Stori, uzandiki msibani


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MSIBA wa watani ni burudani. Katikati ya masikitiko na majonzi kwa wafiwa, kwa watani ni vicheko, stori na vituko.

Baadhi wataigiza utembeaji, uzungumzaji na hata tabia aliyokuwa nayo marehemu, na wengine watatumia fursa hiyo kutoboa siri.

Watani ni washereheshaji; kazi yao kupiga stori. Kwa hiyo, wakati kule ndugu na jamaa watakuwa wanalia, huku watani watafurahisha na kuchekesha kwa stori.

Juzi, mtani mmoja kutoka Chama Cha Magamba alifika katika msiba wa M4C na stori ya watu watatu – Mtasha, Mmanga na Mswahili – ambao eti walipakiwa kwenye ndege na wakapewa mtihani wa kutambua, wakiwa angani, maeneo watakayopitishwa.

Safari ikaanza wakazungushwa saa kadhaa kisha wakaambiwa watoe mikono.

“Hahahahaha,” alicheka Mtasha. Akasema, “tupo New York, napapasa skyscrapers (maghorofa). Alipoulizwa mpango wa baadaye, Mtasha alisema sirikali ya Barack Obama itajenga majengo marefu zaidi.

Wakaendelea na safari; wakaambiwa watoe nje mikono na waeleze waliko. Mmanga alijibu haraka akisema wako Kuwait na kilichomjulisha ni unyevunyevu wa mikono uliotokana na mafuta.

Alipoulizwa mipango ya baadaye, akasema sirikali ya Mfalme Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah itachimba visima zaidi vya mafuta.

Wakaondoka. Baada ya saa mbili wakaambiwa watoe tena mikono na waeleze waliko. Ghafla Mswahili akajibu, “Tuko Bongo.” Alipoulizwa amejuaje akajibu, “Si mnaona, nimeibiwa pesa!”

Alipoulizwa atachukua hatua gani, akadai atamwomba rais awaite wezi ikulu ili warudishe.

Tuliangua kicheko kwa stori hiyo na kusababisha watu kutunyamazisha kwa sauti za “shiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii”.

Tulinyamaza, lakini kila vijana walipoitafsiri stori ile waliendelea kucheka chini chini hekima ya Mswahili kumbeleza wezi warejeshe walichoiba.

“Shishishi,” tulinyamazishwa tena ili tumsikilize mtani mwingine kutoka Chama Cha Magamba akitoa salamu za rambirambi.

Mara waliposema kuwa Bob Willy Soni Mukamia atatoa salamu za chama, waombolezaji wakainamisha chini vichwa wakihofu ataropo tu.

Hofu ya magamba ilikuwa dhahiri, kwani alipoanza kusema “…ndugu wafiwa, natoa salamu kwa niaba ya magamba, poleni sana,” akaanza bashasha.

“Tunajua huyu alikuwa katibu mkuu wa M4C, alikuwa mtu shupavu, katibu mkuu asiyependa kuongea wala kuhubiri ‘kama mke aliyepoteza mume’ au ‘familia iliyopoteza baba.’

Kama vile kuna watu walikuwa wanamchagiza “sema baba sema,” Mukamia aliinua uso wake akatazama watu kisha akatoa mpasho “alikuwa mwadilifu ikilinganishwa na viongozi wa sasa. ”

Mtani huyo akaendelea kudai eti kati ya viongozi tisa walioasisi chama hicho yeye pekee ndiye alikuwa katibu mkuu wa kwanza aliyetoka nje ya kanda ya kaskazini. Chama Cha Magamba mtendaji mkuu choka mbaya.

Huyu katibu anasumbuliwa na mambo mawili; kwanza anahubiri ukabila na udini, pili anajifanya profesa wa mambo yasiyomhusu.

Bwana huyu alipopewa kazi ya kuangalia kwa nini wameota magamba kiasi cha kuzomewa kila kona huku watani wao M4C wanavutia makundi ya watu, aliona hiyo ilikuwa fursa ya kupiga fitina.

Akapeleka Neki wazo la kuvuana magamba, huku chini chini akijipigia debe awe mtendaji mkuu. Kwa bahati mbaya, wajumbe choka mbaya hawakujiuliza mara mbili mantiki yake, wakamtimua Mzee Kambakamba akapewa kazi yeye.

Mwaka jana katika kikao na waandishi wa habari jamaa huyu alidai IMF ilitoa fedha za kuanzisha M4C. Juzi msibani akachakachua historia ya waasisi.

Kama ujenzi wa chama unategemea hila, uongo, fitina, uzandiki, porojo, propaganda, umbeya, unafiki, kejeli, dharau na upotoshaji Chama Cha Magamba hakiwezi kusalimika.

0658 383 979
0
No votes yet