Sura mbili tofauti za Samwel Sitta


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyemaliza muda wake, Samwel Sitta ameomba “kuvaa viatu” vya Jakaya Kikwete kupambana na Dk. Willibrod Slaa katika mdahalo juu ya utoaji elimu na afya bure kwa wananchi.

Sitta, ambaye ni mgombea ubunge katika jimbo la Urambo Mashariki, mkoani Tabora, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anadai kuwa sera ya utoaji bure huduma ya elimu na afya ambayo Dk. Slaa ameishikia bango, haitekelezeki.

Anataka CCM imruhusu kupambana katika mdahalo na Dk. Slaa. Lakini CCM imekataa.

Hivi Sitta hajui anachokisema Dk. Slaa kuhusu elimu na afya au anataka kubisha kwa sababu yeye ni mwana CCM?

Kwanza, Sitta na wenzake wanajua kwamba taifa hili limesheheni utajiri, rasilimali na limebahatika kuwa na vitu vingi ambavyo havipatikani kwa wengine.

Pili, anajua kwamba kinachokosekana ni umakini katika maamuzi na usimamizi mbovu wa rasimali za taifa.

Miongoni mwa waliobahatika kupata elimu ya bure wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni Samwel Sitta ambaye leo anapinga mpango wowote wa ukombozi wa kurejesha elimu bure.

Anasema, “Hatua hiyo itasababisha bajeti yote kuteketea katika sekta ya elimu.” Ningeelewa kama nisingewafahamu baadhi yao, hasa jinsi wanavyoponda anasa kwa kutumia raslimali za taifa.

Spika Sitta anaelewa vizuri kuwa kinachosemwa elimu ya bure siyo bure kama yeye na wenzake wanavyotaka kuaminisha wananchi.

Anachosema Dk. Slaa ni kwamba akiridhiwa kuwa rais wa nchi hii, watoto wote watasoma kwa gharama itakayolipiwa kodi na wazazi wao kama Sitta na wenzake walivyosoma kwa kodi ya wazazi wao.

Dk. Slaa anasema hili litawezekana kama serikali itajiepusha na matumizi ya hivyo kama yale ambayo Sitta alitengeneza ikiwamo kuangalia malalamiko ya mbunge wa Mkuranga, Adam Malima na mfanyabiashara Reginald Mengi.

Kamati ilitumia zaidi ya Sh. milioni 100. Lakini ilishindwa kumchukulia hatua Malima ambaye ilithibitika kwamba alisema uwongo bungeni.

Jiulize, kulikuwa na sababu gani kuunda kamati ambayo ripoti yake haikutumika? Sh. 100 milioni zingesomesha wanafunzi wangapi? Hiyo haikutosha.

Akaunda kamati feki teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza kashfa ya Richmond. Wajumbe wake wakazunguka ndani na nje ya nchi kutafuta ushahidi.

Ushahidi ukapatikana. Mwizi akajulikana. Bunge la Sitta likakubali kumtupia uovu wote mtu mmoja, ikagawa ushahidi nusu; ikauwasilisha bungeni nusu na mwingine ikabaki nao mpaka leo.

Kamati hiyo ilitumia zaidi ya Sh 500 milioni. Je, fedha hizo zingewasomesha watoto wetu wangapi kama zisingetumika vizuri? Ni kiasi gani cha fedha kingeokolewa, kama Sitta asingekubali kurudi nyuma hadi serikali kuwajibisha waliotuingiza mkenge?

Sitta na wenzake waliwaambia Watanzania kuwa kila siku iliyokuwa inakwenda kwa Mungu, serikali ilikuwa inailipa Richmond/ Dowans Sh. 152milioni.

Kama serikali ingemudu kulipa Sh. 152 milioni kila siku kwa muda wa miaka miwili ya mkataba, ni kiasi gani cha fedha kingetumika? Tukipata serikali isiyo na ufisadi kama huu ni mwanafunzi gani atakosa kusoma bure?

Anachoshangaa Sitta wanafunzi kusoma bure ni kipi? Ana makazi Dodoma na mengine Dar es Salaam. Nyumba moja serikali inalipa pango dola 10,000 kila mwezi (sawa na Sh. 15 milioni kwa mwezi).

Je, kama angekaa katika nyumba yake ambayo ameuziwa na serikali, angeokoa kiasi gani ambacho kingetosha kulipia masomo ya watoto wetu? Kiasi hicho cha fedha kinatosha kununulia vitabu vingapi?

Ni Sitta huyu na wenzake walipigania kinachoitwa leo, “Mfuko wa Jimbo” ambao ni aina nyingine ya unyang’anyi wa fedha za umma.

Je, hizi fedha ambazo Sitta na wenzake wanazitapanya kwa kuzigawa kama rushwa kwa wabunge, zinatosha kujenga shule ngapi kwa kila wilaya? Zinanunua vitabu vingapi?

Slaa anasema kuwa mshahara wa mbunge ukichanganywa na marupurupu mengine unafikia Sh. 7 miloni kwa mwezi. Hivi, ukipunguzwa ufanane na watumishi wengine, fedha zinazobaki zingewasomesha wanafunzi wangapi?

Posho ya mbunge kwa siku moja hata kama anasinzia tu bungeni ni Sh. 180,000 zaidi ya mshahara wa mwalimu kwa mwezi.

Yeye mwenyewe kwa muda wote huu amekuwa akipokea Sh. 2,500 pesa za walipa kodi kwa kuidanganya serikali kuwa ndiyo bei ya lita moja ya mafuta anayonunua, wakati hakuna mahali nchini ambapo mafuta yamefikia bei hiyo.

Bado Spika alitetea ufisadi mwingine wabunge kuchukua posho mbilimbili kwa kazi moja. Katika eneo hili, mawaziri wanalipwa na serikali na bunge.

Hata madereva wanalipwa hivyo. Je, huu si ufisadi? Ni kiasi gani cha fedha kingeokolewa? Fedha hizo zingesomesha wanafunzi wangapi bure? Je, hakitoshi kusomesha bure watoto wetu?

Fedha hizi ni kodi ya wananchi inayofujwa na kuibwa kifisadi. Mgombea urais akisema atahakikisha ufisadi huu wa watu hawa unadhibitiwa ili fedha hizo zisomeshe watoto wetu bure, Sitta anashangaa nini?

Ni Sitta aliyezuia mijadala ya Meremeta, Tangold, EPA hata mafisadi wa elimu kujadiliwa bungeni. Bila ufisadi wa rada, ndege ya rais, IPTL ni mwananchi gani asingetibiwa bure?

Spika wa Bunge anayeongoza Bunge lisilo na uwezo wa kuhoji kwa nini nchi ipate asilimia tatu katika madini, hana ubavu wa kusema kwamba elimu haiwezi kutolewa bure.

Bado katika hizo hizo asilimia tatu anakuja mtu anaitwa Alex Stuart anachukua asilimia 1.1. Bunge linaruhusuje ufisadi huu?

Ni muhimu Sitta akasema jingine, kuliko hili la kupinga utoaji bure wa elimu. Katika hili, wale wanaojua jinsi serikali inavyotafuna fedha za walipa kodi kama zile zinazoteketea katika aafari zisizo tija za Kikwete, wengi watamdharau Spika Sitta.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: