Sumaye kasema kweli: CCM wajibu hoja za kisiasa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Gumzo

WAZIRI mkuu mstaafu, Fredick Sumaye amekirejesha darasani chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sumaye anaamini CCM hakijahitimu au kimepotea njia. Anataka kisome upya ili hatimaye kiweze kutunukiwa cheti cha ushindani katika mfumo wa vyama vingi.

Kama ni kujifunza, CCM bado kina umri wa kwenda shule – miaka 34 sasa; kwani Sumaye alipokwenda kusoma, Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani alikuwa na umri wa miaka 55 – baada ya kumaliza ngwe ya uwaziri mkuu kwa miaka 10 mfululizo.

Akizungumza na gazeti la kila siku la Mwananchi, Sumaye ameitaka CCM kujifunza kujibu hoja za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kisiasa, badala ya kuiachia serikali kupambana na chama hicho.

Amesema, “…CHADEMA wanafanya kazi za siasa, lakini CCM wamekaa kimya, wanataka serikali ndio ijibu hoja za CHADEMA. Hili si jambo zuri kwa kuwa chama kinapaswa kujibu kila hoja inayoelekezwa kwake. Kama hakina majibu kinatakiwa kuomba (hata) serikalini. Hiyo ndiyo kazi ya chama cha siasa kilichopo madarakani.”

Kauli ya Sumaye imekuja siku moja baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya CCM wa Habari na Uenezi, John Chiligati kuomba vyombo vya dola viwe imara kuwachulia hatua viongozi wa CHADEMA kwa kile alichoita, “…kutoa kauli hatari za kujaribu kughilibu akili za watu.”

Chiligati alisema, “CHADEMA kinaendeleza siasa za visasi; umwagaji wa damu na wanapanga njama za kutaka kuiondoa serikali iliyopo madarakani kwa nguvu kutokana na matamshi yao yanayochochea wananchi kuichukia serikali yao.”

Matamshi ya CHADEMA yanadaiwa kutolewa katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Kagera.

Aidha, kauli ya Sumaye imekuja wiki moja tangu Rais Jakaya Kikwete kulalamikia wimbi la maandamano na mikutano ya CHADEMA, ambapo maelfu ya wananchi wamekuwa wakijitokeza kuliko hata ilivyokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana.

Mbali na Chiligati, wapo wengine waliojitokeza kupinga maandamano na mikutano ya CHADEMA. Hao ni John Tendwa, msajili wa vyama vya siasa; Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki, Agustine Mrema mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), na John Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa United Democrat Party (UDP).

Cheyo na Mrema wanafahamika. Tayari wamemaliza vyama vyao na sasa wanaishi kwa baraka za CCM. Naye Tendwa anajulikana jinsi alivyo mahiri wa kutetea CCM. Kuna wakati Tendwa anafanya kazi za CCM kuliko viongozi wakuu wa chama hicho.

Naye Kilango, hawezi kujilinganisha na viongozi wa CHADEMA katika ushupavu wa kutetea rasilimali za taifa. Hadi anatoa kauli ya kupinga maandamano, Kilango alikuwa hajajibu tuhuma zilizotolewa na Sophia Simba, alipokuwa waziri wa nchi, ofisi ya rais (Utawala Bora), kwamba yeye (Kilango) na mumewe John Malecela, walinufaika na fedha za EPA.

Simba alisema, Kilango alinufaika na fedha hizo zilizoibwa na Jeetu Patel, kwa maelezo kwamba alifadhili kampeni za urais wa mumewe mwaka 2005. Kilango hajawahi kujitetea na kujiaminisha kwa jamii kuwa haikuwa hivyo.

Kimsingi kila aliyesikiliza wote waliojitokeza kupinga kazi za kisiasa za CHADEMA, amebaini haraka kuwa Sumaye amegundua tatizo linalokikabili chama chake. Kwamba hakina makada wa kukisemea na kukitetea; hawana ujasiri wala mkakati.

Msingi wa kauli ya Sumaye ni kwamba, “…kazi za kisiasa hufanywa na chama cha siasa na hujibiwa na wanasiasa.” Sumaye anajua kuwa si kazi ya serikali kujibu hoja za kisiasa. Wajibu mkuu wa serikali ni kutawala.

Ndivyo ilivyofanyika kwenye maandamano na mikutano ya CHADEMA iliyomalizika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria. Ndivyo ilivyofanyika pia katika mikutano na maandamano ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, 5 Februari 2011.

Katika maelezo yake, Chiligati amesema, chama chake hakiogopi kukosolewa; lakini akataka CHADEMA watumie bunge kukosoa serikali, badala ya utaratibu wake wa mikutano ya hadhara na maandamano.

Hapa Chiligati atakuwa anataka kujipa kazi nyingine. Kazi ya kupangia CHADEMA jinsi ya kutenda shughuli zake. Lakini Chiligati anajua kuwa hiyo si kazi yake na CHADEMA hawatamruhusu kuwaandalia taratibu wala ratiba.

Chiligati anasema pia kwamba CHADEMA imekuwa ikiwapotosha wananchi kuwa “serikali na CCM tayari wameamua, tena kwa furaha, kuilipa Dowans Sh. 94 bilioni” kutokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Biashara (ICC).

Anasema huo ni uzushi na uchochezi kwa sababu suala hilo, serikali pamoja na CCM, wamekuwa wakisisitiza isilipwe na ifanyike mikakakti ya kisheria ya ama kuliondosha kabisa au kulipunguza.

Wakati Chiligati akieleza hayo, wananchi bado wanakumbuka kauli yake, kuwa kamati kuu (CC) ya chama chake “imeridhia malipo hayo kufanyika.” Kile ambacho anashabikia leo, ni uamuzi wa kamati ya wabunge wa CCM iliyotaka serikali isitishe malipo hayo hadi hapo kesi itakapokuwa imesikilizwa. 

Je, Chiligati anataka kueleza kuwa mkutano wa wabunge wa chama, unaweza kufuta maamuzi ya CC ya chama? Kama ndiyo, basi CCM itakuwa na matatizo makubwa zaidi ya haya tunayoyafahamu.

Kinachotatiza viongozi wengi wa CCM, ni hatua ya CHADEMA kuanika wezi wa mali ya umma. Hili ndilo Chiligati anaita “Tatizo ni lugha na kauli za upotoshaji na za kuchochea vurugu, ghasia na uvunjaji wa sheria.”

CHADEMA wanafanya kazi ambayo CCM imeshindwa kufanya. Wanawapeleka wezi, mafisadi, waongo ndani ya serikali na viongozi dhaifu wasiochukua hatua, katika mahakama ya wananchi. Wanawaeleza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kukamata, hata kuhoji wezi na mafisadi wakuu.

Kwa mfano, katika mkutano wake mkoani Shinyanga, katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa ameeleza wananchi kuwa anayesababisha matatizo yote haya ya ukosefu wa umeme, ni Rostam Aziz. Amesema Rostam ndiye aliyeingiza Dowans nchini kwa baraka za Edward Lowassa, ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu.

Wananchi wakauliza, “Huyo Rostam Aziz ni nani?” Dk. Slaa akajibu, Rostam ni mjumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na mbunge wa Igunga kupitia CCM. Akasema Rostam si mwanachama wa kawaida ndani ya chama hicho bali “Rostam ni swahiba mkuu wa Rais Kikwete.”

Kupitia mkutano huo wananchi wakaelewa wizi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa katika Benki Kuu ya Taifa (BoT). Viongozi wa CHADEMA, kila walikopita, walifafanua juu ya wizi mkuu serikalini na ndani ya BoT na hasa zaidi ya Sh. 40 bilioni kupitia kampuni ya Kagoda.

Wananchi wakafahamu jingine. Kwamba mabilioni mengine ya shilingi yaliyokwapuliwa kupitia ununuzi wa rada, yanahusishwa na aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge.

Dk. Slaa akataja vyeo vya Chenge kuwa ni mjumbe wa CC, mbunge wa Bariadi Magharibi na mjumbe wa kamati ya maadili ya CCM. Hivyo ndivyo ziara ya CHADEMA imekuwa ya kusambaza taarifa kwa wananchi.

Kabla ya Rais Kikwete na Chiligati kukimbilia kulaumu CHADEMA ni muhimu kwanza wangejiuliza maswali yafuatayo: Kwanza, si kweli kwamba serikali yake imeshindwa kutatua matatizo ya wananchi?

Kwa mfano, matatizo ya umeme yaliyoanza tokea mwaka 1994 - miaka 17 iliyopita. Pamoja na kelele za wananchi, hili limeshindwa kufanyiwa kazi.

Badala yake, katika kipindi chote cha miaka sita ya utawala wa Kikwete, serikali imeshindwa kununua mitambo yake yenyewe, badala yake imebaki kupigia magoti Rostam kupitia mtambo wake wa Dowans. Mwenye kujali anauliza, “Kuna nini hapa?”

Matokeo yake, rais analazimika kukana kila uchao; “…simfahamu mmiliki wa Dowans, wala sijawahi kukutana naye,” jambo ambalo limemfanya Rostam kuleta mtu nchini ambaye alimwita, na yeye kujitambulisha, kuwa ndiye mmiliki wa Dowans.

Wachunguzi wa mambo wanasema mkakati wa kumleta nchini anayejiita mmiliki wa Dowans, Sulaiman Al Adawi, kutakuwa kulilenga mambo mawili makubwa.

Kwanza, kumuumbua Rais Kikwete ambaye alidai kuwa hamfahamu mmiliki wa Dowans ili asiweze tena kuibuka na kusema hafahamu lolote kuhusu Dowans. Pili, kulilenga kumtoa Rostam katika gome la Dowans.

Wakati hili la kutaka kumnyamazisha rais linaweza kufanikiwa, lile la kumwondoa Rostam katika utata wa Dowans haliwezi kufanikiwa. CHADEMA wanafanya kazi ya kulifafanua, miongoni mwa mengi wanayofafanulia wananchi.

Hivyo wenye nia safi wanadiriki kusema kuwa kama CCM ingekuwa chama kinachotaka tena uongozi wa nchi, basi wangekiacha CHADEMA kiseme yote ili chenyewe kipate nafasi ya kuyafanyia kazi na kujirekebisha, ikiwamo kuwaondoa ndani ya chama chao watuhumiwa wakuu wa ufisadi.
    
Kwani hata kama CHADEMA watanyamazishwa leo, wananchi tayari wamepata kuelewa kuwa kuna ghiliba. Inawezekana vipi kuwa na dharura ya umeme kwa miaka sita yote ya kipindi cha kwanza cha Rais Kikwete?

Hata mitambo inayoleta kero iliwasili nchini wakati mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme yakiwa tayari yamejaa. Kwa muda wote huo, serikali ilikuwa inachukua hatua zipi kuondokana na kiza? Ni mambo ya utata mtupu.

Sauti za CHADEMA na wananchi haziwezi kuzimwa kwa vitisho kwa kuwa ukweli uko wazi. Ushauri katika ujumbe wa CHADEMA na wananchi hauna maana ya kumchagulia rais marafiki. Wala!

Ni kwamba kwa ustawi wa utawala wake, Kikwete hana budi kuachana na urafiki wa Rostam kwa kuwa Rostam anahusishwa na Dowans na Dowans inahusishwa na Kagoda; na kwa kuwa Dowans inahusishwa na Richmond; na kwa kuwa Richmond inahusishwa na Edward Lowassa; na kwa kuwa Lowassa anahusishwa na Kikwete na Kikwete anahusishwa na Rostam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: