Sumaye apembua UV-CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Asema wametumwa kuua chama
WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema hakuna wa kumzuia kugombea urais, iwapo ataamua kufanya hivyo na kwamba rais ajaye aweza kutoka popote katika Jamhuri ya Muungano.

Sumaye alikuwa akijibu kile alichoita, “matamshi ya hovyo” yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wakuu wa chama chake – katibu mkuu Yusuf Makamba, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC), William Lukuvi na viongozi wa umoja wa vijana wa chama chake (UV-CCM).

Kauli ya Sumaye imefuatia UV-CCM mkoani Pwani na taifa, kumtuhumu kutafuta urais pale aliposema kuwa hoja zinazotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), zijibiwe na CCM na siyo kuacha jukumu hilo kwa serikali.

Sumaye alitaka chama chake kuacha kulalamika; badala yake kufanya kazi za kisiasa katika kukabiliana na CHADEMA ambayo leo hii imeonyesha kukubalika kwa wananchi hata kuliko ilivyokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Hata hivyo, vijana wamesema, Sumaye amechelewa kwani suala la urais wa 2015, lipo mikononi mwa mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete” na kwamba hatatoka Kaskazini mwa nchi.

Akijibu hoja hiyo, 25 Machi 2011, Sumaye aliwaambia waandishi wa habari, “Tumekuwa tukimchagua rais kutegemea uwezo wake; hatujawahi kuchagua rais kutokana na eneo analotoka, kabila lake, dini yake wala jinsi yake.”

Amesema, “Kusema rais ajaye hatatoka Kaskazini, ni ubaguzi na ni hatari kwa mustakabali wa taifa. Rais ajaye atatoka hata Bagamoyo.” Akiongea kwa kujiamini Sumaye alisema, “Mwaka 2015 akitokea mtu mwenye sifa za urais, lakini amezaliwa Bagamoyo, asichaguliwe kwa kuwa ndiko anakotoka rais wa sasa, Jakaya Kikwete? Hii si sahihi,”

Amesema Rais Kikwete hatoki Kaskazini. Mtangulizi wake, Benjamin Mkapa hakutokea Kaskazini na wala Rais Ali Hassani Mwinyi hakutokea Kaskazini. “Naye Mwalimu Nyerere alitokea Musoma, sijui kama wanaiita na yenyewe ni Kaskazini,” alisema huku waandishi wakiangua kicheko.

“Hakuna kiongozi yoyote atakayeweza kuongoza nchi hii kwa misingi ya ubaguzi. Uwe ubaguzi wa eneo, kabila, dini, rangi, wala jinsia. Alisema ukishauweka utaratibu wa ubaguzi, basi uongozi umekushinda,” amesema.

Sumaye amesema mbali na kujaa matusi na kejeli, maudhui ya kauli za vijana yanatisha, hasa ukilinganisha kauli ya awali kuwa rais ajae amefahamika tayari.

Hii maana yake ni kuwa “…hao vijana wanaye mgombea wao ambaye wanampigania, siyo kwa sababu ana uwezo wa kuongoza nchi, bali ili iwe zamu yao ya kula,” Sumaye aliwaambia waandishi kwa sauti ya mshangao.

“Kumbe unaweza kusema kuwa madongo yote tunayopigwa sisi wengine, ni kwa sababu tunaonekana tunaweza kuwa kikwazo kwa anayesafishiwa njia, ameeleza Sumaye.

Kama vijana wanawapigania watu ili nao wale, kama wao walivyosema katika tamko lao, “basi hata amani, usalama na mshikamano wa nchi, uko hatarini kwa kuwa, itakuwa ni kudra ya Mwenyezi Mungu kumpata kiongozi bora, kwa sababu tutakuwa tunampima anayetaka kuongoza si kwa uwezo wake wa uongozi, bali kwa uwezo wake wa kutushibisha matumbo yetu,” amesema.

Sumaye akionekana kujiandaa kujibu tuhuma moja baada ya nyingine amesema, “…Mimi sijaamua kugombea au kutogombea, lakini nina haki zote nikitaka kugombea. Na iwapo nitaamua kugombea, nitawaeleza wananchi kwa uwazi.”

Anasema wote wanaotaka urais tayari wanafahamika kwa kuwa wamejenga makundi na mabilioni ya shilingi yanatumika kusaka urais.

Waziri mkuu mstaafu aliwashukia pia Yusuf Makamba, katibu mkuu wa CCM na William Lukuvi, waziri ofisi ya waziri mkuu na mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

“Hawa wamendelea kunishutumu kwa kuongea nje ya vikao na kuhoji kwamba mimi niko chama gani ninaposema CCM ijibu mapigo ya CHADEMA. Wamesema yote yanayonifika nimejitakia, kwa sababu ya utovu wangu wa nidhamu wa kutokutumia vikao,” ameeleza Sumaye.

Ameuliza iko wapi mantiki kama amesemea kwenye vyombo vya habari na wao wakamjibu kutipita vyombo hivyohivyo lakini sasa wanamtuhumu kutumia magazeti badala ya vikao vya chama. “Tangu lini basi gazeti la Taifa Letu likawa ndio Kamati Kuu au NEC ya mheshimiwa Makamba na mheshimiwa Lukuvi?” anahoji.

Hata hivyo, Sumaye amesema alipoongea na Lukuvi, alikanusha taarifa hiyo na kusema hajawahi kuongea na mwandishi yoyote wa habari kutoka gazeti la Taifa Letu na wala hajawahi kusema maneno kama hayo dhidi yake.

Kuna mwandishi mmoja alinipigia simu aliniambia aliongea na Lukuvi, lakini simkumbuki, na kwamba sina haja ya kumkumbuka. Lakini kama alivyoyasema Lukuvi kwamba hajaongea na gazeti, basi namshukuru.

Sumaye amesema, hata hivyo, kuwa hana uhusiano mbaya na chama chake; UV-CCM; serikali yake wala viongozi wa ngazi yoyote serikalini na katika chama na kwamba alichosema ni kuwa “wananchi ndio wenye nguvu za mwisho za kuweka madarakani chama wakitakacho.”

“Baada ya kuona kazi ya kisiasa inayofanywa na CHADEMA ya maandamano na mikutano ya hadhara na kupokelewa kwa wingi sana na wananchi, huku CCM ikiwa bado ipo kimya… nikashauri, kwa nia njema kabisa kuwa CCM nayo ifanye kazi ya kisiasa kujibu hoja za CHADEMA badala ya kazi hiyo kuiachia serikali peke yake.”

Amesema, “Nilisema CCM ifanye kazi. Sasa hiki ni Kiswahili safi tu, maana nazungumzia chama. Sizungumzii watu. Nilisema chama changu kifanye kazi. Hii haimaanishi kuwa mimi simo kama walivyotafsiri baadhi ya wengine. Hapana. Nilitaka chama kifanye, kitume makada wake mikoani na wilayani kujibu hoja za CHADEMA. Hiyo ndiyo ilikuwa nia yangu.”

Sumaye anakana kusema kuwa serikali isifanye kazi. Badala yake alisema, “…tusiiachie serikali peke yake. Serikali ni chombo cha amri na maguvu na kama kazi ya siasa haijafanyika watu huishia kuikasirikia kwa kudhani inawaonea. Hapa atakayeadhibiwa au kukasirikiwa ni chama tawala; ndio utaratibu wa kawaida.”

Amesema malumbano ya kisiasa hujibiwa kwa malumbano ya kisiasa, ili umma uelewe kinachobishaniwa. Serikali huja kwa wakati wake kufanya kazi ya utawala, ikiona inabidi kufanya hivyo.

Kuhusu tuhuma kwamba matamshi hayo yalipaswa kutolewa ndani ya vikao vya chama Sumaye anasema, “Si kila jambo katika chama linahitaji lipelekwe katika vikao. Ukitaka kuwahimiza wanachama kulipa ada za chama unahitaji kupeleka agenda maalum katika kikao cha chama?”

Aliuliza, “Je, uhimizaji wa mikutano katika matawi, wilaya, mikoa na kata kunahitaji vikao maalum? Je, wenyeviti au wajumbe wa Kamati Kuu (CC) au NEC kufanya mikutano ya hadhara au ya ndani huhitaji ajenda au kibali kutoka katika vikao vya chama? Haihitajiki.

“Hizi ni kazi za kila siku za vyama vya siasa. Kwa miaka yote mwanachama akikumbushia jambo hili, haijawahi kuwa tatizo isipokuwa hapa sasa alipokumbushia Sumaye, ndiyo imeonekana utovu wa nidhamu. Ndivyo walivyotafsiri wale wote walionipinga na kunishutumu na wengine hata kunitukana,” ameeleza.

Amesema alilolisemea lilikuwa suala lililohitaji kushughulikiwa haraka bila kusubiri vikao. “CHADEMA wanaendelea na maandamano na mikutano, lakini sisi tunasubiri mikutano iitishwe ili tujadili kwenda kuwajibu au la… Katika siasa, muda ni suala la msingi sana,” anaeleza.

Sumaye alishambuliwa kwanza na Kaimu Katibu wa Kitengo cha propaganda cha CCM, Tabwe Hiza aliyemwita mchochezi na mtu anayevuruga chama.

Waliofuatia kumsulubu walikuwa UV-CCM mkoa wa Pwani ambao walisema Sumaye na Lowassa wana mpango wa kukivuruga chama na kukidhoofisha ili wafikie malengo yao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 (urais).

“Sasa mimi najiuliza: Unapotaka kupitia chama fulani kupata urais, hivi ndio unakazana kukidhoofisha au unakiimarisha?” anauliza Sumaye  na kuongeza kuwa “Lazima mtu mwenye akili timamu atajitahidi sana kukiimarisha kile chama ambacho anataka akitumie kwenda huko anapotaka kufika.”

Kuhusu kumtukana Rais Kikwete, Sumaye anasema, “Mimi sijawahi wala siwezi kuthubutu kumtukana rais wangu. Sijalelewa hivyo kutukana watu, na wala sijajifunza tabia hiyo mbaya ya kuweza kutukana, sembuse kumtukana rais wangu. Katika niliyoyasema, kama nilivyoyaeleza, hakuna mahali popote ambapo nimemtaja rais.”

Shutuma na tuhuma nyingine kwa Sumaye zimetoka kwenye kikao cha Baraza Kuu la UV-CCM kilichofanyika Dodoma. Kiongozi huyo amesema gazeti moja la kila siku (hakulitaja) liliandika, "UV-CCM kupambana na wakina Sitta, Sumaye."

Sumaye amesema, “taarifa ilisema, ‘Sisi vijana tunasema watu kama hao wasipewe nafasi kabisa katika chama hiki.’ Nasema tutapigana ndani na nje ya vikao vya chama kuhakikisha kuwa watu wa aina hiyo hawapati nafasi yoyote ya kuchaguliwa…msimamo ni kuwa hatutakubali kulala usingizi na kuruhusu watu hao wapewe nafasi.’”

Akiongea kwa mshangao, Sumaye amesema, “Yaani sisi tusipewe kabisa nafasi katika chama hiki? Chama hiki kipo hapa kwa sababu ya ushirikiano na mshikamano na kuheshimiana. Kama tangu zamani jumuiya yoyote ingefanya kazi kwa vitisho na ubabe, sidhani kama tungekuwa na CCM kama tunavyoiona leo.”

Amesema fikra kwamba mtu akiwa mwanachama au kiongozi katika chama basi hana uhuru wa kutoa maoni yake, si sahihi. Kama kiongozi hana uhuru wa kutoa maoni yake, basi hana sababu ya kuitwa kiongozi,” amesema.

Amesema kwa vile maoni mengine yanaweza kuwa na athari mbaya kwa chama, hasa kama yanakwenda kinyume na sera, itikadi au kanuni, ni juu ya kiongozi husika kupima kama ayasemayo ni salama, “bali lazima tukubali kwenye vyama vya kidemokrasia kama chetu, uhuru wa kutoa maoni nao lazima uwepo pamoja na kuwa utakuwa na mipaka ili mradi mipaka hiyo isiwe imeungana.”

Waziri mkuu mstaafu amesema ni muhimu kukubali kwamba wastaafu wana ujuzi ambao watu wanapenda kuutumia na hivyo wao kulazimika kusema, “lakini wanaposema sio kwamba wanahujumu chama au serikali. Hapana,” ameongeza.

Amesema demokrasia maana yake ni “chetu kwa ajili yetu. Tupende tusipende. Chochote ambacho watu wamekiweka lazima watakisema au kukisemea, na yote ni sahihi. Chama kama ni cha kidemokrasia, watakisema au kukisemea.”

Kama wamemchagua rais kidemokrasia, amesema Sumaye, watamsema au kumsemea. Kila  rais aliyepita alisemwa na kusemewa. Aliyeko sasa anasemwa na kusemewa na atakayekuja atasemwa na kusemewa.

“Mfumo au taasisi ambayo haisemwi au kusemewa ni ya kiimla; ni ya kidikteta. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ‘Waacheni waseme Mungu amewapa midomo ya kusema, wewe utawazuiaje?’ ”

Kuhusu kauli ya vijana kuwa Rais Kikwete anamjua rais ajaye, Sumaye amesema, “Binafsi siamini kama Rais Kikwete anamjua rais ajae labda kama chama chetu kimebadilika na kuwa cha kisultani. Lakini kwa CCM ninayoijua mimi, Kikwete asisingiziwe mambo ambayo najua hawezi kuyafanya.”

Amsema UV-CCM ikipinga chama, haoni uwezekano wa kuendelea kuwa na chama.

“Kumzuia mwanachama kugombea uongozi, kunaingiliana na haki za msingi za mwanachama. Ili chama chochote kiwe na uhai na uhalali, lazima kilinde haki za msingi za wanchama wake; moja ya haki kubwa kabisa ni kuchagua na kuchaguliwa.

“Kwa hiyo, huwezi kutangaza mtu fulani namzuia. Lazima azuiliwe na taratibu fulani za chama. Taratibu za chama zikimzuia, hiyo sawasawa lakini kwa mapenzi yako au kundi la watu fulani, hiyo si sahihi,” amesema.

Kuhusu hoja ya urais, Sumaye anaonya kuwa pamoja na kwamba makundi mengi yameundwa, lakini kama itadhihirika kuwa mgombea amepitishwa kwa njia chafu, rushwa kutenganisha watu, huyo hafai kuchaguliwa na sharti wananchi wamuache na kutafuta rais mwingine ambaye hataigawa nchi.

Amesema, “Tungependa kumpata rais ambaye ni mzuri, mchapakazi, mwadilifu anayefanya kazi kwa niaba na kwa ajili ya Watanzania. Hicho ndicho tunachotaka.”

Lakini ameonya kuwa, kwa yanayofanywa na vijana wa CCM, kupatikana rais bora kutoka ndani ya chama hicho, itakuwa ni kazi kubwa.

Miongoni mwa maswali ambayo Sumaye aliuliza ni pamoja na lililosema, “Watu wanasema, mtoto akitukana ametumwa na baba yake.” Sumaye alijibu, “Ni kweli, kwamba kuna huo msemo. Lakini mimi siamini kuwa vijana wale walitumwa na CCM. Hawa wamejituma wao wenyewe.”

Akijibu hoja ya kwa nini anaendelea kubaki katika chama hicho, huku tayari akiwa amejeruhiwa kwa maneno ya kejeli, Sumaye aliuliza, “Kwa nini nitoke? Hawa vijana ndiyo wananitoe katika chama. Haiwezekani.”

Juu ya taarifa kwamba vijana wanaomshambulia tayari wamejitambulisha kutetea kundi la watuhumiwa wa ufisadi au mafisadi wenyewe, Sumaye alijibu, “Sina hakika na hilo. Lakini nadhani wanatumwa.”

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: