Sumaye aliifukuza Richmond


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 November 2009

Printer-friendly version
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alimfukuza ofisini kwake Mohamed Gire, anayedaiwa kuwa ni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Richmond Development Company (LLC), baada ya kutilia shaka uwezo wake kama mwekezaji mwaka 2001, imefahamika.

Taarifa za kuaminika kutoka watu walio karibu na Sumaye zimesema kuwa kiongozi huyo alifanya hivyo baada ya kuthibitishiwa na wasaidizi wake kuhusu ubabaishaji wa Gire, alipotaka kuruhusiwa kuwekeza nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ambazo Sumaye amekataa kuzijadili sasa, baada ya kupokea maombi ya matarajio ya Gire kiuwekezaji nchini, aliagiza mmoja wa wasaidizi wake, Dk. Enos Bukuku, afuatilie kwa kufanya uchunguzi wa historia ya utendaji wa Gire.

Uchunguzi wa Dk. Bukuku ulibaini kuwa Gire hakutambuliwa kama ni mwekezaji makini kutokana na taarifa zilizopatikana.

Gazeti hili limefahamishwa kuwa hakukupatikana kumbukumbu ambazo zingeiwezesha serikali, chini ya Rais Benjamin Mkapa, kumuidhinisha Gire kama mwekezaji na hatimaye kumpa kibali cha uwekezaji nchini.

Gire alianza mawasiliano na serikali ya Tanzania mwaka 2001 alipotaka kibali cha kuwekeza katika mradi mkubwa wa kutandika bomba la kusafirishia mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, lakini alinyimwa ruhusa.

Mawasiliano hayo yalipitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wakati huo kikiongozwa na Samwel Sitta, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIC.

Taarifa za mawasiliano ya serikali na Gire zimegusia pia namna alivyokutana na Sumaye wakati waziri mkuu huyo alipofanya ziara ya kikazi nchini Marekani na kuonana na Watanzania walioko Marekani katika jiji la Houston.

Watu waliokuwa karibu na Sumaye, wamesema Sumaye alipata maelezo yanayomhusu Gire lakini hakuwahi kukutana naye hadi alipoenda Marekani na kukutanishwa na kundi la Watanzania kwa majadiliano ya kawaida.

Msaidizi mmoja aliyekataa kutambulishwa jina gazetini amesema, “huyu bwana alikuwa katika kundi la Watanzania waliokutana na waziri mkuu lakini hakuwa karibu hivyo. Wala si Gire aliyeandaa chakula kwa ajili ya waziri mkuu na ujumbe wake.”

Juhudi za kuwasiliana na Dk. Bukuku aliyetumwa na Sumaye kufuatilia umakini wa Gire, hazikuzaa matunda. Mara kadhaa hakupokea simu alizopigiwa na gazeti hili. Baadaye alituma ujumbe wa maandishi akitaka aelezwe anachoitiwa kwa njia hiyo hiyo ya ujumbe mfupi wa maandishi.

Aliandikiwa ujumbe wa kumfahamisha kinachotakiwa na kuombwa atoe ushirikiano kwa kujibu ili kusaidia kujulikana ukweli wa suala hilo. Hakupiga simu wala kutuma majibu kwa njia ya ujumbe mfupi. Alipopigiwa tena na tena alikuwa akipokea na kukata simu papo hapo.

Gire aliruhusiwa kuwekeza nchini mwaka 2006 pale alipopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura kupitia kampuni yake ya Richmond Development Corporation (RDC) katika mkataba tata uliozusha kashfa nzito kwa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.

Richmond ilishindwa kutekeleza mkataba huo na ikarithisha kazi kwa Dowans, kampuni nyingine iliyoonekana kama “chanda na pete” na Richmond kwa vile kampuni hizo zilibainika kushirikiana katika baadhi ya hatua za kibiashara.

Hadi leo sakata la mkataba wa Richmond linaendelea kuihangaisha serikali ya Rais Kikwete licha ya kusababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Bado serikali inasubiriwa kuwasilisha bungeni taarifa yake ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge ambalo lilitaka serikali iwawajibishe wote waliohusika katika mchakato wa kifisadi wa mkataba wa Richmond.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: