Sura mbili za Rostam Aziz


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly version
Huku anang'aka, kule anadoda
Rostam Aziz

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limemzuia mbunge wa Igunga na mfanyabishara Rostam Aziz, kuwasilisha hoja yake bungeni.

Kamati ya Uongozi ya Bunge, imesema hoja ya Rostam haiwezi kuwasilishwa bungeni kwa sasa kutokana na "kwenda kinyume" na Kanuni za Bunge.

Imefahamika sasa kwamba Rostam, katika hoja yake, hakuwa anajibu hoja aliyotakiwa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kinyonyaji kati ya serikali na kampuni ya Richmond, bali aliibuka na mashambulizi dhidi ya kamati hiyo na hasa Mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe.

Bunge katika mkutano wake wa kumi, lilimtaka Rostam athibitishe au akanushe madai yake kwamba Kamati Teule ilikuwa inaendelea kufanya kazi hata baada ya kuwa imekabidhi ripoti yake kwa Spika.

Jumatano iliyopita, Rostam aliwasilisha kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta, kile alichokiita "Maelezo binafsi kuhusu hoja ya Dk. Harrison Mwakyembe."

Katika maelezo yake ya kurasa nne yalioandikwa 9 Aprili 2008, Rostam anaishambulia Kamati Teule akisema ilipika tuhuma.

Ukiisoma kwa makini barua ya Rostam, mara moja utabaini kwamba hakuwa na majibu ya kile alichotakiwa kueleza na Kamati ya Dk. Mwakyembe.

Ujumbe mzima unaoonekana katika hoja yake ni kile wengi wameita "matusi, dharau na kebehi kwa Bunge na Kamati yake."

Bunge lilitaka Rostam afanye mambo mawili: Kwanza, kukana au kuthibitisha kushiriki kwa kampuni yake katika umiliki wa Richmond/Dowans, na pili, kuthibitisha Kamati Teule kufanya kazi baada ya ripoti yake kuwasilishwa kwa walioiunda.

Kauli yake inadaiwa kulenga hoja kuwa Bunge lilikuwa na ripoti mbili: Moja ilikuwa ile iliyowasilishwa kwa Spika mwishoni mwa muda wa Kamati wa kufanya kazi; na nyingine iliyosomwa bungeni.

Sasa Rostam hajajibu lolote kati ya hayo mawili. Hajakana au kukubali uhusiano wake na Richmond/Dowans; wala hajafafanua taratibu za kuandaa ripoti.

Tujadili hili la kuwasilisha ripoti. Kuwasilishwa kwa ripoti maana yake ni kuwasilisha kwa Bunge lililounda Kamati. Muda wowote kabla ripoti haijasomwa bungeni, ambako ndiko kuwasilishwa kwa wadau, yaweza kufanyiwa marekebisho kwa shabaha ya kuiboresha.

Taarifa inabaki kuwa ya Kamati, hadi pale inaposomwa bungeni na Kamati inaweza kuondoa na, au kuongeza chochote inachoona kinafaa kwa madhumuni ya kuiboresha.

Hapo ndipo Rostam alikwama. Kilichositishwa ni gharama za wajumbe wa Kamati, lakini uboreshaji wa ripoti, unaofanywa na wahusika wenyewe, na wakati ikiandaliwa vema kwenda kwa waliounda Kamati, hauwezi kuwa dosari.

Rostam, kwa kile baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM wanaita matusi, dharau na kebehi kwa Bunge na Kamati yake, hajajibu hoja wala hawezi kuepuka kibano.

Kwa kutaka kumuokoa na kumlinda Rostam, wajumbe wa Kamati ya Uongozi, walimueleza wazi kuwa, "Hoja yako inakiuka Kanuni za Bunge."

Walimfahamisha kuwa Kamati ya Uongozi haiwezi kupeleka bungeni hoja ile kwa vile ilikuwa ikijadili jambo jipya ambalo walisema lingesababisha ubishi na walioshambuliwa kuhitaji kujitetea. Rostam hakukubali ushauri, MwanaHALISI limeelezwa.

Habari za ndani ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya bunge zinasema Rostam alizua zogo katika kikao, alifoka na kung'aka na hatimaye kutishia kujiuzulu ubunge.

Haijafahamika iwapo tishio lake la kujiuzulu lilitoka moyoni, au alikuwa anatingisha kiberiti.

Kamati ya uongozi inaundwa na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Spika wa Bunge, Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni (Waziri Mkuu), Katibu wa Bunge na Kiongozi wa Upinzani bungeni.

Hapa ndipo baadhi ya wabunge wanasema Kamati ya uongozi ilikosea. Wanasema ingemruhusu Rostam kuwasilisha kile alichotaka, hata kama kwa kufanya hivyo ingekiuka kanuni ya 54 ya Bunge.

Ibara hiyo inasema, "hoja ambayo, kwa maoni ya spika ina lengo la kutaka jambo ambalo lilikwisha amuliwa na Bunge katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita kabla ya kikao kinachoendelea lifikiriwe tena, haitakubaliwa na spika, isipokuwa tu kama ni hoja ya kutaka uamuzi wa Bunge uliokwishafanyika ubadilishwe."

Inaaminika kuwa kwa kuruhusu Rostam awasilishe "kitu" chake, umma ungepata fursa adhimu ya kuthibitisha sura halisi ya mbunge huyo; na kwa hatua yake ya kuponda kazi za Kamati, wabunge wangepata fursa ya kumuhoji anahusika vipi na kampuni ya Richmond?

Je, madai ya Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salva Rweyemamu, kwamba ni yeye aliyemtambulisha kwa Mohammed Gire (mkurugenzi mtendaji wa Richmond Development Corporation (RDC), yana ukweli kiasi gani? Nani anasema kweli hapa, kati yake na msaidizi wa rais?

Anaifahamu vipi Dowans? Kwa nini Dowans wanatumia anuani zake? Kwa nini yeye ndiye anayetajwa kufuatilia malipo ya Dowans hazina, na pale serikali inapochelewa kutoa fedha, mara moja anang'aka.

Labda muhimu zaidi ni anapata wapi nguvu na ujasiri wa kuing'akia serikali pale anapokuwa hajalipwa? Ana siri gani na serikali?

Rostam analeta kile anachoita "utetezi" zaidi ya miezi miwili baada ya Kamati teule kumaliza shughuli zake. Anasema alikuwa safarini wakati Kamati ilipomuita kumhoji.

Kwa nini basi Rostam hakwenda kwenye Kamati mara aliporejea na wakati Kamati ilikuwa haijafunga kazi zake.

Kama bunge lingemruhusu Rostam kuwasilisha "kitu" chake, angekaangwa kwa maswali iwapo kampuni ya Richmond haikuwa kampuni hewa; mkataba wake haunyoji uchumi wa taifa; na kwamba kauli ya Nazir Karamagi bungeni, kwamba Richmond ilikuwa "kampuni ya kitapeli" haikuwa ya kweli.

Rostam ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni katika vikao hivi, ambavyo Kikwete ni mwenyekiti, ndiko hoja ya Richmond iliwasilishwa na kujadiliwa kwa mapana. Ripoti ya siri ya Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM ambayo ilichapishwa katika gazeti hili wiki iliyopita, inapongeza kazi nzuri ya Kamati teule ya Bunge.

Ndani ya vikao hivyo, Rostam hakuthubutu kunyoosha mkono. Alijifanya mnyenyekevu ili kuzima moto wa upinzni dhidi yake mbele ya mwenyekiti Jakaya Kikwete.

Bado Rostam ana deni kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Je, Kikwete anayajua hayo ya rafiki wake wa karibu zaidi? Anajua kwamba rafiki yake huyo ana sura mbili tofauti?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: