Sumaye agoma kumchafua Slaa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameingia katika kampeni za mgombea urais wa chama chake kwa sharti la kutomchafua Dk. Willibrod Slaa.

Taarifa zilizofikia gazeti hili kutoka Moshi zinamnukuu Sumaye akisema, hatamchafua mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa vile kufanya hivyo kutamvunjia hadhi.

Sumaye ameingia kwenye kampeni kufuatia mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, kuwaomba msaada viongozi wastaafu wanaodaiwa “kukacha” kampeni zake.

“Naweza kukuthibitishia pasipo shaka kwamba, Kikwete amewaangukia baadhi ya wazee wetu kumsaidia katika mikoa ambako CCM ina “hali mbaya.” ameeleza mtoa taarifa.

Chanzo hicho cha habari kimesema, awali ilionekana Kikwete angeweza kushinda bila msaada wa wastaafu, lakini sasa ameoana upepo umegeuka.

Taarifa zinasema Kikwete alimwomba Sumaye kumsaidia hasa katika mikoa ya kanda ya Kaskazini ambako imeelezwa kuna upinzani mkubwa.

“Awali, Sumaye alisita kukubali ombi hilo la rais, lakini baadaye akakubali kwa kutoa masharti ya mahalai hasa anapoweza kwenda,” kimeeleza chanzo cha habari.

Hata hivyo, alimwambia Kikwete kwamba atakwenda tu katika maeneo ambayo anadhani anaweza kutoa msaada mzuri,” kimeeleza chanzo hicho.

Ofisa mmoja wa ofisi ndogo ya makao makuu, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam ameliambia gazeti hili kuwa awali Sumaye alielekezwa kwenda majimbo ya Moshi Mjini, Hai, Rombo, Moshi Vijijini na Vunjo.

MwanaHALISI lina taarifa kuwa Sumaye amekataa kufanya kampeni katika majimbo hayo, kwa maelezo kwamba anaamini wagombea ubunge wa CHADEMA huko “hawana matatizo.”

Haikufafanuliwa iwapo kwa “hawana matatizo,” Sumaye alikuwa na maana ya kusema hawashikiki au wana uwezo wa kuwakilisha majimbo yao.

Philemon Ndesamburo anapigania kiti chake Moshi Mjini wakati Freeman Mbowe anagombea Hai.

Kuna taarifa kwamba ilibidi Sumaye awasiliane na Kikwete moja kwa moja kumweleza uamuzi wake huo. Imeripotiwa kuwa Kikwete amekubaliana naye.

Taarifa zilizopatikana juzi Jumatatu zimesema Sumaye amekubali kufanya kampeni katika majimbo ya Vunjo na Hanang.

Aidha, imefahamika kuwa Sumaye amekubali kuingia kwenye kampeni kwa sharti la kutoshiriki kumkashifu mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, jambo ambali amenukuliwa akisema linaweza kumwondolea hadhi.

Taarifa zaidi zimesema Sumaye amegoma kumfanyia kampeni mgombea ubunge wa jimbo la Rombo kupitia CCM, Basil Mramba, kwa vile ana wasiwasi ataonekana ni mtetezi wa watuhumiwa wa ufisadi na anaweza kuanza kuandamwa baadaye.

Msimamo huo wa Sumaye unalingana na kauli yake ya Jumapili iliyopita alipowataka wananchi kutowachagua mafisadi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza katika sherehe ya kumweka wakfu Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Pare ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mkoani Kilimanjaro, Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi alisema, mgombea anayetoa rushwa asichaguliwe, “hata kama ni wa chama chako.”

Sumaye alisema wanaowapa wanasiasa fedha wanazotumia kutoa rushwa, ndio wanaoamua wanasiasa hao wafanye nini baada ya kuchaguliwa.

Kauli ya waziri mkuu huyo wa zamani ni nadra sana katika hotuba za wanasiasa na viongozi wengi wa CCM.

Wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Sumaye akiwa amekabwa na wana mtandao kwa tuhuma mbalimbali kupitia magazetini alisema, wanaotafuta kwenda ikulu kwa kalam, wakifika huko watatumia risasi kusafisha njia.

Sumaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka kumi mfululizo wakati wa serikali ya Benjamin Mkapa.

Gazeti la Tanzania Leo, wakati huo likiwa chini ya uhariri wa Muhingo Rweyemamu, mwana mtandao na Ofisa Habari wa Kampeni ya Kikwete ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa kampuni ya New Habari (2006) ya Rostam Aziz, ndilo lilieneza madaai ya Sumaye kuwa tajiri kupindukia.

Gazeti liliandika kuwa Sumaye ana mabilioni ya shilingi katika akaunti za nje ya nchi. Ilithibitika baadaye kuwa habari hiyo haikuwa kweli.

Tarehe 29 mwezi uliopita, MwanaHALISI lilichapa habari iliyosema kuna madai ya baadhi ya viongozi wakuu wastaafu wa CCM na serikali “kukacha” kampeni za Kikwete kwa sababu mbalimbali.

Viongozi hao ni rais mstaafu Benjamin Mkapa na makamu mwenyekiti mstaafu, John Samwel Malecela.

Wengine wanaodaiwa kukacha kampeni ni rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba na katibu mkuu mstaafu CCM, Philip Mangula.

Taarifa kutoka ndani ya CCM zinasema, uamuzi wa viongozi hao wastaafu unatokana na kile walichoita “Kikwete kuwa kichwa ngumu.”

Hata hivyo, kuna taarifa kwamba wastaafu wengine bado wanachumbiwa kujiunga na kampeni hasa baada ya kuona mporomoko katika kura za maoni za baadhi ya asasi za utafiti – REDET na Synovet.

Kwa mujibu wa taarifa za walio karibu na viongozi wastaafu, hatua hiyo imefuatia Kikwete kushindwa kutekeleza ushauri mbalimbali wa chama na viongozi hao.

Moja ya mambo yanayotajwa kutofurahisha wastaafu ni pamoja na serikali ya Kikwete kushindwa kupeleka bungeni muswada wa sheria ya “kutenganisha biashara na siasa” kabla ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Tangu mapema baada ya kuingia madarakani, Kikwete aliahidi kurejesha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na hasa maadili ya uongozi kwa jumla, katika serikali na chama chake kwa njia ya kutenganisha siasa na biashara.

Pamoja na ahadi hizo, Kikwete hakutekeleza. Jingine ambalo linatajwa kutofurahisha wastaafu ni hatua yake ya kuhamishia kampeni za uchaguzi katika familia yake.

Sababu nyingine ambayo inadaiwa kuwakoroga wastaafu ni Kikwete kuendelea kumkumbatia Yusuf Makamba katika nafasi yake ya katibu mkuu.

Taarifa zinasema viongozi wastaafu walimtaka Kikwete kumwondoa Makamba katika wadhifa wake kwa maelezo kwamba hana uwezo wa kusimamia chama wakati huu wa uchaguzi.

Makamba amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wanachama, wabunge na wajumbe wa NEC, kwamba “anavuruga chama” na anatenda kinyume na maagizo ya vikao vya chama.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: