Sura mbili za matatizo ya walimu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version

LENGO kubwa la kugatua madaraka ya usimamizi wa shule za sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hadi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilikuwa kusogeza huduma karibu.

Kuiondolea wizara mzigo mkubwa wa kushughulikia shule za sekondari na vyuo vya elimu na ufundi. Kama ilivyo kwa shule za msingi, serikali iliona busara kuzirejesha shule hizo mikononi mwa Tamisemi.

Lengo halijakamilika; malalamiko ya walimu, hasa wapya, bado hayajamalizika. Walimu wengi walioajiriwa katika shule za mkoani Shinyanga na halmashauri ya wilaya ya Kilosa, wameambulia mshahara wa hisani wa Sh. 100,000 badala ya kati ya Sh. 380,000 na Sh. 500,000.

Wamepewa taarifa kwamba huenda hata mwezi huu, walimu hao watalipwa mshahara wa hisani wa Sh. 100,000 kutokana na kilichodaiwa kuwa majina yao hayamo kwenye daftari la malipo.

Pamoja na walimu waliojikusanya kwenye ofisi za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na wengine katika wilaya ya Kilosa, waliishia mwanzoni mwa mwezi huu kupata kifuta jasho cha Sh. 100,000 tu kila mmoja.

Tatizo hilo limekuwepo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa miaka mingi na sasa limerithishwa Tamisemi.

Kwa nini walimu tu ndio wanasumbuliwa hivi? Kwa nini haujapatikana ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya walimu? Kilichogatuliwa ni usimamizi au matatizo?

Jambo lililowazi ni kwamba mwalimu mwenye matatizo hawezi kufundisha kwa ari na uwezo wake wote, na pia hawezi kuwa na mapenzi na kazi.

Mambo mengine yanayokatisha tamaa walimu na hata kuwafanya wajilaumu kuchagua kazi hii ya kuelimisha vijana ni kama nilivyowakuta walimu wa Shule ya Sekondari Bulyanhulu.

Nilipotembelea shule hiyo Machi 8, 2011 niliwakuta walimu watatu—mkuu wa shule msaidizi, Henry Mnungu; mwalimu wa Historia, James Christopher Masatu, na mwalimu Jografia, Faith Kanyi – wakiwa kwenye darasa lililogeuzwa ofisi ya walimu.

Ugumu wa maisha, udogo wa mishahara, mzigo mkubwa wa kazi na majukumu mengine vinaonekana wazi katika mahojiano. Shule hiyo iliyoanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2007 imefelisha zaidi ya nusu ya wanafunzi mwaka jana.

Kati ya wanafunzi 53 walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, mmoja alipata daraja la pili; wawili daraja la tatu, 18 daraja la nne na 32 ubuyu.

Mnungu anasema matokeo hayo mabaya yamechangiwa na matatizo mengi lakini kubwa ni uhaba wa walimu. Shule hiyo yenye wanafunzi karibu 600 sasa ina walimu wanne wa kuajiriwa na wanne wa kujitolea.

Walimu hao wote wanne wa kuajiriwa ni wa masomo ya sayansi jamii yaani sanaa wakati walimu wa kujitolea ambao ni wahitimu wa kidato cha sita, ndio baadhi yao wanafundisha masomo ya sayansi.

Mwalimu wa Jografia, Faith Kanyi anafafanua kwamba walimu hao wa kujitolea wanaweza kuondoka wakati wowote kwa vile wanasubiri ajira zikipatikana kwenye mgodia wa dhahabu wa Bulyanhulu au kazi ya kudumu sehemu nyingine.

Masatu anataja matatizo mengine ya ukosefu wa maabara na vifaa vya kufundishia na kubadilishwa mara kwa mara kwa muhtasari.

Mabadiliko ya mihutasari ya masomo huwa na athari kubwa kwani walimu wanaokuwa wamepewa mafunzo na muhtasari wa awali huwa hawajui muhtasari mpya, hivyo hufundisha kwa kubabaisha.

Shule ina jumla ya vitabu vya kiada na ziada 907 huku kukiwa hakuna nyumba za walimu, maji, matundu manane ya vyoo na chumba kimoja kikitumika kama stoo. Mazingira haya yanahatarisha elimu ya vijana nchini.

0776 383 979
0
No votes yet