SUMATRA futeni mpango utakaoumiza Watanzania


Nicoline John's picture

Na Nicoline John - Imechapwa 17 February 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) inataka wawekezaji wageni ndio waendeshe huduma ya usafirishaji abiria ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Mamlaka hiyo inapanga kukaribisha makampuni ya wenye fedha yalete mabasi yapatayo 600 ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.

Mpango huu ukitekelezwa, maana yake ni kukatisha kipato cha maelfu ya wananchi wanaoendesha maisha ya kila siku kwa kutegemea biashara ya usafirishaji abiria katika jiji lenye wakazi wapatao milioni saba.

Ninajiuliza ni vipi kama Sumatra ingetoa mapendekezo ya aina ya mabasi inayotaka yasafirishe abiria Dar es Salaam na ikaruhusu wenyeji kuingia katika mpango huu?

Ningeuona mpango wa Sumatra una uhalali iwapo kusingekuwa na mjasiriamali mzalendo aliyejitokeza kuendesha biashara hiyo.

Hapo mtu angesema “ni sawa” kwani huduma ya usafiri ni jambo muhimu na kama hakuna Mtanzania aliyejitokeza kuwekeza kwa kununua basi la kisasa la kiwango ambacho Sumatra wanataka, waruhusiwe wawekezaji wakubwa kutoka nje.

Lazima kufafanua kwamba kulingana na tangazo la Sumatra, wanatafuta wawekezaji wa kigeni walete mabasi ya kisasa ya kuhudumia wasafiri katika jiji la Dar es Salaam. Hapa wawekezaji wazalendo wamepigwa panga.

Tunaelekea wapi Watanzania kutaka kila huduma iendeshwe na wawekezaji kutoka nje? Ni lini walio katika mamlaka za utendaji wataona umuhimu na haki kwa Watanzania kuendesha mambo yao?

Kutoa huduma ya usafiri ni shughuli ya kiuchumi ambayo inaweza kufanywa na wenyeji. Ni uamuzi usio na tija kwa nchi kuwanyima haki Watanzania kutoa huduma hiyo. Huku ndiko kuwapa Watanzania maisha bora au kuwakatisha maisha?

Maisha bora yatapatikana vipi wakati watendaji wa serikali na taasisi zake bado wanaamini ni wageni tu wenye uwezo wa kuhudumia Watanzania?

Hakuna anayebisha kwamba wapo wananchi wenye uwezo wa kununua mabasi ya kisasa; kama si matatu basi angalau moja. Lakini wapo waliojikusanya katika SACCOS wakiwezeshwa wanaweza kumiliki mabasi ya kubeba abiria.

Vinginevyo, nataka kuamini kwamba mpango wa Sumatra hauna nia njema na wananchi wa kipato cha chini na kati ambao maisha yao yamekuwa yakitegemea shughuli hiyo.

Badala yake, ninachokiona ni watendaji wakuu wa Sumatra na mawakala wake kujitafutia ulaji kupitia zabuni watakazoitisha ili kupata makampuni makubwa ya kuleta mabasi ya kisasa. Hapo ni rushwa tu itafanya kazi.

Inawezekana ikawa ni kiini macho tu ili wajanja wajipenyeze na kuleta watu wanaowahitaji kwa kutegemea asilimia fulani kama ilivyozoeleka.

Sumatra na serikali wamejiuliza itakavyokuwa hatima ya maelfu ya Watanzania watakaopoteza kipato kutokana na kutolewa katika shughuli ya kusafirisha abiria Dar es Salaam?

Wanawafikiriaje watu hawa waliojiajiri baada ya kunyang’anywa ajira zao? Watakwenda wapi? Vipi watahudumia familia zao?

Tayari baadhi ya makampuni yanayomilikiwa na wageni yanasafirisha abiria wanaokwenda mikoani kutoka kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo. Sasa wakubwa wanataka abiria ndani ya Dar es Salaam nao wasafirishwe na wageni.

Si kila biashara inayotokea nchini ni lazima ifanywe na wageni. Fursa waliyopewa wageni ya kusafirisha abiria waendao mikoani inatosha. Mengine waachiwe Watanzania kushughulikia kwa kushirikiana na vyama vya wadau wa usafirishaji.

Hii ndio fursa nzuri ya kuwajenga Watanzania kiuchumi kwa kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika kutoa huduma hii ya usafirishaji abiria.

0
No votes yet