa wazalendo wanaolifahamu taifa hili na historia yake, wanashangaa kuona serikali na chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakosa msemaji na mtetezi kiasi cha kumbeba Wassira na kumfanya kuwa ndiye msemaji na mtetezi wake.

Historia inamhukumu Wassira kuwa yeye si mpenzi wa CCM, bali ni mpenzi wa watu fulani ndani ya chama. Anapokosana na watu, huhama chama na akipatana na wengine hurejea katika chama. Hajawahi kuonyesha kuwa anatumika kwa manufaa ya umma unaodaiwa kumchagua.

Ndiyo maana baada ya kurejea ndani ya CCM, akitokea NCCR-Mageuzi, alikaa kijiweni kwanza na ndipo kundi la mtandao lilipomwendea na kumpa wajibu maalum.

Wassira yuko kwenye rekodi ya kudhalilisha watu wenye heshima mbele ya jamii; kila wiki kwa kuandika makala za kukashifu wenzake ndani ya chama. Ilifika wakati mwanamtandao asilia Rostam Aziz alikuwa anamwandikia cha kusema na Wassira kwa uadilifu mkubwa alifanya kazi hiyo.

Bado nina makala kadhaa za Wassira alizoandikia gazeti la Rai, na kila ninapozisoma siamini macho yangu kuwa huyu naye yumo ndani ya serikali yetu ya sasa.

Kwa CCM na serikali kumtumia Wassira, mambo mawili yanatokea. Kwanza, taswira ya CCM na serikali mbele ya jamii inatiliwa shaka na kila mtu makini, wakiwamo marais wastaafu. Naelewa kuwa hili linaweza kupuuzwa na viongozi wa serikali ya sasa, lakini wanafanya hivyo kwa hasara yao wenyewe na si hasara ya marais na wazee hawa.

Ndani ya serikali, Wassira sasa ndiye tegemeo la kuisemea mbele ya jamii. Manunguniko yameenea ndani ya serikali kuwa Wassira anaiobomoa serikali anayodai kuijenga na kuitetea. Kuna madai pia kuwa anautumikia mtandao wa mafisadi ili uiangushe serikali.

Baada ya malalamiko ya muda mrefu ndani ya serikali na vikao vya CCM, mtandao asilia ulionekana kusambaratika kabla haujaanza kujipanga upya. Hivi sasa mtandao huo una makundi matatu na Steven Wassira anatumikia kundi mojawapo, lakini si la Rais Jakaya Kikwete aliyemteua.

Kwa hali hiyo, kelele za Wassira juu ya maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) si kutetea serikali ya Kikwete, bali kujaribu kuzuia maandamano hayo yasimshawishi Kikwete kushughulikia baadhi ya kero zinazopigiwa kelele na CHADEMA.

Hoja za CHADEMA zinatishia maslahi ya mtandao asilia unaoongozwa na Rostam Aziz na Steven Wassira amewahi kutamka hadharani kuwa mpaka sasa haoni tatizo la Rostam. Iwe Richmond, Dowans, mfumuko wa bei, Kagoda, Import Support, na kashfa nyingine nyingi zinazopigiwa kelele katika maandamano ya CHADEMA, zinamhusu zaidi Rostam Aziz kuliko zinavyokihusu CCM na serikali yake.

Makada wanaoheshimika ndani ya CCM kama John Malecela wamewahi kutamka hadharani kuwa CCM kama chama si fisadi, bali ufisadi ni tabia ya mtu binafsi na ashughulikiwe mhusika binafsi.

Ikiwa CCM na serikali yake wanaamini hivyo, kuna haja gani ya Wassira kupoteza muda wake kupambana na CHADEMA inayoandamana kupinga ufisadi wa mtu binafsi?

Na ikiwa ufisadi ni tabia na hulka ya CCM na serikali yake, bado Wassira hana sababu ya kupambana na CHADEMA inayopinga ufisadi iwe ni kwa mawe, hoja au hata nguvu ya umma.

Hii ni kwa sababu, badala ya kutumia misuli kupambana na CHADEMA, CCM na serikali wangetumia maandamano kueleza jinsi wasivyo mafisadi au wangewataka CHADEMA wathibitishe madai yao pasipo kuwatishia kutumia nguvu ya dola.

Kwangu mimi, ni hesabu za kutazamia kwa waziri mwenye kuifahamu kazi yake, kuthubutu hata kufikiria kutumia nguvu ya dola kupambana na nguvu ya umma. Historia inaeleza hakuna nguvu ya dola iliyowahi kuishinda nguvu ya umma.

Ikiwa ni kweli kuwa serikali ya CCM imeishiwa uvumilivu kama alivyosema Wassira, na kwamba ina mpango wa kutumia nguvu ya dola kuzima nguvu ya umma, napenda niwe mtabiri badala ya kuwa mnajimu kwamba: Hii ni njama ya Wassira na mafisadi wa mtandao asilia, wanaojaribu kuiyumbisha serikali ya Kikwete kwa kutumia mgongo wa CHADEMA.

Hili la kupambana na CHADEMA kwa nguvu ya dola, ni mojawapo ya masuala yanayoweza kuidhalilisha serikali ya Kikwete endapo itakubaliana na mtizamo wa watu kama Wassira.

Ni jambo lililo wazi kuwa kwa CCM na serikali kushindwa kuwashughulikia mafisadi ndani yake, ndicho chanzo cha minyukano na makundi ndani ya chama chenyewe na ndiyo kichocheo cha wananchi kuipenda CHADEMA.

CHADEMA hawana fedha za kuhonga watu ili waende kwenye maandamano yao, hawatumii vitisho wala vikundi vya sanaa kuwavuta wananchi. Safari hii hata kisingizio cha helikopta hakipo na bado watu wengi wanajitokeza kwa wingi katika mikutano yao. Inahitajika hekima kulieleza hili mbele ya vyombo vya dola vinavyoandaliwa kutumiwa ili kuwadhibiti CHADEMA.

Kutokana na kuenea kwa ushawishi wa haki za binadamu katika jamii, Wassira na wenzake inabidi wawe macho na matumizi ya dola kugandamiza nguvu ya umma.

Hii ni kwa sababu maaskari wengi wa siku hizi wamesoma na wanajua kuwa kutii amri inayovunja haki za binadamu si kinga kwa askari kukamatwa na kushtakiwa baadaye kwa makosa ya uvunjaji wa haki za binadamu.

Ikifikia hatua hiyo, CCM haiwezi kutumika kumuondolea hatia askari huyo. Kwa mtazamo wa kihafidhina, haya yatakuwa maasi ya vyombo vya dola dhidi ya serikali halali, lakini kimsingi huo utakuwa ni mwanzo wa ukombozi kwa wananchi.

Kwamba iwe ni mwiko wa chombo cha dola kutumia raslimali na kodi za wananchi, kuwakandamiza wananchi wenyewe ambao ndio msingi wa utawala wowote ulio halali.

Steven Wassira katika mambo mengi aliyoapa kufanya akiwa waziri, ni kumshauri rais bila woga wala huruma. Namshauri aifanye kazi hiyo kwa umakini. Asipoteza muda kuwashauri wananchi badala ya rais na chama chake.

Kwa macho yangu nimemshuhudia Wassira akipingwa na mawaziri wenzake hadharani kwa misimamo yake hii inayochochea machafuko badala ya amani. Naamini hali ni hiyohiyo hata ndani ya chama chake kwa sababu wapo wana-CCM makini ambao wako tayari kupambana na CHADEMA kwa hoja, badala ya nguvu ya dola.

Kumshauri rais kutumia nguvu ya dola dhidi ya wananchi ni kashfa itoshayo kumfanya rais amfukuze kazi Wassira. Lakini kwa kuwa utamaduni huu umekufa na kuzikwa katika awamu ya nne, hilo haliwezi kutokea.

Matumizi ya nguvu ya dola dhidi ya chama halali chenye wafuasi wengi wanaodai haki itendeke ili kupunguza makali ya maisha, ni hatua ya mwisho kabisa ya chama na serikali iliyochoka kutawala.

Wananchi hawahawa ambao Wassira anashawishi wapigwe na nguvu ya dola, ndio haohao ambao anadai miezi mitatu tu iliyopita walipiga kura na kuichagua CCM kwa kura nyingi. Sasa inakuwaje, wananchi haohao, wanaandamana dhidi ya serikali hiyo?

Wassira asipodhibitiwa, kuna hatari ya kutoboa hata siri kubwa zaidi juu ya uchaguzi huu uliopita ambao sasa tunashuhudia serikali inayosema ilishinda kihalali, inaanza kubabaika bila hoja za maana.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: